Mtoto wa Ruge amuombea msamaha baba yake

Mwachi ambaye ni mtoto wa kwanza wa marehemu, Ruge Mutahaba 

Muktasari:

Amesema kwa niaba ya familia wanaomba wamsamehe baba ili apumzike kwa amani

 


Dar es Salaam. Mwachi ambaye ni mtoto wa kwanza wa marehemu, Ruge Mutahaba amemuombea msamaha baba yake kwa watu aliowakosea enzi za uhai wake.

Mwachi aliyasema hayo leo Jumamosi Machi 2, 2019 wakati akisoma wasifu wa baba yake katika shughuli za kumuaga zinazoendelea katika viwanja ya Karimjee jijini Dar es Salaam.

“Ninamuombea msamaha baba yangu kwa wale wote aliowakosea enzi za uhai wake, nasi tunawasamehe wote waliomkosea baba,” amesema Mwachi ambaye ni mmoja kati ya watoto watano wa marehemu huku kauli hiyo ikizidisha simanzi kwa waombolezaji

Amesema baba yake alikuwa mtu aliyejitoa kwa wengine mpaka familia ilifikia wakati inaona watu wa nje wanamfaidi kuliko wao.

“Alitenga muda mwingi kusaidia kwa kuzingatia misingi ya utu, alipambana kwa hali zote kufanikisha mambo mengi katika jamii,” alisema huku akijitahidi kujizuia kutoa machozi.

Amesema jamii inachoweza kufanya ni kuchukua jukumu la kusaidia japo Watanzania wawili, watafanikisha ndoto za wengi.

Miongoni mwa waombolezaji ni; Rais wa Tanzania, John Magufuli, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harison Mwakyembe pamoja na viongozi wengine wa Serikali.

Mwili wa Ruge uliwasili saa 4.00 asubuhi katika viwanja vya Karimjee ukitokea Hospitali ya Jeshi Lugalo ulipokuwa umehifadhiwa jana baada ya kuwasili kutoka Afrika Kusini.

Umati mkubwa wa waombolezaji waliowasili katika viwanja vya Karimjee kutoa heshima za mwisho wakiwamo wasanii wanafuatilia ibada ya kuaga mwili wa Ruge kupitia runinga mbalimbali zilizofungwa.

Waombolezaji wengi wameshindwa kufuatilia wasifu wa Ruge uliosomwa na Mwachi hasa eneo alipopata kigugumizi kutokana na huzuni wakijikuta wanalia.

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea