Ndugai: Bunge limeshamlipa Tundu Lissu

Sunday April 7 2019

 

By Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema mhimili huo wa Dola umeshamlipa madai yake yote mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu huku akimwagiza kuwa kama ana jambo lolote kuwasiliana na mamlaka husika na si kutumia mitandao ya kijamii.

Ndugai alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na Mwananchi kwa simu ikiwa zimepita siku 10 tangu mnadhimu huyo wa kambi rasmi ya upinzani bungeni kumwandikia barua Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai akimtaka kumlipa mshahara na posho zake za kuanzia Januari, ndani ya siku 14 vinginevyo atashtaki mahakamani.

Machi 27, Kagaigai alipoulizwa kama amepata barua hiyo, alisema hajaipata lakini wakili wa Lissu, John Mallya alisema kwamba aliituma barua hiyo kwa wahusika kwa njia mbili, moja ikitumwa ofisi ndogo ya Bunge Dar es Salaam kwa njia ya kitabu cha hati ya kupokea kwa kutia saini (dispatch) na nyingine kwa EMS.

Lissu alibainisha kuwa mawakili wake waliandika barua hiyo kutaka alipwe mshahara na posho zake za kibunge za tangu Januari, 2019.

Kabla ya kuthibitisha kwamba mbunge huyo ameshalipwa madai yake, Ndugai alisema, “pale bungeni hatumuonei mtu hata kidogo labda nikate simu yako niangalie kama kweli amelipwa ninaweza kufanya kazi hiyo,” alisema Ndugai na baadaye kupiga simu na kueleza kuwa Mnadhimu huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni tayari ameshalipwa, “wameshamlipa,” alipoulizwa amelipwa madai gani alisema, “usitake tena… yaani hana madai. Kama ana madai mengine atasema.”

Advertisement

Mbunge huyo amekuwa nje ya nchi tangu Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi katika makazi yake Area D jijini Dodoma. Mpaka sasa yupo Ubelgiji akiendelea na matibabu.

Katika maelezo yake, Ndugai alisema Lissu anatumia njia zisizo nzuri kueleza masuala yake, likiwamo hilo la madai yake.

“Hii si njia nzuri ya mawasiliano. Ninachosisitiza mtu ni mtumishi katika taasisi unatakiwa kuwajibika kwa watu fulani fulani lakini huwatambui huwasiliani nao,” alisema Ndugai.

Alimshauri Lissu kutafuta ufumbuzi wa masuala yake ya bungeni kupitia viongozi mbalimbali wa upinzani.

“Haki ya mtu ni haki ya mtu, siwezi kusimama katikati ya haki ya mtu… sifuatiliagi mshahara wa mtu mmojammoja mwisho wake nitahamia uhasibu,” alisema Ndugai huku akicheka.

Alisema huenda kulikuwa na shida ya huduma ya malipo ya kibenki au fedha kuchelewa, “ni kama ilivyo kwa malipo ya mahala popote pa kazi, mfano hata makandarasi wanadai.”

Hata hivyo, Mwananchi lilipomtafuta Lissu kujua kama kweli amelipwa alisema apewe muda awasiliane na watu wa benki kisha akishapata majibu atarejea. Lakini hadi saa 1:30 jioni alikuwa hajapata majibu kutoka benki kutokana na kuwa nje ya nchi.

Advertisement