Basi lililobeba wanafunzi lagonga treni, mmoja afariki, 30 wajeruhiwa

Muktasari:

  • Ajali ya basi aina ya Coaster kuligonga treni imetokea leo Ijumaa saa 10 jioni katika njia panda ya Dolphine jijini Tanga na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wanafunzi 30 kujeruhiwa

Tanga. Mtu mmoja amefariki papo hapo na wengine 30 kujeruhiwa baada ya basi aina ya Coaster lililokuwa limewabeba wanafunzi kugonga treni katika njia panda ya mtaa wa Dolphine jijini Tanga.

Basi hilo lililokuwa limebeba wanafunzi wachezaji pamoja na washangiliaji zaidi ya 30 liliweza kuburuzwa umbali wa mita 50 kutoka eneo ilipotokea ajali .

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe akizungumzia ajali hiyo iliyotokea leo Ijumaa Machi 15, 2019 amemtaja aliyefariki katika ajali hiyo kuwa ni kondakta wa basi hilo ambaye jina lake halijatambulika mara moja.

Majeruhi waliofikishwa hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo ni wanafunzi 30 ambapo 19 kati yao hali zao si nzuri na madaktari wanaendelea na kuwapa matibabu.

Mwananchi limeshuhudia jinsi majeruhi walivyokuwa wakinasuliwa kwenye mabati ya basi hilo huku wananchi wakimiminika katika Hospitali ya Bombo kuwatambua wanafunzi majeruhi.

Katika Hospitali ya Bombo askari wa jeshi la polisi walilazimika kuingilia kati kuwazuia wananchi waliokuwa wakiminyana kutaka kuwaona majeruhi.

Umati huo ulitulia baada ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella kuwasihi wananchi kuwaachia nafasi madaktari ili waweze kufanya kazi yao ya kuwatibu majeruhi kwa nafasi.

Amesema kutokana na kuzidiwa nguvu madaktari pamoja na wauguzi wa hospitali hiyo, ameomba madaktari kutoka hospitali za binafsi pamoja na vituo vya afya vya jirani kwenda kuongeza nguvu ili wanafunzi hao waweze kuhudumiwa ipasavyo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Bombo, Dk Jumanne Karia amesema baada ya kupokea majeruhi hao kazi inayofuata ni kuwapeleka katika vipimo majeruhi wote ili kubaini kila mmoja ameumia wapi na anahitaji matibabu ya aina gani.

Mkuu wa Shule ya  Sekondari Horten, Eugenia Kinamboi amesema wanafunzi hao walikuwa wakielekea Shule ya Sekondari Masechu kwenye mashindano ya mchezo wa soka ikiwa ni sehemu ya masomo.

Hata hivyo, Kamanda Bukombe amesema dereva wa basi hilo alikimbia baada ya kutokea ajali hiyo na kwamba jeshi la polisi litamsaka ili aweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu shitaka la kusababisha ajali.