R, Kelly matatani tena kwa ngono za watoto

Friday July 12 2019

 

Washington, Marekani. R. Kelly amekamatwa tena akituhumiwa kuhamamisha watoto katika masuala ya ngono, gazeti la New York Times limeripoti ikiwa ni kesi mpya baada ya nyota huyo wa muziki wa R&B kukumbwa na kashfa kadhaa za ngono.
Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 52, ambaye kisheria anaitwa Robert Kelly, alipelekwa mahabusu na mawakala wa serikali wa Chicago jana Alhamisi jioni, gazeti hilo limeripoti.
Waendesha mashtaka wa serikali wametoa mashtaka 13 dhidi ya mwimbaji huyo, ambayo yanajumuisha kuhamamisha watoto walio chini ya umri unaotakiwa na kuzuia mashtaka, mwanasheria msaidizi wa serikali ya Marekani, Joseph Fitzpatrick aliliambia gazeti hilo.
Waendesha mashtaka wanadai matukio hayo yalitokea kati ya mwaka 1998 na 2010.
Kelly ana historia ya muda mrefu ya tuhuma za masuala ya ngono, hasa dhidi ya wasichana wenye umri mdogo, na aliepuka mashtaka ya ngonom kwa watoto karibu miaka kumi iliyopita.
Mwaka 1994 alimuoa mwanamuziki aliyekuwa akimsimamia, Aaliyah, nyota wa muziki wa R&B ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 15.
Kelly, ambaye wakati huo alikuwa na miaka 27, alisimia utayarishaji wa albamu ya kwanza ya Aaliyah iliyopewa jina la "Age Ain't Nothing But a Number (Umri Hauna Maana Zaidi ya Namba)."
Harusi yao ilibatilishwa baadaye, na Aaliyah akafariki katika ajali ya ndege mwaka 2001.
Licha ya tuhuma zake kutomaliza, R. Kelly, ambaye ameshinda tuzo kadhaa na ambaye anajulikana kwa nyimbo nyingi ukiwemo wa "I Believe I Can Fly (Naamini Nawewza Kupaa)" -- ameendelea kufanya maonyesho na kuendelea kuwa na mashabiki wengi.
Lakini hali ilianza kubadilika mwezi Januari baada ya kutolewa makala ya video ya sehemu sita iliyoitwa jina la "Surviving R. Kelly."
Makala hiyo, ambayo inamtuhumu Kelly kujihusisha na kunyanyasa kingono, kiakili na kimwiliwasichana wadogo na wanawake, iliwastua waendesha mashtaka wa Chicago na kuanza kuwasaka walionyanyaswa.
Kabla ya tukio la jana, Kelly alikuwa nje kwa dhamana baada ya kushtakiwa kwa makosa matano ya aina hiyo.
Alikaa mahabusu siku tatu na aliachiwa baada ya kutoa dola 100,000 ambayo ni asilimia 1 ya dhamana ya dola 1 milioni iliyopwekwa na mahakama.
Akipatikana na hatia ya kosa lolote kati ya hayo, Kelly atakabiliwa na hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa kila kosa.
Mwezi Machi, Kelly alikanusha kwa nguvu mashtaka dhidi yake, akisema "anapigania" maisha yake.
"Sikufanya haya mambo," aliiambia CBS News.
"Iwe ni tuhuma za zamani, mpya au za baadaye si za kweli," alisema katika mahojiano na kituo cha televisheni na baadaye kuangua kilio.

Advertisement