Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makosa manane yanayochochea ajali za bodaboda

Muktasari:

  • Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza watu katika nchi zenye kipato cha chini wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuhusika katika ajali za barabarani kuliko wale wenye uwezo mkubwa wa kiuchumi.



Dar es Salaam. Wakati Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) ikieleza majeruhi wa ajali za bodaboda ndio wanaoongoza kupokelewa hospitalini hapo, Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kimetaja makosa manane yanayofanywa na waendesha bodaboda likiwemo tabia ya kupenya katikati magari makubwa.

Katika miaka ya hivi karibuni, usafiri wa bodaboda umekuwa muhimu mijini na vijijini. Usafiri huo umebadilisha namna wananchi wanavyofika maeneo mbalimbali kwa haraka huku vikitoa ajira kwa maelfu ya vijana na kurahisisha shughuli za biashara.

Makosa mengine yaliyotajwa ni dereva na abiria kutovaa kofia ngumu (helmeti), kubeba zaidi ya abiria mmoja, kutumia simu wakati wa kuendesha, kuendesha baada ya kutumia pombe au dawa za kulevya, kutoheshimu alama na taa za barabarani, kuendesha bila leseni na kuendesha bila bima au usajili halali wa chombo husika.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Mambo ya Ndani zilizotolewa Februari 11, 2025, jumla ya wananchi 1,113 walipoteza maisha kutokana na ajali zilizohusisha pikipiki, maarufu bodaboda katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2024.

Takwimu hizo zilitolewa bungeni na aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye kwa sasa ni Naibu Spika,  Daniel Sillo, alipokuwa akijibu maswali ya wabunge kuhusu idadi ya wananchi waliopoteza maisha kutokana na ajali za pikipiki kati ya mwaka 2022 na 2024.

Vilevile  Shirika la Afya Duniani (WHO) linaonesha, takribani watu milioni 1.19 hufariki dunia kila mwaka kutokana na ajali za barabarani, majeraha yanayotokana na ajali hizo ndiyo sababu kuu ya vifo kwa watoto na vijana wenye umri wa miaka mitano hadi 29.

WHO inaeleza asilimia 92 ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani hutokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, licha ya nchi hizo kuwa na takribani asilimia 60 tu ya magari yote duniani.


Alichokisema Kamanda Mkonda

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, William Mkonda ametoa kauli hiyo huku rejea za takwimu za MOI za mwaka 2024 zikionesha kati ya Januari na Desemba hospitali hiyo ilipokea wagonjwa 8,202 katika kitengo cha dharura.

Kati yao, majeruhi ni 4,852 sawa na asilimia 59 walitokana na ajali za barabarani, miongoni mwa majeruhi hao  asilimia 21 walihusika katika ajali za magari na asilimia 38 walitokana na ajali za bodaboda.

Akizungumza na madereva wa bodaboda, bajaji na maguta jijini Dar es Salaam jana Jumamosi, Julai 4, 2026, Kamanda Mkonda amewataka viongozi wa vyama vya waendesha pikipiki kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi katika kudhibiti ajali hizo.

"Viongozi wa waendesha bodaboda, bajaji na maguta, endeleeni kutoa elimu kwa wanachama wenu na kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi kuzuia ajali na kudhibiti vitendo vya ukiukaji wa sheria,” amesema Kamanda Mkonda.

"Kutumia simu wakati wa kuendesha, kuendesha baada ya kutumia pombe au dawa za kulevya, pamoja na kutoheshimu alama na taa za barabarani si ukiukaji wa sheria pekee, bali ni vitendo vinavyoweka maisha ya madereva, abiria na watumiaji wengine wa barabara katika hatari kubwa," amesema.

Aidha, Mkuu huyo wa Kikosi cha Usalama Barabarani amewataka madereva wa bodaboda kuacha tabia ya kupenya katikati ya magari makubwa, akisema ajali nyingi zinazowahusisha waendesha pikipiki husababishwa na tabia hiyo.

"Tuache kupenya katikati ya malori na magari makubwa, ajali nyingi zinazosababisha waendesha pikipiki kukanyagwa hutokana na tabia hiyo. Tuongeze umakini katika shughuli zetu za kila siku ili tuendelee kuwa salama," amesema.


‘Hawana uwezo kulipa faini’

Kwa upande wake, Katibu wa Shirikisho la Waendesha Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam, Michael Riganya amesema changamoto kubwa inayowakabili madereva hao ni kulazimika kulipa faini papo hapo wanapokamatwa kwa makosa ya usalama barabarani.

Amesema madereva wengi wa bodaboda hawana uwezo wa kulipa faini hizo mara moja, hivyo ameiomba Serikali kuweka utaratibu wa kuwaruhusu kulipa ndani ya wiki moja, kama ilivyo kwa baadhi ya madereva wa magari.

"Dereva anapokamatwa anatakiwa kulipa faini papo hapo. Sisi tuna mfumo wa kidijitali wa kuwasajili madereva wa bodaboda, tunaomba mfumo huo uunganishwe na Jeshi la Polisi ili dereva anapopatikana na kosa aweze kutambulika na kuruhusiwa kulipa faini ndani ya siku saba," amesema.

Akijibu ombi hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, amewataka madereva bodaboda kujisajili ili watambulike kwa urahisi. Amesema sababu ya kutozwa faini papo hapo ni ugumu wa kuwapata wanapotenda makosa na kuondoka.

Hivi karibuni akizungumza na Mwananchi juu ya ajali za bodaboda, Balozi wa usalama barabarani, Ramadhani Msangi alisema miaka ya karibuni kumekuwa na ongezeko la njia nyingi za usafirishaji na kuzalisha ajira kwa vijana, lakini changamoto iliyopo ni kutokuwapo kwa mazingira yaliyokuwa yameandaliwa ili kuifanya sekta hiyo kuleta manufaa badala ya matatizo.

“Tunachoweza kufanya ni kuhakikisha sheria inaandaliwa kufanya sekta hiyo kuwa rasmi, kuhakikisha watu wanaotoa mikataba kwa vijana wajulikane, ili wanaoajiriwa wajulikane wana sifa zipi na kama wanafaa kuingia barabarani.

“Mikataba iwe na vipengele gani, ili kuhakikisha haimbani tu dereva bali hata mmiliki,” amesema Msangi ambaye ni mkurugenzi msaidizi wa elimu, habari na mahusiano wa Road Safety Ambassadors (RSA).

Alisema hatua hiyo itapunguza hatari barabarani na watu watajifunza huku kukiwepo sheria mahususi za bodaboda badala ya kutumia sheria ya usalama barabarani kwa ujumla.

“Pia usimamizi ni muhimu kwa kuwajua wako madereva hao wangapi na wanapatikana wapi, tukishirikiana na serikali za mitaa ambako ndiko vijiwe hivi vya bodaboda vinapatikana, itasaidia,” alisema.