VIDEO: Hiki ndicho kilichomtokea Kibonde hadi kufariki

Muktasari:

  • Mtangazaji huyo alipatwa na mshtuko baada ya kumaliza kuendesha shughuli ya msiba wa Ruge Mutahaba kisha kukimbizwa hospitali Bukoba

Dar es Salaam. Mtangazaji na Meneja Ubunifu wa Clouds, Siza ameeleza kuwa Ephrahim Kibonde alianza kuumwa tu ghafla baada ya kuendesha shughuli nzima ya kuuzika mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds, Marehemu Ruge Mutahaba.


Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Machi 7, Siza amesema baada ya Kibonde kuendesha shughuli nzima nyumbani kwa kina Ruge mjini Bukoba alianza kujisikia vibaya akiwa eneo hilohilo la msiba na kusaidiwa na watu wa msalaba mwekundu wakisaidiana na Dk Issac Maro wa Clouds.


Amesema baada ya hilo kumtokea aliingizwa ndani ya nyumba ya kina Ruge na kuvuliwa viatu pamoja na kulegezwa mkanda kwa kuwa ilionekana kama amepatwa na presha hivyo akapewa huduma hya kwanza akiwa hapohapo nyumbani.


“Baada ya huduma ya kwanza tulimpeleka katika hospitali ya Bukoba kwa kuwa hali yake haikuwa nzuri hivyo akatibiwa pale na kupata chakula hivyo akarudi katika hali nzuri kidogo,”amesema Siza.


Amesema kuwa baada ya Kibonde kupata nafuu Dk Issac na wenzake walijadiliana na madaktari wa hospitali ya Bukoba kama  Kibonde anaweza kusafiri hadi Mwanza kwa ajili ya matibabu zaidi.


“Baada ya majadiliano tulimuuliza Kibonde kama anaweza kusafiri hadi Mwanza kwa kuwa ndege yetu ilikuwa inaondoka asubuhi hivyo alisema anaweza na tukakukabiana tukampeleka uwanja wa ndege kwa safari,”amesema Siza.


Amesema kuwa walifanikiwa kufika Mwanza na walimweka Kibonde kwenye wheel chair akisaidiwa na Dk Issac ambaye alikutana na mwenzake ambaye ana hospitali Mwanza.


“Baada ya kufika pale tulimwacha Kibonde na Dk Issac na hiyo daktari mwingine ambaye ni rafiki yake sisi tukaendelea na safari kuelekea Dar es Salaam  hadi leo asubuhi tunapata taarifa kuwa amefariki hivyo ndivyo ilivyokuwa,”amesema Siza.