Wabunge CCM wampongeza CAG, wapingana na Zitto

Mbunge wa Mbinga Mjini Mjini, Sixtus Mapunda

Muktasari:

Leo wabunge wa CCM wamezungumza na waandishi wa habari ambapo wamempongeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kwa kuitikia wito wa kamati ya bunge ya haki, maadili na madaraka ya bunge ili kuhojiwa kuhusu madai ya kudharau na kudhalilisha chombo hicho.

Dodoma. Wabunge wa CCM wamempongeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kuitika wito wa  kamati ya bunge ya haki, maadili na madaraka ya bunge licha ya kuwapo propaganda za watu mbalimbali zinazoenezwa kwenye vyombo vya habari na mitandao wa jamii.

Akizungumza leo jijini hapa, mbunge wa Mbinga Mjini Mjini, Sixtus Mapunda kwa niaba ya wabunge wenzake wa chama hicho, alisema hatua ya CAG kukubali kuhojiwa na bunge ni ya  kiungwana.

"Tunapenda kutumia fursa hii kumpongeza sana kwa uungwana wake na nia ya kutii wito wa mamlaka ya Spika na bunge.”

“Sisi wabunge wa CCM tuna imani kuwa hatua hii itaendelea kudumisha na kuboresha mahusiano mazuri ya ofisi ya CAG na ofisi ya bunge katika kutumikia umma," alisema Mapunda.

 

Pia, wabunge hao wamempongeza Spika, Job Ndugai kwa jitihada za kulinda heshima ya mhimili wa bunge kwa kusimamia sheria ya kinga, madaraka na haki za bunge.

Wabunge hao wamesema kitendo cha mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe kufungua kesi na kuandika barua kwa katibu mkuu wa mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) pamoja na wadhibiti na wakaguzi wakuu juu ya hatua ya Spika kumpeleka CAG katika kamati hiyo ni kudharau mamlaka ya Spika.

Mapunda alisema Zitto ni mbunge mkongwe ambaye anazielewa taratibu za kikanuni zinazosimamia shughuli za bunge hivyo wamemshangaa kwa hatua yake hiyo.