KESI MAUAJI YA BILIONEA MSUYA: Hivi ndivyo mipango ya mauaji ilivyosukwa

Washitakiwa watano katika kesi ya mauwaji, ya mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite, Erasto Msuya, wakitoka katika chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Moshi baada ya kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa, hukumu hiyo ilisomwa  na Jaji Salma Maghimbi aliyekuwa akiskiliza kesi hiyo. Na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

  • Katika eneo la tukio kuliokotwa maganda ya risasi za SMG 22, huku gari yake aina ya Range Rover namba T800 CKF, bastola zake na simu zake mbili zikikutwa eneo la tukio.

Washtakiwa watano waliomuua kwa makusudi mfanyabiashara tajiri wa madini Mirerani mkoani Manyara na Arusha, Erasto Msuya, wamehukumiwa kunyongwa huku maelezo yao ya kukiri kosa yakiwachangia adhabu hiyo. Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa jijini Arusha, aliuawa kwa kupigwa risasi na bunduki ya kivita ya Sub Machine Gun (SMG), Agosti 7, 2013 eneo la Mijohoroni wilayani Hai.

Katika eneo la tukio kuliokotwa maganda ya risasi za SMG 22, huku gari yake aina ya Range Rover namba T800 CKF, bastola zake na simu zake mbili zikikutwa eneo la tukio.

Watu hao waliohukumiwa kunyongwa ni mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed; mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu; mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa, wa sita Sadik Jabir na wa saba, Ally Majeshi.

Hata hivyo, Jaji Salma Maghimbi wa Mahakama Kuu alimuachia huru mshtakiwa wa pili, Shwaibu Jumanne maarufu kwa jina la Mredii, kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kumtia hatiani kwa kosa la mauaji.

Akichambua ushahidi dhidi ya washtakiwa hao, Jaji Maghimbi alisema mahakama imezingatia maelezo ya kukiri kosa na ya ungamo ya washtakiwa wanne na pia ushahidi huru kuunga mkono.

Maelezo ya kukiri kosa ambayo yalipokewa mahakamani na kusomwa yakieleza mpango mzima wa mauaji hayo na ushiriki wa kila mmoja ni ya Sharifu, Mangu, Karim, Sadick na Majeshi.

Awali kesi hiyo ilipofunguliwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi mwaka 2013, ilikuwa na washtakiwa wanane, akiwemo mfanyabiashara mwingine tajiri, Joseph Mwakipesile au Chussa.

Hata hivyo Aprili 16, 2014, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), alimfutia mashtaka mfanyabiashara huyo akitumia kifungu Na 91 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) ya 2002.

Mei 14, 2018, Jaji Maghimbi alimuachia huru mshtakiwa wa nne, Jalila Zuber baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 32 wa mashtaka na vielelezo 26, na kumuona hana kesi ya kujibu.

Alichoeleza mshtakiwa wa kwanza

Katika maelezo yake ya kukiri kosa yaliyoandikwa na Inspekta Damian Chilumba, mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Athman, alieleza mpango mzima ulivyofanyika hadi kuuawa kwa Msuya.

“Mwishoni mwa mwezi Julai 2013 nilimtembelea Chussa na akaniambia Sharifu naomba uniangalizie shughuli zangu za madini zisikwame na ikibidi kugharamia shughuli za uendeshaji,”

“Wakati najiandaa kuondoka Chusa aliniomba nimsogelee ana jambo nyeti ambalo hataki watu wengine wasikie,”ananukuliwa mshtakiwa huyo wa kwanza akisema katika maelezo hayo.

Akinukuu alichoambiwa, shahidi huyo alidai, “unajua mateso yote haya ninayoyapata yanatokana na Msuya. Msuya ndiye amehonga niunganishwe kwenye kesi ya mauaji wakati sikuhusika,”

“Kwa sauti ya chini Chusa aliniambia unajua wewe ni rafiki yangu nisaidie kumuondoa duniani Msuya. Nilipigwa na butwaa. Kasema fanya ufanyavyo ndani ya siku chache Erasto Msuya afe.”

Mshtakiwa huyo katika maelezo hayo anadaiwa kumweleza Chussa kuwa asingeweza kumuua Msuya kwa kuwa hana ugomvi naye na ni mfanyabiashara mwenzake, kauli iliyoonekana kumuudhi Chusa.

“Alibadilika na kuonyesha hasira akaniambia kama umeshindwa basi nikitoka nitafanya mwenyewe. Baada ya kutafakari nikaona nikimwacha afanye mwenyewe angeniua kwa sababu alishaniweka wazi.

“Siku nyingine nilienda kumtembelea aliniuliza tena na kuniambia au rafiki yangu unataka kunisaliti? Nilimuuliza anataka nifanyeje hiyo kazi, akasema niwe mfadhili wa kazi yote akitoka atanirudishia”. Katika maelezo hayo, mshtakiwa anadaiwa kueleza kuwa Chusa alienda mbali na kumweleza kuwa kuna kijana anaitwa Mredii (Shaibu Jumanne, mshtakiwa wa pili) ametoka gerezani ashirikiane naye.

“Mimi na Mredii tulionana Mirerani nikamuuliza kama amepewa maelekezo yoyote na Chussa, akasema ni kweli ana maelekezo ya kutekeleza mpango mzima wa mauaji,” anadaiwa kueleza hivyo Sharifu.

“Tuliondoka kwenda Babati na kuonana na Chussa na lengo la kwenda ni kutaka anithibitishie Mredii aliyemtuma kwangu ndio huyo, naye akathibitisha ndio amemwagiza kutekeleza mauaji hayo.

“Mredii aliniambia ngoja atafute watu wa kazi anaowajua na ataleta gharama za kazi nzima. Baada ya siku mbili Mredii alikuja Arusha na kuniambia tayari ameshapata mtu mmoja.

“Nilienda nikakutana nao na Mredii akanitambulisha huyo mtu mwingine kuwa ni Ally Majeshi (mshtakiwa wa saba). Ally Majeshi aliniambia kikosi kitahitaji kuwa na watu wanne.”

Katika maelezo hayo, mshtakiwa huyo anadaiwa kueleza kuwa Majeshi ndiye aliyetoa wazo la kusajiliwa kwa laini mpya na kununua pikipiki mbili na baada ya hapo ndio watafute silaha.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, mshtakiwa huyo anadaiwa kueleza kuwa Majeshi alifanya mawasiliano na watu wengine wawili na siku iliyofuata alikutana nao Shamoo Guest House.

“Siku iliyofuata tulikutana Shamoo Guest House (inayomilikiwa na Sharifu) na ndipo nilitambulishwa kwa Sadik (Jabir-mshtakiwa wa sita) na Karim (Kihundwa - mshtakiwa wa tano), ”anadaiwa kueleza Sharifu.

“Walisema wanahitaji usafiri na nikawapa gari yangu aina ya Toyota Landcruicer LX pamoja na dereva wangu Mussa (Mangu-mshtakiwa wa tatu) wakaenda Namanga kutafuta silaha.

“Zilitengenezwa laini mpya sita na kununuliwa simu mpya sita zilizosajiliwa kwa jina la Adam Leani. Ally Majeshi ndio aligawa simu hizo. Zililetwa pikipiki King Lion nyeusi na Toyo nyekundu.

“Mredii, Sadick na dereva wangu ndio waliokwenda Namanga kwa ajili ya kukodi silaha, lakini siku hiyo haikupatikana ilibidi walale. Siku iliyofuata niliwapelekea Sh4 milioni za kukodi silaha. Siku hiyo walileta SMG na ilipelekwa nyumbani kwangu nikaihifadhi hadi siku ya tukio. Siku moja kabla ya tukio yaani tarehe 6/8 tulikutana wote Shamoo Guest House kukamilisha mipango.

“Siku hiyo tulikubaliana tutumie mbinu ya kufanya biashara ya madini ili kumvuta marehemu. Ally Majeshi aliniambia nitoe jiwe moja (la Tanzanite) ili aende kufanya biashara na Erasto.

“Jioni alienda na jiwe lile wakakubaliana kufanya biashara siku inayofuata (tarehe 7.8.2013, siku ya mauaji) maeneo ya Bomang’ombe. Alimwambia lile jiwe wako wawili na mdogo wake.”

Katika maelezo hayo, mshtakiwa anadaiwa kueleza kuwa siku ya mauaji, pikipiki aina ya King Lion nyeusi iliwabeba Mredii na Sadick wakati aina ya Toyo ilimbeba Karim na Majeshi.

“Majeshi alishukia eneo la Kia-Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (makutano ya barabara). Mimi nilikuwa na Suzuki na nilibaki na Jalila (Jalila Zuberi -mshtakiwa wa nne) ila hakutumika sana. Waliogopa kama wangemwacha angetoa siri.

“Mimi (Sharifu) ndiye nilibeba silaha hiyo kuelekea hadi Kia lakini tulipofika eneo la King’ori nilikabidhi silaha ile kwa Sadik aliyekuwa anatumia Toyo (pikipiki) nyekundu,” anadaiwa kueleza.

“Niliwaambia watakapomaliza kazi ya mauaji wasichukue chochote kwani hayo ndio yalikuwa maelekezo ya Chusa. Kaburu alinipigia simu baadaye na kuniambia kazi ya mauaji imekamilika.

“Kaburu ndiye mtu wa karibu na Chusa na ndiye alikuwa akimhudumia wakati akiwa amelazwa kule Babati na kuna wakati alikuwa akilala naye na alikuwa akijua mpango mzima wa mauaji.”

Mshtakiwa katika maelezo hayo ananukuliwa akieleza kuwa Kaburu ndiye aliyekuwa akifuatilia kila hatua ya mipango ya mauaji na yeye (mshtakiwa) alikuwa akimpa taarifa ili naye ampe Chusa.

“Baada ya tukio la mauaji kukamilika tulikutana wachache. Tulikutana na Mredii na Sadick maeneo ya Hoteli ya City Link na tukajadiliana kuhusu malipo yao na tathmini ya kazi nzima,” anadaiwa kueleza.

Mshtakiwa anadaiwa kueleza kuwa washtakiwa hao walitaka walipwe pesa zao zote hivyo siku hiyo aliwalipa Sh10 milioni, lakini kabla ya siku hiyo alikuwa tayari amewapa malipo ya awali ya Sh6 milioni.

“Baadaye Majeshi na Sadik walirudi wakataka niwapeleke Babati. Niliendesha gari kwenda Babati na tulifika saa 3:00 usiku,” mshtakiwa anadaiwa kueleza hayo katika maelezo yake hayo.

“Nilipofika Babati nikaenda moja kwa moja kwa Chusa (hospitalini alikokuwa amelazwa chini ya ulinzi ) na nikamweleza kukamilika kwa kazi ya kumuua Msuya na Chusa alifurahi sana.”

Katika maelezo hayo, mshtakiwa ananukuliwa kuandika uthibitisho wa maelezo hayo kwa mkono wake na kuweka saini na dole gumba akisema ameyatoa kwa hiari bila kushurutishwa.

Alichokiri mshtakiwa wa tatu

Akisoma maelezo ya Mangu, Januari 19, 2016, shahidi wa nane, Inspekta Herman Mtungi, mshtakiwa anadai kwa aonavyo yeye, kwa asilimia 100 mauaji hayo yalipangwa na kutekelezwa na Sharifu.

Katika maelezo yake hayo, Mangu ananukuliwa akisema anakumbuka Jumamosi moja ambayo hakumbuki tarehe, Sharifu alipeleka majina kwa mtu aliyemtaja ni Adamu ili akasajili laini za simu.

Mshtakiwa huyo anaeleza kuwa alimpelekea Adamu majina hayo na ilipofika saa 12:00 jioni alimpigia simu ili amfuate kwamba laini hizo tayari zilikuwa zimesajiliwa.

“Nilipomfuata nilimkuta kwa dada mmoja anayesajili simu na alinikabidhi laini mbili za Airtel na nilizipeleka nyumbani kwa Sharifu na kumkabidhi,” yanasomeka maelezo hayo.

Katika maelezo hayo, Mangu ananukuliwa akisema anakumbuka Julai 29, 2013 alipigiwa simu tena na Sharifu na kumwelekeza aende kwa Adamu akamchukulie laini nyingine mbili.

Agosti 3, 2013, Mangu katika maelezo hayo anadaiwa kumwambia Inspekta Herman kuwa alipigiwa simu na mshtakiwa wa kwanza na alipomfuata alimkuta akiwa na gari aina ya Toyota Noah.

Ndani ya gari hilo kulikuwa na vijana wawili ambapo alimtaka aende na Adamu kumsaidia kununua pikipiki mbili, na pikipiki hizo walizinunua kwa Sh3.4 milioni na kuzipeleka kwa Sharifu.

Pikipiki hizo zilisajiliwa kwa jina la Motii Ndoole ambalo ni jina lililotumika pia kusajili laini za simu ambazo Adamu aliagizwa azisajili na baadaye kukabidhiwa kwa mshtakiwa huyo wa kwanza.

Mshtakiwa huyo katika maelezo hayo anadai katika siku ya Jumanne ambayo tarehe haikumbuki, bosi wake alimwita katika hoteli yake ambako alimkuta na vijana watatu wakifanya mazungumzo.

“Alitoka ndani akiwa ameongozana na watu watatu nisiowafahamu. Mimi ndio niliendesha ile Noah, wale vijana watatu wakawa wanaulizana nani akafanye naye biashara (Msuya), ” anaeleza Mangu.

“Nilimuuliza Sharifu (mshtakiwa wa kwanza) wanaenda kufanya biashara gani, akasema wanaenda kumuuzia mawe (madini ya Tanzanite) Erasto Msuya.”

Katika maelezo hayo, Mangu ananukuliwa akidai Agosti 7, 2013, mshtakiwa alikuja akiwa na gari aina ya Suzuki Vitara ndani yake kulikuwa na wale vijana aliowakuta na bosi wake jana yake.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, Mangu anadai bosi wake alimwelekeza aendeshe hiyo Suzuki Vitara kuelekea Moshi, lakini akawa anaongea na watu kwenye simu kuwa wamsubiri King’ori.

“Tulipofika King’ori, Sharifu alinielekeza nisimame mahali walipokuwa wamesimama vijana wawili ambapo niliwatambua wawili kuwa ni wale niliokutana nao jana yake,” anaeleza Mangu.

Mangu katika maelezo hayo, anadaiwa kumweleza Inspekta Ngurukizi kuwa watu hao wanne walikuwa na pikipiki mbili ambazo walizinunua jana yake na kuzipeleka nyumbani kwa Sharifu.

“Tulianza safari gari yetu ikiwa mbele huku pikipiki zikiwa nyuma. Tulielekea hadi kwenye miti ya mijohoro (Wilaya ya Hai), Sharifu aliniambia nisimamishe gari,” ananukuliwa Mangu.

Anadai katika maelezo hayo kuwa, baada ya kusimamisha gari, ilikuja pikipiki nyekundu ambayo ni moja kati ya zile walizonunua ambapo aliwaambia, “biashara ifanyikie hapa.”

Anaeleza kuwa wao walirudi Arusha na kuwaaacha wale vijana, lakini alipokuwa kijiweni siku hiyo hiyo saa 8:10 mchana alisikia taarifa kuwa Erasto amekufa kwa kupigwa risasi Kia.

Katika maelezo hayo, mshtakiwa huyo anadai alipata picha vijana wale ndio waliofanya mauaji hayo kwa vile eneo la mauaji ndilo bosi wake aliwaambia wale vijana wafanyie biashara hapo.

Pia, anadai anaamini ndio waliohusika na mauaji hayo kwa vile jana yake, bosi wake alimweleza kuwa vijana wale wanakwenda kufanya biashara na Erasto na asubuhi yake aliona mfuko ukiwa na bunduki.

Katika maelezo ya nyongeza aliyoyaandika polisi, Mangu anadai Agosti 4, 2013, Sharifu alimwelekeza awapeleke watu ambao aliwatambua baadaye kwa majina ya Mredii na Msoja hadi Namanga.

“Nili-pack (egesha gari) upande wa Kenya. Mredii na Msoja walienda nisikokujua hadi saa mbili usiku waliporudi na kuniambia itabidi tulale Namanga kwa vile walichokifuata hawajakipata,” anasema mshtakiwa huyo katika maelezo yake.

Siku iliyofuata saa 4:00 asubuhi, Mredii alimpigia simu kwamba awafuate upande wa Kenya na alipowakuta walimwambia ampigie simu Sharifu kumjulisha kuwa ‘mzigo’ umepatikana.

Hata hivyo, Mangu ananukuliwa akisema alikataa kumpigia simu bosi wake na ndipo Mredii alipiga simu Sharifu na baadaye alimsikia akisema atatuma pesa kwa M-Pesa na ameikagua ni nzuri na inapiga.

Mangu anadaiwa kukataa kubeba mzigo huo na ndipo Mredii akampigia simu Sharifu aje mwenyewe kuubeba na wakati wanasubiri pale, alikuja Msomali mmoja akawa anazungumza nao. “Sharifu alikuja baada ya saa tatu. Mredii na yule Msomali wakapanda kwenye gari la Sharifu. Nilihisi walichofuata Namanga ilikuwa ni bunduki, lakini sikujua ni ya aina gani,” anaeleza Mangu

Mshtakiwa wa tano alivyofyatua risasi

Katika maelezo yake ya ungamo (extra judicial statement), ya mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa yaliyoandikwa Septemba 16, 2013, mshtakiwa huyo alieleza namna alivyomfyatulia risasi Bilionea Msuya.

Maelezo hayo yaliandikwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Moshi, Ponsian Claud aliyekuwa shahidi wa 12 na yalipokewa kama kielelezo na kusomwa mahakamani.

Katika maelezo hayo, shahidi huyo alidai mshtakiwa aliyatoa kwa hiari na kwa ridhaa yake, akieleza alifika eneo la tukio na mshtakiwa wa sita, Sadick Jabir wakiwa na pikipiki.

Mshtakiwa anadaiwa kumweleza mlinzi huyo wa amani kuwa ndiye aliyefyatua risasi kwa kutumia bunduki aina ya SMG akishirikiana na mtu aliyemtaja kwa jina moja la Sharifu na kumuua Erasto.

Halikadhalika katika maelezo hayo ya ungamo, mshtakiwa anadaiwa kueleza kwa hiari yake kuwa katika kutekeleza mauaji hayo, alishirikiana na watu wengine watatu ambao ni Sharifu, Mredii na Sadik.