VIDEO: Lugola atoa agizo, trafiki kupigana na dereva

Muktasari:

  • Tukio la polisi wa usalama barabarani kupigana na dereva mkoani Songwe ambalo video yake imesambaa kwenye mitandao ya kijamii, limemuibua Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ambaye amemtumia video hiyo Kamanda wa Polisi Usalama Barabarani ili afuatilie na kujua undani wake.

 Wakati video inayoonyesha askari watatu wa Kikosi cha Usalama Barabarani wakimshambulia dereva wa lori ikizua mjadala mitandaoni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limesema litatoa tamko la tukio hilo haraka iwezekanavyo.

Katika video hiyo, askari hao wanaonekana wakimshambulia dereva huyo kabla ya kundi la wananchi waliokuwa wakiwashangaa awali, kuamua ugomvi huo.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alisema, “Nimemtumia kipande hicho cha video Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslimu ili afuatilie kujua undani wake na taarifa itatolewa.”

Hata hivyo, alipotafutwa kwa simu jana, Kamanda Muslimu hakupatikana kwani simu yake iliita bila kupokewa.

Lakini akizungumza na Mwananchi jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange alisema tayari wameshapewa maelezo na watatoa ufafanuzi kuhusu jambo hilo.

“Mimi mambo yote huwa yanatolewa ofisini kwa njia ya ‘Press’ (mkutano na waandishi wa habari) sio kwa njia ya simu hivyo mtafahamu ni kitu gani,” alisema.

Tukio hilo limeibua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii kutokana na jinsi askari hao walivyotumia nguvu kubwa kumkamata dereva huyo ambaye haikufahamika mara kosa alilotendana alikokuwa akitokea au kuelekea.

Katika video hiyo, askari wanaonekana wakimshambulia dereva huyu katika jitihada za kutaka kumkamata na kumdhibiti lakini alionekana kufanikiwa kujinasua katika mikono yao.

Katika patashika hiyo, dereva huyo anasikika akipiga kelele kuomba msaada akilalamika kung’atwa shingoni na mmoja wa askari.

Baada ya kufanikiwa kutoka katika mikono ya askari dereva wa lori alionekana kukimbilia katika gari na kuchukua panga jambo ambalo liliwafanya watu kutimua mbio.

Lugola asimamisha kazi maofisa

Katika hatua nyingine Lugola amewasimamisha kazi maofisa watano wa Idara ya Wakimbizi kwa madai ya kushindwa kutoa taarifa mapema za uwepo wa marobota 1,947 ya nguo zinazodaiwa kuwa ni za jeshi kwenye kambi za wakimbizi za Nduta na Mtendeli.

Lugola amewataja waliosimamishwa kazi kuwa ni mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi Harrison Mseke, mkurugenzi msaidizi wa huduma kwa wakimbizi Deudsdedit Masusu, mkurugenzi msaidizi huduma kwa wakimbizi usalama na operesheni, Seleman Mziray, mkuu wa Kambi ya Nduta Peter Bulugu (Kibondo) na John Mwita, mkuu wa Kambi ya Mtendeli iliyopo Kakonko.

Akizungumza na wanahabari katika ofisi ndogo ya wizara hiyo Dar es Salaam jana, Lugola alisema nguo hizo zilitolewa kama msaada na shirika la Japan la Uniqlo kwa ajili ya wakimbizi wa kambi hizo lakini viongozi wa idara hiyo hawakutoa taarifa mapema.
Amemwagiza katibu mkuu wa wizara hiyo kuunda kamati ndani ya siku kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo ndani ya siku 10.