Mbowe, Matiko sasa wabakiza kiunzi kimoja

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko wakiwa chini ya ulinzi wa askari magereza wakati wakiingia Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam jana kusikiliza rufaa yao ya kupinga kufutiwa dhamana katika kesi ya jinai inayowakabili wao na wanachama wengine saba wa Chadema. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Baada ya kuvuka hatua hiyo, kiongozi huyo wa upinzani bungeni, sasa amebakiza hatua moja tu muhimu ya Mahakama Kuu kusikiliza rufaa yao itakayotoa hatima yao ya kuendelea kuishi gerezani wakati kesi yao iliyo Mahakama ya Kisutu ikiendelea, au kuachiwa huru.

Dar es Salaam. Baada ya kushinda rufaa iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), sasa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mhazini wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Esther Matiko, wamebakiza hatua moja tu kurudi nyumbani ikiwa watashinda.

Hatua hiyo ni ya usikilizwaji wa rufaa yao iliyosimamishwa kusikilizwa Mahakama Kuu, ambayo waliikata kwa hati ya dharura, wakipinga kufutiwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika kesi ya jinai inayowakabili na wenzao saba.

Hadi jana Mbowe, ambaye ni mbunge wa Hai, na Matiko (Tarime Mjini), walikuwa wamekaa mahabusu katika Gereza la Segerea kwa siku 98 baada ya kufutiwa dhamana Novemba 23 mwaka jana.

Sasa wanasubiri kupangiwa tarehe ya kusikiliza rufaa yao.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mahakama ya Rufani kutupa pingamizi la DPP la kuiomba isisikilize rufaa hiyo kwa madai ina kasoro za kisheria na kuamua kuendelea kuisikiliza.

Katika uamuzi wa jopo la majaji watatu, Stella Mugasha, Dk Gerald Ndika na Mwanaisha Kwariko, Mahakama ya Rufani ilisema hoja za DPP hazikuwa na mashiko.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Sylvester Kainda alisema wakati akisoma hukumu hiyo kuwa mahakama imeikataa rufaa yote.

“Kwa hayo tuliyotangulia kuyasema, tunaikataa rufaa hii yote. Tunaelekeza jalada la kesi hii lirejeshwe Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji wa rufaa,” alisema Kainda.

Baada ya kuvuka hatua hiyo, kiongozi huyo wa upinzani bungeni, sasa amebakiza hatua moja tu muhimu ya Mahakama Kuu kusikiliza rufaa yao itakayotoa hatima yao ya kuendelea kuishi gerezani wakati kesi yao iliyo Mahakama ya Kisutu ikiendelea, au kuachiwa huru.

Kwa hiyo, kwa tarehe watakayopangiwa watakuwa na kibarua kizito cha kuishawishi Mahakama Kuu kuwa uamuzi wa Mahakama ya Kisutu kuwafutia dhamana haukuwa sahihi.

Kupitia kwa mawakili wao Peter Kibatala na Prosefa Abdallah Safari, watatakiwa kutoa hoja za kisheria na hata kufanya rejea ya kesi mbalimbali katika kuishawishi mahakama iweze kukubaliana nao.

Hapana shaka huo nao utakuwa ni mchuano mkali wa hoja za kisheria baina yao na mawakili wa Serikali, ambao pia watakuwa wakipambana kuishawishi Mahakama ikubali Mahakama ya Kisutu ilikuwa sahihi kwa kuwafutia dhamana.

Ikiwa Mahakama Kuu itakubaliana na hoja zao, itatengua uamuzi wa kuwafutia dhamana na hivyo kuendelea na kesi yao ya msingi huku wakiwa nje.

Hata kama DPP hatakubaliana na hukumu ya Mahakama Kuu na akaamua kukata tena rufaa Mahakama ya Rufani, kupinga sababu za Mahakama Kuu kutengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, bado wataendelea kuwa nje hadi hapo Mahakama ya Rufani itakapoamua vinginevyo.

Lakini kama katika hatua hiyo watashindwa kuishawishi Mahakama Kuu au Mahakama Kuu ikikubaliana na hoja za DPP kuwa uamuzi wa kuwafutia dhamana ulikuwa sahihi, Mbowe na Matiko wataendelea na maisha ya mahabusu wakisubiri hukumu ya kesi ya msingi.

Na hata kama hawatakubaliana na hukumu ya Mahakama ya Kuu na wakaamua kukata rufaa, bado wataendelea kuishi mahabusu hadi Mahakama ya Rufani itakapotoa hukumu ambayo ndio itakuwa ya mwisho na pande zote zitawajibika kuifuata.

Hata hivyo upande wowote unaweza kuomba marejeo kama utaona kuwa kuna kasoro katika hukumu hiyo ili mahakama hiyo izitafakari kwa lengo la kubadilisha hukumu hiyo kwa namna itakavyoona inafaa.

Aliyekuwa Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri alifuta dhamana ya Mbowe na Matiko Novemba 23, 2018, baada ya wawili hao kushindwa kufika mahakamani ambako wanakabiliwa na kesi ya jinai pamoja na viongozi wengine saba wa Chadema.

Siku hiyo, wakili wao Peter Kibatala alikata rufaa Mahakama Kuu kupinga kufutiwa dhamana yao chini ya hati ya dharura sana.

Lakini DPP aliweka pingamizi akiiomba mahakama hiyo isiisikilize rufaa hiyo pamoja na mambo mengine, akidai kuwa haina mamlaka kwa kuwa rufaa hiyo ilikuwa inakiuka matakwa ya sheria kwa kutoambatanisha mwenendo wa uamuzi waliokuwa wakiupinga.

Jaji Sam Rumanyika alitupilia mbali pingamizi hilo la DPP na akaamua kuendelea kusikiliza rufaa ya kina Mbowe, lakini kabla ya kuanza kuisikiliza, DPP akaenda Mahakama ya Rufani, ambako pia amegonga mwamba.

Katika hoja zake, DPP aliiomba mahakama hiyo itengue uamuzi wa Mahakama Kuu, akidai kuwa Mahakama Kuu ilikosea kukubali kusikiliza rufaa hiyo kwa kuwa inakiuka matakwa ya kisheria na kwamba hawakupewa fursa ya kutosha kusikilizwa, kabla ya kufikia uamuzi wa kukubali kuendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo.

Lakini katika hukumu yake, Mahakama ya Rufani imesema Mahakama Kuu ilikuwa sahihi kwa kuwa jaji alitumia mamlaka yake kuamua kuendelea na kusikiliza rufaa hiyo, aliyopewa na kifungu cha 361 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai.

Pia imesema madai ya DPP kunyimwa haki, hayana mashiko kwa kuwa alipewa muda wa kusikiliza pingamizi na mahakama ikatoa uamuzi na kwamba baada ya kupanga muda wa kusikiliza rufaa hiyo, hakuna maombi ambayo aliyatoa akakataliwa kusikilizwa.

Katika kesi ya msingi Mbowe, Matiko na wengine saba wakiwemo wabunge watano na viongozi wawili wa chama, wanakabiliwa na mashtaka 13, yakiwamo ya uchochezi na uchochezi wa uasi.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16, 2018 katika Viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni wakati wakihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Kinondoni.

Mbali na Mbowe na Matiko, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji, manaibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara), ambaye pia ni mbunge wa Kibamba na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Wengine ni Mchungaji Peter Msigwa (mbunge wa Iringa Mjini, Halima Mdee (mbunge Kawe), Ester Bulaya (mbunge, Bunda), na John Heche (mbunge, Tarime Vijijini).