Mke wa bilionea Msuya ‘akiri’ kumuua wifi yake

Muktasari:

  • Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita alisema mshitakiwa, Miriam Mrita ambaye ni mke wa Bilionea Msuya, alikiri kumuua wifi yake kwa kumchinja katika mauaji yaliyofanyika Mei 25, 2016.

 

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya Aneth Msuya, dada wa marehemu bilionea Erasto Msuya, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mshtakiwa wa kwanza, Miriam Mrita, ambaye ni mke wa Erasto alikiri kumuua wifi yake.

Maelezo hayo yametolewa jana na wakili wa Serikali mwandamizi, Patrick Mwita wakati akisoma maelezo ya mashahidi katika kesi hiyo akisaidiana na wakili wa Serikali Faraji Nguka.

Walisoma maelezo hayo kuanzia saa 5:15 asubuhi hadi saa 9:55 alasiri baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika na kufungwa katika mahakama hiyo kwa ajili ya kuhamishia Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji.

Katika kesi hiyo ya uchunguzi wa mauaji namba 5 ya mwaka 2017, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, washtakiwa Mariam na mwenzake Revocatus Muyella, wanaotetewa na wakili Peter Kibatala, wanadaiwa kumuua kwa makusudi Aneth kwa kumchinja akiwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, Mei 25, 2016.

Bilionea Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi kwa bunduki ya kivita ya Sub Machine Gun (SMG), Agosti 7, 2013 eneo la Mijohoroni wilayani Hai.

Akisoma maelezo ya mashahidi katika kesi hiyo, wakili Nguka aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa Mariam baada ya kukamatwa, Agosti 7, 2016 akihojiwa na askari Koplo Mwaka, mrakibu msaidizi wa Polisi (ASP) Jumanne na WP Latifa Mohamed, alikiri kuhusika katika mauaji ya wifi yake.

Wakili Nguka alidai kuwa Mariamu alieleza kuwa aliamua kumuua wifi yake kutokana na mgogoro wa mali za mumewe (bilionea Msuya) na kwamba pia alikuwa na hasira kutokana na Aneth (Marehemu) kumtumia picha za kumkashifu umbile lake.

Amedai kuwa mshtakiwa alieleza kuwa Aneth alikuwa akimtumia picha za wanawake wenye maumbile makubwa mabaya, wenye matumbo makubwa, jambo ambalo lilimfanya apate hasira.

Kwa mujibu wa Wakili Nguka, mshtakiwa Mariam baada ya kuchukizwa na kitendo cha wifi yake kumtumia picha hizo, aliamua kutafuta ushauri kwa mshtakiwa wa pili Muyella, ambaye alimshauri kuwa huyo dawa yake ni kumuua tu.

Amedai kuwa mshtakiwa huyo alieleza kuwa ndipo walipopanga na kutekeleza mauaji hayo, huku mshtakiwa wa kwanza akimuahidi mshtakiwa wa pili kumlipa Sh20 milioni kwa kazi hiyo.

Wakili Nguka alieleza kuwa mshtakiwa alieleza kuwa alimlipa mshtakiwa wa pili Sh10 milioni za awali wakiwa jijini Dar es Salaam na kwamba baada ya kutekeleza mauaji hayo ndipo alipommalizia Sh10 milioni nyingine jijini Arusha.

Hata hivyo, Wakili Mwita aliieleza kuwa baada ya kumkamata na kumhoji, mshtakiwa wa pili alikubali kumfahamu Mariam kuwa ni mfanyabiashara mwenzake na alikuwa akifahamiana na marehemu mumewe, lakini alikana kuhusika na mauaji hayo.

Licha ya kukana kuhusika katika mauaji hayo, wakili Mwita aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa huyo alitambuliwa kwenye gwaride la utambuzi na Getrude Mafuru, msichana wa kazi wa marehemu Aneth.

Wakati mawakili hao wa Serikali wakiendelea kusoma maelezo hayo, baadhi ya ndugu wa marehemu Aneth walikuwa wakilia huku mshtakiwa Mariam akionekana kubasamu.

Miongoni mwa ndugu wa Aneth waliokuwa wakilia ni dada yake mkubwa, Happy Msuya ambaye alishindwa kuendelea kusimama na kukaa chini hadi karani wa Hakimu Simba alipomtafutia kiti.

Dada mwingine wa marehemu Aneth aitwaye Esther Msuya, ambaye pia aliwahi kunusurika kuuawa kwa kupigwa risasi yeye na mumewe, alionekana akilia mara kwa mara na kila alipotulia alionekana kunywa na maji na kisha kuendelea na kilio.

Upande wa mashtaka baada kueleza hayo, umedai kuwa utakuwa na mashahidi na jumla ya mashahidi 45 na vielelezo zaidi ya 14.

Awali kesi hiyo iliwahi kufutwa na Hakimu Godfrey Mwambapa, Februari 23, 2016, kutokana na upelelezi kuchelewa kukamilika, katika kesi ya awali namba 32 ya mwaka 2016 .

Hata hivyo washtakiwa hao walikamatwa tena na baadaye kusomewa mashtaka upya ya mauaji hayo.