Lema alivyohojiwa kwa dakika 132, hatima yake kesho

Muktasari:

  • Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imetumia dakika 132 kumhoji Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbles Lema kwa kauli yake kuwa bunge ni dhaifu

Dodoma. Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imetumia dakika 132 kumhoji Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbles Lema lakini uamuzi wa suala hilo utatolewa kesho bungeni.

Lema ameingia kwenye kamati hiyo mara tatu akihojiwa na kutoka kisha akaitwa tena na hadi saa 11:58 jioni alimaliza kuhojiwa na kuruhusiwa.

Awali mbunge huyo aliingia ndani ya kamati akitumia dakika 44 kisha akatoka na kuitwa  tena saa 9:52 akatoka 10:56, kisha akaitwa kwa mara ya tatu saa 11:34 hadi saa 17:58 alipomaliza kuhojiwa.

Wakati akiitwa mara ya tatu, alikuwa ameketi na Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde ambaye alimtaka akitoka wawasiliane kwanza.

Majira ya saa 11:06 kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freman Mbowe alifika katika eneo alilopumzika Lema wakakaa wakizungumza kisha kisha wakaagana.

Mbunge huyo ameitwa mbele ya kamati kuhojiwa kutokana na mchango wake bungeni jana aliponukuu kauli ya Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kuwa Bunge ni dhaifu.

Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliagiza kamati ya maadili kumuita mbunge huyo na kumhoji, agizo ambalo liliungwa mkono leo na Spika Job Ndugai na kutaka mahojiano hayo yakamilike leo na kesho kamati ipeleke mapendekezo ndani ya Bunge kuhusu hatma yake.