MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA: Ungamo la mshtakiwa lagusa wengi

Tuesday April 16 2019

Ndugu jama na marafiki wakiwa ndani ya chumba

Ndugu jama na marafiki wakiwa ndani ya chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, wakisubiri usikilizwaji wa kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa kidato cha pili Humphrey Makundi wa Shule ya Sekondari ya Scolastika iliyopo Himo wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro. Picha na Dionis Nyato 

By Daniel Mjema na Janet Joseph, [email protected]

Moshi. Mshitakiwa wa kwanza, Hamis Chacha anadaiwa kukiri kumpiga kwa ubapa wa panga na kisha kumuua mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Sekondari ya Scolastica, Humphrey Makundi.

Katika maelezo ya ungamo yaliyopokelewa mahakamani jana kama kielelezo namba P8, mshitakiwa aliyekuwa mlinzi, anadaiwa kukiri kuua, lakini akadai hakufahamu ni mwanafunzi wa shule hiyo.

Mbali na kudaiwa kutoa maelezo hayo, lakini mshitakiwa huyo anadaiwa kueleza alivyowasiliana usiku huo kwa simu na mshitakiwa wa pili, Edward Shayo na mshitakiwa wa tatu Laban Nabiswa.

Katika maelezo hayo yaliyosomwa jana na shahidi wa 14 wa upande wa mashitaka Irene Mushi, inadaiwa Shayo ambaye ndiye mmiliki wa shule ya Scolastica, alitoa wazo la mwili kutupwa mtoni.

Shahidi huyo ambaye ni Hakimu waMahakama ya Mwanzo Moshi Mjini, alidai aliandika maelezo hayo Novemba 20, 2017 baada ya mshitakiwa kukubali kwa hiyari yake kutoa maelezo bila kushurutishwa.

Maelezo hayo yalisomwa mahakamani baada ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Firmin Matogolo, kulitupilia mbali pingamizi lililowekwa na jopo la mawakili wa utetezi.

Mawakili hao, Elikunda Kipoko, David Shillatu, Wakisa Sambo na Patrick Paul, walipinga maelezo hayo wakidai uchukuaji wake una dosari kisheria na mshitakiwa hakuyatoa kwa hiyari yake.

Jaji baada ya kupitia hoja za kisheria na kusikiliza kesi ndani ya kesi ili kujiridhisha kama alitoa maelezo kwa hiyari ama la, alitupilia mbali pingamizi hilo na kupokea maelezo hayo kama kielelezo.

Akisoma neno kwa neno la maelezo hayo, shahidi huyo amemnukuu mshitakiwa akieleza kuwa Novemba 6,2017 saa 2:58 usiku, alisikia kishindo cha mtu akishuka (ukuta) na aliamua kufuatilia.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali mkuu, Joseph Pande anayesaidiana na mawakili wengine watatu kutoa ushahidi wake, Shahidi huyo alieleza kuwa Chacha alijitambulisha kama mlinzi wa Scolastica.

Mshitakiwa huyo anadaiwa kueleza kuwa alimulika tochi kuelekea eneo hilo na mtu huyo alianza kukimbia na yeye kumkimbiza na kwa vile alikuwa na silaha aina ya panga, alimpiga nalo kwa ubapa.

“Nilimpiga bapa mgongoni na aliendelea kukimbiana nikakimbizana naye, kuna sehemu alifika na kuanguka chini na alipasuka kwenye paji la uso. Baada ya hapo akawa katulia,”anaeleza na kuongeza;-

“Nikampiga bapa la pili na ndio mauti yalipomkuta pale pale. Nilimpigia simu mwalimu Laban nikamwambia kuna mtu nimemkimbiza lakini sijui kama ni mwanafunzi au mtu wa nje”.

“Ndipo mwalimu Laban ambaye ni mwalimu wa nidhamu akaja. Palepale akaniuliza nimeshampigia mkuu wa shule nikamjibu nishampigia, mzee wa shule Mzee Shayo anakuja.”

“Baada ya hapo nilimwambia mwalimu Laban inawezekana huyu mtu kazirai tumbebe tumpeleke hospitali, mwalimu Laban akadai tumsubiri Mzee Shayo. Mzee Shayo alivyofika ndio nikamueleza.”

“Mzee Shayo akamuuliza mwalim Laban unamfahamu huyu mtu, Laban alijibu naona kavaa sare za shule lakini siwezi kumfahamu kwa muda huu,” ananukuliwa mshitakiwa.

“Mzee Shayo akasema kama humfahamu kwa muda huu ukatupwe mtoni labda ni kibaka na mimi na mwalim Laban tulienda kumtupa mtoni,” anadaiwa kueleza Chacha na kuongeza;

“Tulivyomaliza kumtupa nilimwambia Laban akaitishe rokoo (roll call) labda ni mwanafunzi. Akaitisha roll call. Laban alinipigia simu wanafunzi wote wapo na mimi nilirudi ndani ya fence.”

“Nilivyoingia kwenye mabweni ya wanafunzi nilikuta kitanda kimoja hakuna mwanafunzi na muda ule sikujua kama ni wale waliomaliza kidato cha nne na nilimpigia mwalimu Laban,”

Akiendelea kusoma maelezo hayo, shahidi Irene siku iliyofuata, Chacha alieleza mwalim Laban alipanda kwenye mabweni ya wanafunzi na kuulizia kama kuna mwanafunzi hayupo.

“Wanafunzi walimjibu wote tupo. Usiku wa saa 2 mwalimu Laban aligundua mwanafunzi Humphrey Makundi hayupo. Hadi wanamaliza mtihani tarehe 7.11.2017 hakuonekana,” ananukuliwa Chacha.

“Nilimwambia mwalimu Laban lile suala linatakiwa lifanyiwe kazi, akanijibu tumeshatoa taarifa polisi na Mzee Shayo kasema atafuatilia hakutakuwa na tatizo lolote”.

“Jumatano kuamkia Alhamisi ndio wakampigia simu mzazi. Nilikuja kukamatwa siku ya Ijumaa saa 11 jioni nikiwa lindo shuleni Scolastica na tulipelekwa kituoni Himo.”

“Tulikaa pale kuanzia saa 11 hadi saa 1 usiku tukapelekwa Central Police Moshi mjini na kufika kituoni walinipiga polisi wengi ili nitoe maelezo sababu nilitofautiana na mlinzi mwenzangu”.

“Hadi leo tarehe 20.11.2017 niliomba mwenyewe kuja kutoa maelezo kwa mlinzi wa amani. Nakiri kuwa nimeua lakini sikufahamu kabisa kama yule alikuwa mwanafunzi wa pale Scolastica”.

Katika maelezo hayo, mshitakiwa alidai baadaye zilipatikana taarifa za maiti iliyoopolewa mtoni, lakini mwalimu aliyepewa jukumu la kufuatilia, alipofuatilia aliambiwa mwili huo ulizikwa na Manispaa.

Mwanafunzi huyo alitoweka shuleni Novemba 6, 2017, na baadaye kubainika ameuawa na watu wasiojulikana baada ya maiti yake kufukuliwa kwa amri ya mahakama na kubainika ni Humphrey.

Mwili wa mtoto huyo uliokotwa Novemba 10, katika Mto Ghona, mita zipatazo 300 kutoka shuleni hapo, na polisi waliouchukua waliupeleka Hospitali ya Mawenzi na kuzikwa kwa madai haukutambuliwa.

Ushahidi wa Vinasaba (DNA) ambao ushapokelewa mahakamani kama kielelezo cha kesi hiyo, ulithibitisha kuwa mwili huo una vinasaba na Jackson Makundi na Joyce Makundi ambao ni wazazi.

Advertisement