Polepole ampongeza Lowassa kwa ukomavu wa kisiasa

Muktasari:

Leo Jumamosi, Edward Lowassa amepokewa rasmi ndani ya CCM baada ya kujiunga na chama hicho Machi Mosi, 2019 akitokea Chadema


Monduli. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amempongeza Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa kwa kuonyesha ukomavu wa kisiasa kwa kurejea CCM na kuweka siasa pembeni kwa kujali Taifa

Akizungumza katika hafla ya kumpokea Lowassa na wanachama wengine wa upinzani  jana viwanja vya CCM wilaya ya Monduli, Polepole alisema Taifa linataka amani, taifa linataka mshikamano, taifa linataka umoja, taifa linataka kusonga mbele.

Polepole alisema kitendo cha Lowassa ni ishara madhubuti ya ukomavu, kwa kuweza kuweka pembeni siasa na kujali taifa mbele.

Alisema kitendo cha Lowassa ni ishara madhubuti ya ukomavu wa kisiasa. “Leo kwa roho njema ya kupatana tunasimama pamoja, tukachape kazi tupeleke mbele taifa letu la Tanzania,”alisema Polepole.

Polepole alisema Lowassa amefuata taratibu zote za kujiunga CCM, baada ya kikao cha tawi analotoka kukubali kurejea CCM, ikifuatiwa na kikao cha kamati ya siasa ya kata nyumbani ambao wamekubali arejee CCM.

“Napenda kukupa habari njema bwana Lowassa, kikao cha tawi kimeridhia kujiunga na CCM, kama haitoshi kikao cha kamati ya siasa ya kata leo kimekaa na kukubali, leo asubuhi, kamati ya siasa ya halmashauri kuu ya wilaya na kikao kimeridhia kurejea CCM,” alisema Polepole.