Dk Mpango ataka ripoti ya IMF iliyovuja kupuuzwa

Friday May 10 2019
IMFPIC

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango

Dodoma. Baada ya Serikali ya Tanzania kuwasilisha maoni yake Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amewataka wananchi kutoizingatia ripoti iliyovuja ya shirika  la Fedha Duniani (IMF).

Mpango amesema hayo leo Ijumaa Mei 10, 2019 bungeni jijini Dodoma alipokuwa anampa taarifa mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde aliyeinukuu ikionyesha uchumi wa Tanzania unakua kwa wastani wa asilimia nne.

“Hii niliyoshika ni ripoti ya IMF. Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) inakadiria uchumi wa Tanzania atakuwa kwa asilimia 6.8 na Benki ya Dunia inakadiria uchumi wetu utakua kwa asilimia 6.6 mwaka 2019. Hiyo taarifa unayoitumia ni ile iliyovuja,” amesema Dk Mpango.

Waziri huyo ametoa taarifa hiyo kufafanua hoja ya Silinde aliyetaka kujua kwa nini fedha nyingi zinaelekezwa kwenye sekta ya ujenzi na uchukuzi lakini kasi ya ukuaji wa uchumi haiongezeki.

Silinde amesema uwekezaji usio wa kimkakati ndio unaosababisha mafanikio kutoonekana kwenye uchumi licha ya fedha nyingi kuwekezwa kwenye sekta hiyo.

“Ripoti ya IMF inaonyesha uchumi wetu utakua kwa asilimia 4.4 mwaka 2019,” alisema Silinde akihoji kwa nini hali hiyo inatokea wakati ukuaji ulikuwa wastani wa asilimia saba kwa muongo mmoja uliopita na kumlazimu Dk Mpango kutoa ufafanuzi huo.

Advertisement
Advertisement