VIDEO: Walichokisema wananchi baada ya Bundi kutua bungeni

Muktasari:

Jana nyakati za asubuhi na jioni Bundi alionekana ndani ya ukumbi wa Bunge huku Spika Job Ndugai akiwatoa hofu wabunge, lakini kupitia swali lililoulizwa na Mwanachi katika mitandao ya kijamii kuhusu Bundi huyo kuonekana bungeni, wananchi wameeleza mambo mbalimbali, baadhi wakidai ni ishara mbaya

 


Dar es Salaam. Wananchi mbalimbali wametoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuonekana kwa Bundi  ndani ya ukumbi wa Bunge jijini Dodoma, wengi wao wakihusisha tukio hilo na imani za kishirikina.

Leo Jumatano Januai 30, 2019 Mwananchi limeuliza swali katika mitandao ya kijamii ya Facebook, WhatsApp na Twitter linalosema, je Bundi anapoonekana inaashiria nini?

Kufutia swali hilo wananchi mbalimbali wametoa maoni yao.

Bundi huyo alionekana bungeni jana asubuhi na Spika, Job Ndugai aliwatoa hofu wabunge kuwa ndege huyo kuonekana ni jambo la kawaida lakini jana jioni ndege huyo alionekana tena ndani ya jengo la Bunge.

Katika mtandao wa Facebook, Abdul Mngwale amesema “Ina maana walichoazimia kukifanya hakikuwa sahihi, matokeo yataonekana ndani ya siku 21 baada ya kuidhinishwa. Kwa wale ambao hawajawahi kumuona bundi, ni ndege mwenye kichwa cha paka.”

Charles Shayo amesema “kule kwetu Moshi Bundi ni ishara mbaya, akija kulilia nyumbani kwako, inaashiria habari za kifo, huenda kikatokea maeneo hayo kwa wanaoamini hivyo.”

Christian Saleh ameandika “Inaashiria kiongozi mkuu wa wote wa mahali hapo anapotua bundi atakufa akiwa amesimama bila kuumwa, kwa hiyo kana yupo ajikabidhi mikononi mwa Mungu ili aelekee peponi, akishupaza shingo anaenda jehanam.”

Kennedy Manengo ameandika “Tanzania tumepeleka imani zetu kwenye imani za kishirikina, ila kwa nchi zilizoendelea wao wangeamini kwenye tekinologia ya ujasusi, hapo ndio tunapotofautiana na wazungu.”

Katika mtandao wa Instagram, wananchi pia wametoa mawazo yao:  Yahaya Abrahman ameandika “Atakufa mtu mkubwa hapo.”

Deogratius Luhulula ameandika “Mara nyingi huwa ni huzuni na muda siyo mrefu basi hutokea huzuni yaani msiba.”

“Bundi ni ndege ambaye huwa anasikia harufu ya mzoga wa mtu kabla hata hajafa, maana mwanadamu mpaka siku anakufa huwa anaanza kuumwa taratibu na hatimaye kifo, hivyo hapo bungeni kuna mzoga, tusubiri,” ameandika Mbeti Mbeti

Katika mtandao wa Twitter, Steven Kyando ameandika “Kwa kawaida Bundi ni ndege ambaye anafanya mawindo yake muda wa giza usiku. Kwa ishara ya Bundi kuonekana ndani ya Bunge watafakari moja ya ishara mbaya.”

Kighera Kighera ameandika “haiashirii kitu chochote, wanaweza ishi kwako kutokana na mazingira rafiki, mimi ninapoishi pana miti mingi sana na bundi wa kumwaga. Tunaishi vizuri, wao juu ya miti, mimi chini.”

El Diablo amesema, “Niliipata sehemu: Wanasema binadamu unaweza ukafa lakini ukawa hai for almost two weeks (kwa takribani wiki mbili). So (kwa hiyo) maeneo ambayo Bundi wanaenda lazima wanakua wameishanusa harufu ya mtu mfu, so wanamvizia kama mzoga. Ndio dhana ya uchuro wa Bundi ilipotokea.”