VIDEO: CAG amjibu Ndugai, asema ana nia ya kuhojiwa

Muktasari:

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu  Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad  amesema ana nia ya kuitikia wito wa Spika Job Ndugai kwa sababu ofisi yake haiwezi  kufikia ufanisi unaohitajika katika utendaji wake kama ripoti zake hazifanyiwi kazi ya kuridhisha na Bunge


Dar es Salaam.  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu  Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad  amesema ana nia ya kuitikia wito wa Spika Job Ndugai kwa sababu ofisi yake haiwezi  kufikia ufanisi unaohitajika katika utendaji wake kama ripoti zake hazifanyiwi kazi ya kuridhisha na Bunge.

Profesa Assad ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Januari 17, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari huku akibainisha kuwa neno udhaifu ni la kawaida kwa wakaguzi katika kutoa maoni ya utendaji wa mifumo ya taasisi mbalimbali.

Mkaguzi mkuu huyo wa hesabu za Serikali ametoa kauli hiyo baada ya kuibuka mzozo kati yake na  Ndugai kutokana na Profesa Assad wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kusema kushindwa kutekelezwa kwa ripoti anazowasilisha bungeni huenda kunatokana na udhaifu wa chombo hicho kauli ambayo Ndugai alisema ni ya kudhalilisha Bunge na kumtaka kufika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Januari 21, 2019 kuhojiwa.

Amesema majibu yake yaliyozua mjadala hayakuwa na nia ya kuidhalilisha Bunge kama dhaifu bali ni lugha ya kawaida kwa wakaguzi katika kutoa maoni ya utendaji wa mfumo wa taasisi mbalimbali.

" Ni wazi kuwa watu wengine wanaweza kuchukua tafsiri tofauti ya maneno kama haya. Yametokea malumbano makali na marefui katika nyanja zote za mawasiliano kuhusu rai, nafasi na maamuzi mbalimbali yaliyochukuliwa na viongozi,” amesema Assad.

“Binafsi na ofisi ya Taifa ya ukaguzi hatuna namna ya kuathiri tafsiri za viongozi, wanasiasa na wachangiaji wa kawaida. Tunachoshauriana ni uungwana utawala katika mawasiliano.”

Amesema Januari 15, 2019 alipokea wito uliomtaka kufika katika kamati hiyo, kwa katika kudumisha mahusiano mazuri ana nia ya kuitikia wito huo Januari 21, 2019.

"Uhusiano huu una umuhimu ili kila moja ya pande hizi CAG na Bunge uweze kutekeleza majukumu yake ya kikatiba na kwa mantiki hiyo lazima uenziwe na kudumishwa, yaliyotokea hivi sawa hayatufurahishi na yanatusikitisha"