Hatima waliochangia kwa hiari mifuko ya hifadhi za jamii

Muktasari:

Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imesema changamoto inayolalamikiwa na baadhi ya wastaafu haihitaji mabadiliko ya sheria wala kanuni bali wastaafu kuelewana na mifuko husika ili iwaongezee muda wa marejesho ya mkopo.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imesema fedha zote za wachangiaji wa skimu za hiari katika mifuko iliyounganishwa ziko salama, hivyo wanachama hawapaswi kuwa na wasiwasi.

Baadhi ya wachangiaji wa skimu hizo walianza kuwa na wasiwasi juu ya hatima yao baada ya kuunganishwa kwa mifuko hiyo.

Wasiwasi umeibuka zaidi wakati huu ambapo kanuni mpya za Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2014 zimetolewa, lakini hazionyeshi mahali popote kuligusa kundi hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Irene Isaka alisema hakuna mabadiliko yoyote ya sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii yanayowahusu wao.

“Skimu zote za hiari yaani ‘supplementary schemes’ zilizokuwa PPF, PSPF, GEPF na LAPF zimehamishiwa PSSSF, Utaratibu ni uleule kama wa zamani hakuna mabadiliko yoyote,” alisema Isaka.

Alifafanua kuwa mifuko yote ilipeleka taarifa zake muhimu Benki Kuu (BoT) ikiwemo mikataba ya pango, watoa huduma, amana zilizopo benki, na hati fungani.

“Wanachama wote wasiwe na wasiwasi kwani taarifa zote za miradi, mikataba na uwekezaji zimehifadhiwa kwenye ‘strong room’ (chumba chenye usalama wa hali ya juu) Benki Kuu,” alisema Isaka.

Alisema kwa sasa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anafanya ukaguzi wa hesabu katika mifuko yote minne na akikamilisha, bodi za wadhamini wa mifuko iliyounganishwa watakabidhi hesabu hizo kwa Bodi ya Wadhamini ya PSSSF.

“Kama kuna kitu kitakuwa kimepotea kabla ya Julai 31 mwaka huu bodi ya zamani ya wadhamini wa mfuko husika itawajibika na kama kitu kitapotea baada ya Agosti Mosi, bodi mpya ya wadhamini ya PSSF itawajibika,” alisema.

Miongoni mwa wachangiaji wa mifuko ya hiari, Joseph Sendole alisema hafahamu hatima ya michango yake baada ya mifuko kuunganishwa kwani mfuko ambao anautumia haujampatia taarifa yoyote kuhusu mustakabali wa amana zake.

“Mimi nachangia skimu ya hiari tangu mwaka 2015 (bila kutaja mfuko husika), Sijaenda kuuliza kuhusu hatima yangu wala hawajanipa taarifa, nasubiri kusikia kutoka kwao ili nijue kama kuna utaratibu natakiwa kuufuata,” alisema.

Mwingine ambaye hakupenda jina lake liwekwe wazi alisema hana wasiwasi kwani hadi sasa anaweza kuiona akiba aliyonayo kupitia simu ya mkononi na hakuna mfuko uliomtaarifu mabadiliko yoyote.

“Bado naendelea kuchangia mifuko hiyo ya hiari, sina wasiwasi kwa kuwa sichangii pensheni na ninaweza kuchukua fedha zangu muda wowote na hata sasa nikiziangalia kwa simu najua zipo kiasi gani,” alisema mchangiaji huyo wa mfuko wa PSPF wa miaka minne na LAPF miaka miwili.

Mtoa taarifa huyo, ambaye ni mwanachama wa pensheni ya NSSF alisema hadi sasa hajapewa taarifa yoyote kuhusu mabadiliko hayo na anaamini amana zake ziko salama kwakuwa hazihusiani na pensheni.

Kuunganishwa mifuko

Kwa mujibu wa SSRA, malengo ya kuunganishwa mifuko yalikuwa ni kupunguza gharama za uendeshaji wa mifuko hiyo, kuwa na mifuko ya pensheni inayozingatia masharti ya ajira na kuboresha huduma za wanachama wa pensheni.

Malengo mengine ni kuimarisha utoaji wa mafao zaidi kwa wanachama kama ilivyoainishwa kwenye mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), na pia kuweka utaratibu wa kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa wanachama.