Jaguar kusota ndani siku tatu zaidi
Nairobi. Mbunge wa Starehe nchini Kenya, Charles Njagua ataendelea kusota rumande kwa siku tatu zaidi katika kituo cha polisi cha Kileleshwa baada ya mahakama kusema kuna haja ya kulinda uchunguzi unaoendeshwa kuhusu matamshi ya uchochezi anayodaiwa.
Ingawa Hakimu mkazi wa mahakama jijini Nairobi, Tobiko Sinkiyan amesema haijathibitishwa ni vipi Njagua atavuruga uchunguzi, amesema bila shaka mbunge huyo ambaye pia wengi wanamjua kama Jaguar ni mtu mwenye ushawishi.
Hivyo, hakimu amesema hakuna wasiwasi kwamba ipo haja ya kulinda na kuhifadhi ripoti ya uchunguzi.
Jana Alhamisi, maofisa wa polisi walikuwa wameomba mbunge huyo azuiliwe kwa siku 14 katika kituo cha polisi cha Kamukunji.
Jaguar alikamatwa Jumatano ikiwa ni siku chache baada ya kutoa matamshi akitaka wafanyabiashara wa kutoka mataifa ya kigeni hasa wa Tanzania na China wafurushwe nchini Kenya.