Mbunge CCM adai shambulio la Lissu ni mpango wa Chadema

Mbunge wa jimbo la Siha Dk Godwin Mollel, akichangia mjadala wa Taarifa mbili za Kamati za Kudumu za Bunge, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria na Kamati ya Kudumu ya Bunge Sheria Ndogo bungeni  jijini, Dodoma jana. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Mbunge huyo wa Siha aliyehama Chadema na kujiunga CCM amesema tukio la Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 ni mpango uliosukwa na Chadema ingawa hakuwa tayari kuthibitisha madai yake.


Dodoma. Mbunge wa Siha (CCM), Dk Godwin Mollel amesema tukio la Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 jijini Dodoma ni mpango uliosukwa na Chadema na kutoa sharti kwa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania kuwa wakilitimiza atakuwa tayari kuthibitisha.

Dk Mollel, mbunge wa zamani wa Siha kwa tiketi ya Chadema aliyejiunga CCM mwaka 2018 na kupitishwa kuwania ubunge na kuibuka na ushindi, ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Februari 8, 2019 bungeni jijini Dodoma.

Amesema hata siku ya kufanya uchunguzi baada ya Lissu kupigwa risasi, kuna baadhi ya sampuli aliziiba lakini uongozi wa Chadema ulikataa pendekezo lake la kupeleka sampuli hiyo Afrika Kusini kufanya uchunguzi kwani walikuwa na hofu ya kuumbuliwa.

“Mimi nilikuwa huko lakini nilikimbia kwa mipango yao,  hata katika tukio la kushambuliwa Lissu mimi niliingia ndani kwenye uchunguzi na niliiba baadhi ya vitu lakini wakakataa mapendekezo yangu," amesema Mollel.

Hata hivyo, mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka aliomba taarifa akimtaka Dk Mollel kueleza ni kwa nini alikuwa anakiuka kiapo cha udaktari, na mbunge huyo wa Siha kujibu kuwa alifanya hivyo kwa sababu alikuwa kada mwaminifu wa Chadema.

Wakati Mwakajoka akieleza hayo, mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alimtaka Dk Mollel kuthibitisha madai yake kuhusu Lissu.

Katika majibu yake Dk Mollel amesema hawezi kuthibitisha hadi Chadema watakapomueleza fedha za ruzuku zinakwenda wapi na mpango waliotaka kuufanya kwa Zitto Kabwe (mbunge wa Kigoma Mjini) na marehemu Chacha Wangwe, walipotaka kugombea uenyekiti wa Chadema.