Kijana mbaroni akidaiwa kumlawiti mama yake mzazi

Friday July 5 2019

 

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mazengo Chilatu (28) anashikiliwa na polisi mkoani Dodoma kwa tuhuma za kumbaka mama yake mzazi mwenye umri wa miaka 58.

Mkazi huyo wa Kijiji cha Manchali wilayani Chamwino mkoani Dodoma alimfuata mama yake chumbani na kumfanyia kitendo hicho cha kikatili, kisha kurejea katika chumba chake.

Baada ya tukio hilo lilitokea mwanzoni mwa wiki hii, mama huyo alitoka nje ya nyumba hiyo na kuomba msaada wa majirani waliofika na kumkamata kijana huyo.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto aliwaeleza waandishi wa habari kuwa huenda kijana huyo alifanya tukio hilo la kinyama kutokana na imani za kishirikina na ukosefu wa maadili.

Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi na utakapokamilika watamfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo.

Akizungumzia tukio hilo, Muroto alisema matuko ya ubakaji, ulawiti na ukatili wa kijinsia yamekuwa ni mengi, lakini hilo alilielezea kuwa ni “la ajabu sana tena lenye fedheha kwa kijana mwenye nguvu kumuingilia mama yake tena kwa kumlawiti usiku.”

Advertisement

Akizungumza na Mwananchi, diwani wa Manchali, Mary Mazengo alisema walisikia kelele za mama huyo kuomba msaada na walipofika walimkamata mwanaye.

“Maisha yao si mazuri tangu baba wa kijana huyo alipofariki miaka miwili iliyopita. Alipopiga kelele walimkuta kijana huyu akiwa na nia ya kuendelea kufanya kitendo hicho,” alisema Mazengo.

Alisema wanafamilia hao wamekuwa na historia ya kutumia pombe za kienyeji lakini hakukuwahi kutokea ugomvi wala malumbano baina yao.

Mwingine auawa kwa kubaka mtoto

Katika tukio jingine, Muroto alisema kijana mmoja ambaye jina lake halijafahamika anayekadiriwa kuwa na miaka 25, ameuawa kwa kushambuliwa na wananchi baada ya kufumaniwa akimbaka mtoto wa miaka minane.

Alisema hilo ni mwendelezo wa matukio ya ubakaji mkoani humo ambayo alisema yameongezeka kutoka 174 mwaka jana hadi 517, sawa na ongezeko la matukio 343.

Alisema awali, mtu huyo aliwabaka watu watatu kwa nyakati tofauti, wote wa Mtaa wa Mailimbili mjini hapa na kwamba kila alipotimiza azma yake, amekuwa akikimbia.

“Sasa jana (juzi) alimvizia mtoto wa miaka minane ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili, alimkamata na kumuingiza katika nyumba ambayo haijamalizika kujengwa, lakini safari hii wananchi walimkamata na kumpiga,” alisema Muroto.

Katika tukio jingine, Muroto alisema polisi wanamshikilia Donald Justine (25) mkazi wa Nanenane Nzuguni kwa tuhuma za kumbaka kikongwe wa miaka 95.

Advertisement