Mshahara wa Lissu wamfanya Spika ajiulize maswali manne

Wednesday February 13 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Job Ndugai amemtwanga Tundu Lissu maswali manne kuhusu madai ya kutolipwa mshahara wake huku akisema, “akitegemea kulipwa na hela za walipakodi maskini na yeye yuko Marekani malipo hayapo hivyo katika awamu hii ya Awamu ya Tano.”

Kauli ya Ndugai imetokana na swali aliloulizwa na mwandishi wetu baada ya mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema) kukaririwa akisema kwamba amepata taarifa za mshahara wake kuzuiliwa. Alisema hayo akiwa California, Marekani katika mkutano wake na Watanzania waishio nchini humo.

Lissu yupo katika ziara nchini humo baada ya kutoka hospitali Ubelgiji anakodai amepewa kibali cha kutembea wakati akiendelea na matibabu.

Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu mshahara wa Lissu, Ndugai alisema, “mpigieni yeye muulizeni huenda watu wa benki yake wana matatizo, muulize (Lissu) yupo wapi. Huko ulipo bosi wako (Ndugai) anajua. Kama anazurura kama alivyosema Musukuma (Joseph Kasheku – mbunge wa Geita) anataka mshahara upi wa kuzurura?”

katika maelezo yake kwenye mkutano huo, Lissu alisema, huku akitaka usahihi kutoka kwa mkewe aliyekuwa pembeni yake, “nimenyang’anywa mshahara juzi au jana, sio? Sasa jamani hawajanivua ubunge, walisema watanivua ubunge kwa sababu ya utoro na Spika hana taarifa niko wapi. Hawajanivua ubunge angalau tusikate tamaa katika hili lakini wameninyang’anya mshahara.”

Alisema kwa mujibu wa Katiba, sheria ya uendeshaji wa Bunge na kwa kanuni za Bunge, namna pekee ya kugusa mshahara wa mbunge ni iwapo amesimamishwa kuingia bungeni.

Advertisement

“Ukipelekwa kwenye kamati ya maadili na ikapendekeza uadhibiwe kwa kusimamishwa kuingia bungeni na Bunge likipitisha azimio hilo, kanuni za Bunge zinasema utalipwa nusu mshahara na nusu ya posho unazostahili kama mbunge,” alisema Lissu.

“Kuna uwezekano wa kufutwa ubunge. Katiba inasema mbunge asiyehudhuria mikutano mitatu mfululizo ya Bunge bila taarifa ya Spika unaweza ukafutwa ubunge, ukifutwa huwezi kulipwa mshahara.

“Mimi sijafutwa ubunge, sijasimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge lakini nimesimamishiwa mshahara kwa sababu watu wanasema Lissu amepona ndio maana anazurura kwa mabeberu.”

Februari 7, bungeni jijini Dodoma Musukuma alihoji ni lini Bunge litasitisha mshahara wa mbunge huyo aliyedai kuwa amepona na sasa anaitukana Serikali akiwa nje ya nchi.

Alihoji ni lini chombo hicho cha Dola kitasitisha mshahara wake akisema kwamba tayari mbunge huyo amepona lakini hajaripoti bungeni.

Akijibu mwongozo huo wa Msukuma, Spika Ndugai alisema suala hilo linahitaji kuangaliwa kwa upekee, “Jimboni hayupo, bungeni hayupo, nchini hayupo, hospitali hayupo na mimi sina taarifa yoyote wala ya daktari. Hoja yako ina msingi iko haja ya kusimamisha mshahara wake,” alisema Ndugai.

Awali, Januari 31 akiwa bungeni, Ndugai alieleza kuwa hadi mwishoni mwa Desemba mwaka jana, Lissu alikuwa amelipwa Sh207.8 milioni pamoja na Sh43 milioni zilizotolewa kama mchango wa matibabu ya mbunge huyo na kwamba hadi sasa Lissu amelipwa jumla ya Sh250milioni kutoka bungeni.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa malipo hayo Ndugai alisema, “hayo mie sisemi sana hiyo ndiyo mikeka yangu, nasubiri tu akanushe.”

Kuhusu madai ya jana ya mbunge huyo ambaye pia ni mnadhimu mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Spika Ndugai alisema, “Nani amemuambia bwana (kuhusu mshahara), kama mkuu wake wa kazi (Ndugai) sijui yupo wapi hilo ndio ninalolijua mengine hayo aangalie vizuri hesabu zake na kadhalika.”

Mwananchi lilipomtaka Lissu, kutoa ufafanuzi kuhusu kauli yake hiyo aliyoitoa Marekani alisema, “Si umuulize Spika Ndugai aliyesema wanasimamisha mshahara wangu? Mimi sijaangalia kama wameingiza pesa au la. Nilikuwa nazungumza alichokisema Spika Ndugai.”

Alipoulizwa kuhusu stahiki za mbunge anayeugua, Ndugai alisema akifuata utaratibu wa matibabu na kulazwa nje ya nchi, kitanda, chakula na huduma zote anazopata zinalipiwa hivyo hawezi kupewa fedha ya kujikimu.

“Wanaopelekwa nje ni watu wa kulazwa na huwa na malipo madogo sana, Serikali huilipa hospitali kidogo, kama ni hela ya kupewa mgonjwa ni token. Lissu yeye hayajui hayo anapiga hesabu ya mtu anayekwenda kushiriki mkutano,” alisema Ndugai.

Alisema mbunge ambaye anaugua lakini yupo nyumbani, kwa maana ya Tanzania au hotelini, “halipwi chochote kama yupo Tanzania. Ila ikiwa ni mbunge wa Sumbawanga na anatibiwa Dar es Salaam lakini haishi hospitali, atalipwa nusu ya fedha yake ya kujikimu ya Serikali sijui kwa sasa ni 80,000 au 120,000.”

Huku akicheka alisema wagonjwa hawana kipato na ingekuwa hivyo wangeumwa wengi.

Advertisement