Mama wa miaka 64 asimulia alivyopambana na mamba

Mkazi wa kitongoji cha Mwibale  wilayani Serengeti, Chibona Matoyo (64) akihojiwa na Mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Daniel Makaka (kushoto) baada ya bibi huyo kunusulika kifo kufuatia kushambuliwa na mamba alipokuwa akioga ndani ya Ziwa Victoria, wilayani humo. Na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

  • Mama huyo, Chibona Matoyo (64), licha ya kuvunjika mkono na kujeruhiwa paji la uso, alipambana na mamba huyo huku akipiga kelele ndipo wavuvi walipomsaidia kwa kumnasua kutoka kwa mamba huyo.

Buchosa. Chibona Matoyo (64), mkazi wa Kijiji cha Kanyala Wilaya ya Sengerema, Mara amenusurika kifo baada ya kujeruhiwa na mamba wakati akioga katika Ziwa Victoria.

Katika tukio hilo lilitokea Alhamisi iliyopita, Chibona alivunjika mikono na kujeruhiwa paji la uso na sasa anapatiwa matibabu kwenye Kituo cha Afya Mwangika, Buchosa wilayani humo.

Akizungumza na Mwananchi jana, mama huyo mwenye watoto watano na wajukuu tisa, alisema wavuvi ndio waliookoa maisha yake baada ya kupiga kelele akiomba msaada.

“Walipoona napiga kelele walifika eneo la tukio na kunikuta napambana na mamba, walinisaidia kujinasua, walifanikiwa,” alisema.

Baada ya kupata taarifa za tukio hilo, mume wa Chibona, Ernest Majula (81) aliangua kilioakisema mkewe amepata kilema na kuiomba Serikali kuchukua hatua kuwadhibiti wanyama hao.

Mtoto wa mama huyo, Agnes Majula alisema wamekuwa na mazoea ya kwenda kuoga ziwani wakiamini kuwa kufanya hivyo ni vizuri zaidi kuliko majumbani mwao.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mmoja wa wanafamilia ya mama huyo, Joseph Dui aliyesema wakazi wa maeneo hayo mbali ya kuoga, wana desturi kuoshea vyombo ziwani licha ya kujua kwamba maeneo hayo yana wanyama wakali.

Dui alisema Serikali za vijiji zinatakiwa kuweka mkazo kwa wananchi wake kujenga mabafu kila kaya ili wananchi waoge nyumbani kuokoa maisha yao.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Buchosa, Ernest Chacha ambaye alisema mama huyo anaendelea kupatiwa matibabu, aliwataka wananchi wanaopata majanga hayo kuwahi hospitali ili kupatiwa matibabu kwa haraka.

Ofisa Ardhi na Maliasili Halmashauri ya Buchosa, Aliko Ndile alisema kutokana na matukio ya wananchi kujeruhiwa na kuuawa na mamba kuongezeka, idara yake imeweka mkakati wa kuwasaka na kuwaua.

Alisema kuanzia Januari Mosi, watu watano wamejeruhiwa na kutaja maeneo ambayo wananchi huvamiwa zaidi kuwa ni Maisome, Kanyala na Nyambemba.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alisema Serikali inajitahidi kumaliza tatizo la mamba kushambulia wananchi kwa kutoa elimu kwa wananchi kuoga majumbani mwao.