Atuhumiwa kuua mmoja, kujeruhi wawili kwa mshale baada ya kunyimwa bia

Kamanda wa polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki

Muktasari:

  • Polisi mkoa wa Mara nchini Tanzania, linamtafuta kijana mmoja ambaye hajafahamika jina lake kwa tuhuma za mauaji na kujeruhi wawili kwa kile kinachoeleza alitekeleza tukio hilo baada ya kunyimwa bia.

Serengeti. Kijana mmoja (jina halijajulikana) ameibua taharuki katika Kijiji cha Kwitete Wilaya ya Serengeti mkoani Mara nchini Tanzania baada ya kutuhumiwa kuua mtu mmoja na kujeruhi wawili akiwemo baba yake wa kambo kwa sababu ya kunyimwa bia.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki jana Jumatatu Julai 29, 2019 alithibitisha kuwa tukio hilo limetokea Jumapili Julai 28, 2019 kijijini hapo na mtuhumiwa amekimbia wanaendelea kumsaka.

Amesema aliyefariki ni mgeni hajatambulika jina, lakini kabila lake ni Msukuma ambaye aliongozana na mtu mwingine kwenda kwenye mji huo kwa ajili ya kumsalimia mama mwenye mji ambaye pia ametoroka na kijana wake.

Ndaki amesema walinunua kreti ya bia wakati wanakunywa, mtuhumiwa alipewa chupa mbili alipotaka tena wakamnyima ndipo akaingia ndani na kutoka na upinde na kuanza kuwashambulia na kusababisha mauaji ya mtu mmoja na kujeruhi wawili.

Mmoja wa wahudumu wa Hospitali Teule ya Nyerere ambaye hakutaka kutaja jina lake, amethibitisha kupokea mwili wa mtu anayedaiwa kupigwa mshale ambao umeletwa na polisi wa wilaya ya Serengeti na uchunguzi utafanyika baada ya ndugu kujitokeza.