Magufuli atua kwa Mbowe, atoa ujumbe

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Jumanne Julia 30, 2019  ameitembelea familia ya Meja Jenerali mstaafu Albert Mbowe aliyefariki dunia juzi Jumapili Julai 28, 2019 nyumbani kwake, Salasala jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli ametoa pole kwa familia kina Mbowe, kufuatia kifo cha Meja Jenerali mstaafu Albert Mbowe aliyefariki dunia juzi Jumapili Julai 28, 2019 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolea leo Ju

manne Julai 30, 2019 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Tanzania imesema Magufuli amekwenda nyumbani kwa marehemu eneo la Salasala jijini Dar es Salaam na kukutana na familia ikiongozwa na mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe
Taarifa hiyo imesema pamoja na kutia saini kitabu cha maombolezo, Rais Magufuli ameungana na familia hiyo katika sala ya pamoja ya kumuombea marehemu.


Baada ya sala hiyo, Rais Magufuli ameitaka familia hiyo iendelee kuwa na umoja kama ilivyokuwa wakati wa uhai wa Meja Jenerali Mbowe na kumtanguliza mwenyezi Mungu.
Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali  Venance Mabeyo amesema pamoja na kustaafu Meja Jenerali Mbowe alikuwa mshauri wa karibu wa Jeshi.
Amesema katika utumishi wake wa miaka 36 na siku 27 Jeshini, Meja Jenerali Mbowe alitoa mchango mkubwa katika masuala ya usimamizi wa fedha
Meja Jenerali Mbowe alizaliwa Januari 1953, alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) mwaka 1973 na alistaafu utumishi Jeshini mwaka 2009.