Makonda atangazia fursa wanafunzi wa kike Dar wanaosoma sayansi

Muktasari:

  • Makonda aja na ufadhili kwa watoto wa kike kutoka familia maskini, ajipanga kuwagharamia masomo wanafunzi 100 watakaochaguliwa kidato cha tano masomo ya sayansi

Dar es Salaam. Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, ametoa ufadhili wa kuwasomesha kidato cha tano na sita wanafunzi wa kike 100 watakaofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi.

Makonda amesema ufadhili huo unawalenga watoto kutoka familia duni ndani ya mkoa wa Dar es Salaam watakaojiunga kidato cha tano mwaka 2019.

“Nimemua kutengeneza mfuko maalumu wa kusaidia watoto wa kike wanaotoka kwenye familia duni ndani ya mkoa wa Dar es Salaam,” amesema Makonda leo Jumatano Machi 20, 2019  akizungumza na wanahabari.

“Hawa wataingia kwenye mfuko wa Makonda kwa kidato cha tano na sita nitalipia gharama zote za masomo yao kuanzia ada, vitabu, sare na vitu vingine vyote,” amesema

Makonda amesema: “Hawa  kwangu ni watu muhimu sana licha ya ugumu wa maisha wanayopitia lakini wanajikwamua na kufaulu hasa katika masomo magumu haya ya sayansi.”

Amesema kwa mwaka huu ataanza na wanafunzi 100 na mwakani ataongeza 100 wengine.

Amesema amemua kuwasaidia wanafunzi katika mchepuo huo kwa sababu kuna hitaji kubwa la wanasayansi na kwamba, licha ya wingi wa rasilimali zilizopo bila kuwa na wanasayansi wa kutosha zinaweza zisiwe na tija.