Wizara ya Madini kuwezesha wachimbaji wanawake, vijana

Muktasari:

  • Wizara ya Madini imewasilisha mapendekezo yake ya bajeti bungeni huku ikitaja programu mpya ya ‘madini ni mwanga kesho’ (MBT), ni mahsusi kuwainua wachimbaji  wanawake na vijana.

Dodoma. Wakati Wizara ya Madini imekuja na programu ya ‘madini ni mwanga kesho’ (MBT) kwa vijana na wanawake, pia imeliomba Bunge kuridhia bajeti ya Sh231.9 bilioni.

Hayo yamesemwa leo Jumanne, Aprili 30, 2024 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Mavunde amelieleza Bunge kuwa programu mpya ya ‘madini ni mwanga kesho’ au ‘mining for a brighter tomorrow’ (MBT) ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kuwainua wachimbaji  wanawake na vijana.

Kwa mujibu wa Mavunde, MBT itatoa kipaumbele kwa wanawake na vijana katika maeneo ya utoaji wa leseni katika maeneo ya uchimbaji; na wachimbaji kunufaika na vitendea kazi ikiwemo magari, vifaa na mitambo ya uchimbaji.

“Programu hiyo itasaidia kuchochea ukuaji wa sekta ya madini, uchumi wa Taifa na kuongeza ajira kwa Watanzania,” amesema.

Amesema programu ya MBT  imelenga kuongeza tija kwenye shughuli za uongezaji thamani madini kupitia utoaji wa vifaa vya uongezaji thamani madini kwa wahitimu wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), usimamizi wa sheria; na ushiriki wa Watanzania katika shughuli za madini na uwajibikaji wa kampuni kwa jamii.

Mavunde amesema ‘Vision 2030 ya Wizara inasema madini ni maisha na utajiri’ na kwamba Wizara kupitia GST itaendelea kufanya utafiti wa kina wa jiofizikia kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ili kutambua tabia za miamba na kurahisisha tafiti nyingine za jiosayansi zenye kuwezesha kubaini aina mbalimbali za madini yapatikanayo nchini.

“Hadi sasa utafiti wa kina wa jiofizikia umefanyika kwa asilimia 16 ya eneo lote la nchi. Aidha, GST katika mwaka wa fedha 2024/2025 inatarajia kufanya utafiti wa kina wa jiofizikia katika blocks mbili zenye jumla ya kilometa za mraba 165,574. Baadhi ya maeneo yatakayopitiwa yapo kwenye mikoa ya Rukwa, Katavi, Mbeya, Songwe na Kigoma,” amesema Mavunde.

Amesema malengo ya wizara ni kufanya utafiti wa kina wa jiofizikia kufikia angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

“Dhana hii ya “vision 2030” inakusudia kuiendeleza sekta ya madini kwa kufanya yafuatayo: kufanya tafiti za kina za jiofizikia kujenga maabara ya kisasa kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa miamba, udongo, maji na madini; kuanzisha makumbusho maalum ya madini; kuwawezesha wachimbaji wadogo kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kuwapatia mashine 15 za uchorongaji.

“Kuyafanya madini mkakati na madini muhimu yawe na nguvu ya soko; kuongeza thamani madini hapa nchini; kuwaendeleza  wawekezaji wazawa ili kuongeza wigo wa uwekezaji unaotokana na Watanzania; kuongeza ushiriki wa Watanzania  katika kusambaza bidhaa na kutoa huduma migodini; na kuandaa mazingira rafiki na kuvutia uwekezaji mkubwa kutoka nje ya nchi,” amesema.


Biashara ya madini

Mavunde amesema mwenendo wa biashara ya madini kwa kipindi cha kuanzia Julai, 2023 hadi Machi, 2024, bei ya madini ya dhahabu kwa wakia ilipanda hadi kufikia wastani wa Dola za Marekani 2,138.01 ikilinganishwa na bei ya wastani wa Dola za Marekani 1,854.54 katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023.

Amesema kuongezeka kwa bei ya dhahabu kunatokana na sababu mbalimbali ikiwemo mahitaji makubwa ya madini hayo duniani.

“Kwa upande wa madini ya almasi, katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, mwenendo wa biashara ya madini hayo duniani umeendelea kusuasua kutokana na mdororo wa uchumi uliosababishwa na madhara ya vita kati ya Urusi na Ukraine.

“Madini hayo yameshuka bei duniani kwa asilimia 19 kwa Machi, 2024. Aidha, wastani wa mauzo ya madini ya almasi katika kipindi husika ni karati 201.71 yenye thamani ya dola za Marekani 43,231,183.71 ikilinganishwa na karati 271.74 yenye thamani ya dola za Marekani 50,824,739.77 katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi, 2023,” amesema.

Mavunde amesema hatua zilizoanza kuchukuliwa na wazalishaji mbalimbali wa almasi duniani ni kupunguza uzalishaji wa almasi ili kuimarisha bei ya madini hayo.


Mafanikio ya sekta ya madini

Mavunde amesema miongoni mwa mafanikio katika sekta ya madini ni kuendelea kuongezeka kwa mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa kutoka asilimia 6.7 mwaka 2020, asilimia 7.3 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia  9.1 mwaka 2022.

Amesema pia ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali uliongezeka kutoka Sh588 bilioni mwaka 2020/2021, Sh623.2 bilioni mwaka 2021/2022 hadi Sh678 bilioni mwaka 2022/2023.

Ametaja mafanikio mengine ni pamoja na kuongezeka kwa masoko na vituo vya ununuzi wa madini kutoka 41 na 61 mwaka 2020/2021 hadi kufikia 42 na 100 mwaka 2023/2024 ambapo kulifanyika biashara ya madini yenye thamani ya Sh2.095 trilioni na Sh1.9 trilioni.