Nusu siku ya nguvu kwa Mbowe, Matiko

Muktasari:

Viongozi hao wa Chadema kesho wanatarajia kuwa mbele ya Jaji Sam Rumanyika kujua hatima ya kesi yao waliyofungua wakipinga kufutiwa dhamana yao na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mwishoni mwa mwaka jana

Dar es Salaam. Hatima ya rufaa kupinga kufutiwa dhamana na kupelekwa mahabusu kwa viongozi wawili waandamizi wa Chadema inatarajiwa kujulikana ndani ya nusu siku ya leo katika Mahakama Kuu jijini hapa.

Viongozi hao, mwenyekiti, Freeman Mbowe na mhazini wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Esther Matiko wanaopinga kufutiwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, watakuwa mbele ya Jaji Sam Rumanyika kusikiliza hatima ya shauri lao baada ya jana kukamilisha usikilizwaji.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo jana, mawakili wa pande zote walichuana vikali kila upande ukijitahidi kuishawishi Mahakama Kuu, kuwa Mahakama ya Kisutu ama ilikosea au ilikuwa sahihi kuwafutia dhamana hiyo.

Katika rufaa hiyo, warufani hao kupitia kwa mawakili wao, Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya walitoa hoja mbili; walidai kuwa Mahakama ya Kisutu ilikosea kuwafutia dhamana kwa sababu za kushindwa kufika mahakamani wakidai kuwa siku ambazo hawakuwepo mahakamani, wadhamini wao walikuwapo na walieleza sababu za kutokufika kwao.

Wakili Kibatala alidai kuwa hata siku ambayo walifutiwa dhamana, warufani wenyewe walikuwapo mahakamani na kwamba hapakuwa na sababu za msingi za kuwafutia dhamana hiyo.

Katika hoja ya pili, wakili Mtobesya alidai kuwa Mahakama ya Kisutu ilikosea kuwafutia dhamana warufani hao bila kuwapa kwanza nafasi wadhamini wao fursa ya kujieleza.

Alifafanua kuwa dhamana ni mkataba baina ya Mahakama na mdhamini ambaye anaahidi kuhakikisha kuwa mshtakiwa anakuwapo mahakamani siku zote ambazo anahitajika.

Alidai kuwa wakishindwa kufanya hivyo, kuna utaratibu wa kuwafutia dhamana ambao kwanza ni kuwataka wadhamini wajieleze ni kwa nini dhamana waliyowawekea isifutwe,” katika kesi hii wadhamini walikuwepo na cha kushangaza dhamana ilifutwa bila wao kutakiwa kusema chochote kuhusu dhamana hiyo.”

Katika kujenga hoja zao, mawakili hao walirejea hukumu za kesi mbalimbali zilizowahi kuamuriwa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani zenye mazingira yanayofanana na rufaa hiyo.

Wakijibu hoja hizo, jopo la mawakili watano wa Serikali likiongozwa na mawakili wa Serikali wakuu, Faraja Nchimbi na Paul Kadushi lilidai kuwa hoja za warufani hao hazina mashiko kisheria, huku pia wakirejea kesi mbalimbali.

Wakili Jackline Nyantori alidai kuwa kufutwa kwa dhamana za washtakiwa hao halikuwa jambo la siku moja, bali mchakato uliotokana na mwenendo wao wa kushindwa kufika mahakamani kwa nyakati mbalimbali na kwamba kabla ya hapo walikuwa wameshaonywa mara kadhaa.

Huku akitaja tarehe tofuatitofauti ambazo warufani hao hawakuwepo mahakamani na ambazo mahakama ilikuwa imeshawapa onyo, wakili Nyantori alidai kuwa tabia hiyo ilikuwa inachelewesha hata usikilizwaji wa kesi kwa makusudi na kwamba Mahakama ina mamlaka kudhibiti mwenendo wa mashauri yake.

Alidai kuwa washtakiwa kuwapo mahakamani si sababu ya Mahakama kutokuchukua hatua kwani ilishatolewa amri ya kuwakamata ili wajieleze ni kwa nini wasifutiwe dhamana kwa makosa hayo.

Alisisitiza kuwa kabla ya kuwafutia dhamana, iliwapa nafasi ya kujieleza wao pamoja na wadhamini wao na kwamba baada ya Mahakama kupima maelezo yao, iliona kuwa hayana msingi, kwani maelezo yao na ya wadhamini wao yalikuwa yanajikanganya.