Wadaiwa kubugia ARV bila kupima

Muktasari:

Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Kupambana na Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Leonard Maboko amesema Watanzania wengi wana mwamko wa kutumia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV) kuliko kujua hali zao.

Dar es Salaam. Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Kupambana na Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Leonard Maboko amesema Watanzania wengi wana mwamko wa kutumia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV) kuliko kujua hali zao.

Dk Maboko alibainisha hayo jana wakati akizindua mpango mkakati wa miaka mitano wa taasisi ya kupambana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi ya Agpahi.

“Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa asilimia 90 ya wajawazito wanajua hali zao kati yao, asilimia 98 wanatumia dawa za ARV. Hata hivyo, utafiti uliofanyika ilibainika kuna watu hawajui hali zao lakini walipopimwa damu zilionyesha tayari wanatumia ARV,” alisema.

Awali, mkurugenzi mtendaji wa Agpahi, Dk Sekela Mwakyusa alisema kupitia mpango huo wanatarajia kupanua wigo wa huduma ili kufika maeneo mengi zaidi na kuhakikisha maambukizi kwa watoto wanaozaliwa yanakoma.

“Hivi sasa tunatoa huduma mikoa minne ya Kanda ya Ziwa tunatarajia kupanuka zaidi. Mpango wetu huu utakaoisha 2023 tunatarajia kumaliza maambukizi kwa watoto,” alisema.