Ubalozi wa Tanzania Ujerumani wamjibu Lissu

Sunday February 3 2019

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk Abdallah Possi ametoa tamko akijibu madai ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyoyatoa hivi karibuni nchini humo alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha News Africa cha kituo cha televisheni cha Deutsche Welle (DW).

Lissu ambaye kwa sasa yuko nchini Ubelgiji akiendelea na matibabu kufuatia shambulio la risasi la Septemba 7, 2017 jijini Dodoma amekuwa akiituhumu Serikali kuhusika huku akihoji sababu ya kutokamatwa kwa mshukiwa yeyote, mbali pia na madai ya ukandamizwaji wa demokrasia nchini.

Akijibu madai ya Lissu katika tamko lake la Januari 29, 2019, Dk Possi amesema Serikali imekuwa ikilifuatilia suala hilo ikiwa ni pamoja na kuanza uchunguzi.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa taarifa ya kulaani tukio hilo na kuagiza uchunguzi wa kina wa haraka. Kwa nyakati tofauti Rais amemtuma Makamu wake, Rais mstaafu na viongozi wengine wa Serikali kumtembelea Lissu akiwa hospitali akiwa Dodoma, Nairobi na Brussels (Ubelgiji).”

“Ni vema sasa mbunge angepima ishara hizo njema za Rais kwenye madai anayotoa yasiyo na msingi,” amesema Dk Possi katika tamko lake.

Kuhusu madai ya kutochunguzwa kwa tukio hilo, Dk Possi amesema mamlaka za Serikali zingetaka kumpata Lissu ili atoe ushirikiano wa taarifa kuhusu tukio hilo.

Advertisement

Ameongeza uchunguzi ulishaanza mara tu baada ya tukio hilo lakini umeshindwa kuendelea kwa sababu ya kutopata ushirikiano kutoka kwa mbunge huyo.

“Hadi sasa vyombo vya sheria hawajapata ushirikiano wa mbunge huyo na dereva wake ili kupata taarifa muhimu za siku hiyo. Uchunguzi kwa Tanzania bado ni muhimu na bado unawasubiri wao kwa kuwa walishuhudia kwa macho ili waeleze kilichotokea,” ameongeza Dk Possi.

Kuhusu malalamiko ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuwa gerezani, Dk Possi amesema bado hajafungwa, bali utaratibu wa kutoa dhamana ni wa kimahakama na unasimamiwa na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

“Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Dar es Salaam ilisimamisha dhamana baada ya kuvunjwa kwa masharti kwa kutokuwepo mahakamani bila sababu ya msingi. Ubalozi unaendelea kusisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwa imara katika demokrasia,” alisema.

Kuhusu taarifa ya Rais kwa vyama vya upinzani ambayo Lissu alidai kuwa Rais alishatangaza kuwa hataki kuona vyama vya upinzani ifikapo mwaka 2020, Dk Possi alisema madai hayo hayana msingi.

“Kwenye nchi yoyote ya demokrasia ya vyama vingi, kuendelea au vinginevyo  kunategemea jinsi vilivyojipanga kuuza itikadi zao na sera zao. kama vile Lissu na wanachama wa chama chake ambavyo wamekuwa wakisema wataiondoa CCM kwenye uwanja wa siasa,” alisema Dk Possi.

 

Advertisement