Fursa mpya marufuku ya mifuko ya plastiki

Wadau wa mkutano wa wazalishaji na wauzaji wa mifuko ya plastiki wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makumu wa Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao

Muktasari:

  • Makamba alifafanua kuwa katazo hilo linahusu mifuko ya plastiki inayotumika kubebea bidhaa mbalimbali zinazouzwa madukani na halitahusu vifungashio vya maziwa, dawa, korosho na pembejeo.

Dar/Moshi. Wakati Serikali ikisisitiza kuwa haitarudi nyuma katika uamuzi wake wa kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki kuanzia Juni Mosi, baadhi ya wazalishaji wamesema kuna fursa mpya ya kuendeleza kipato chao.

Jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), January Makamba alisema wanaodhani kuwa Serikali itagwaya kuhusu marufuku hiyo wamefeli kwa sababu hawatauacha msimamo huo.

Alitoa kauli hiyo jana kwenye kikao kilichowakutanisha watendaji wa Serikali, wazalishaji na wauzaji wa mifuko mbadala jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki, Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Joseph Sokoine na wadau kutoka Zanzibar, Makamba alisema, “kuna watu wanatumwa kusema kwamba muda uliotolewa hautoshi. Wengine ni wanyonge wanadhani wakizungumza Serikali itawahurumia. Uamuzi huu hautobadilika.”

Akiwa bungeni Aprili 9, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitangaza kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo kuanzia Juni Mosi.

Kusisitiza utekelezaji wa msimamo huo wa Serikali, Makamba alisema marufuku hiyo ilikuwapo tangu mwaka 2017 lakini sakata la viroba liliingilia kati. Machi Mosi mwaka huo, Serikali iliendesha msako wa pombe za viroba baada ya kuwataka wazalishaji kucha uzalishaji wake.

“Hakuna mjadala tena kuhusu mifuko ya plastiki, atakayezungumza anatuchelewesha kwa sababu athari zake zinajulikana,” alisema Makamba.

Makamba alifafanua kuwa katazo hilo linahusu mifuko ya plastiki inayotumika kubebea bidhaa mbalimbali zinazouzwa madukani na halitahusu vifungashio vya maziwa, dawa, korosho na pembejeo.

Fursa mpya

Kwa wazalishaji, mkurugenzi wa kiwanda cha Harsho Group, Harold Shoo alisema alibadilisha mitambo ya kuzalisha mifuko ya plastiki na sasa wanatengeneza mifuko mbadala na marufuku hiyo inawapa uhakika wa soko.

Akizungumza na Mwananchi mjini Moshi jana, Shoo alisema alipata wakati mgumu kubadilisha mitambo ya kiwanda hicho ambacho sasa kinazalisha vifungashio mbadala ambavyo ni rafiki kwa mazingira.

Alisema mwaka 2016 walipewa barua iliyofuatiwa na waraka wa kuwataka kujiandaa kusitisha uzalishaji wa mifuko ya plastiki hivyo akatumia zaidi ya Sh1 bilioni kubadili mitambo aliyonayo kukidhi matakwa hayo.

“Serikali ilitoa waraka na kufanya vikao vya mara kwa mara na kampuni husika ili tuhame kutoka teknolojia moja kwenda nyingine. Changamoto kubwa ni kuwekeza kwenye miundombinu ya kuzalisha vifungashio vya aina nyingine,” alisema Shoo.

Baada ya kupokea waraka kutoka serikalini, wakati huo akizalisha mifuko 150,000 ya plastiki kwa siku, alifanya maandalizi mapema na sasa anazalisha mifuko 500,000 kwa siku ya kitambaa laini.

“Tunapata soko hapa nchini na hata Kenya pia,” alisema.

Kama ulivyo msimamo wa Shoo, mzalishaji wa mifuko mbadala aliyehudhuria mkutano wa jana, John Benedict alisema suala kuondokana na mifuko ya plastiki linawezekana huku akiwataka wajasiriamali kuchangamkia fursa iliyopo.

Meneja msaidizi wa kiwanda cha karatasi cha Mufindi, Gregory Chogo alisema wapo tayari kuongeza uzalishaji kukidhi mahitaji ya mchakato ya wajasiriamali wa mifuko nchini.

Alisema awali walikuwa wakizalisha tani 4,500 za karatasi zinazotumika kutengenezea mifuko lakini wako tayari kuongeza uzalishaji.

Waziri wa Uwekezaji, Angellah Kairuki aliwataka wadau kujipanga kuzalisha mifuko mbadala. “Nimefurahi namna wadau walivyoshirikishwa katika mchakato huu. Nawaomba mchangamkie fursa hii hasa katika utengenezaji wa vifungashio, bado kuna nafasi,” alisema Kairuki.