Wito kupinga Bunge kutofanya kazi na Profesa Assad watua kwa Spika

Muktasari:

  • Wito wenye lengo la kumuunga mkono Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Assad umekuwa ukiendeshwa kwa njia ya mtandao na ulianzishwa siku chache baada ya Bunge kupitisha azimio la kutofanya kazi na CAG

Dar es salaam. Wakati kampeni ya mtandaoni kupinga azimio la Bunge la kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad  ikifikisha zaidi ya watu 15,000, waraka wa kampeni hiyo umefikishwa katika ofisi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai

Waandaaji wa kampeni hiyo ambao ni Taasisi ya Change Tanzania wamesema leo Jumatatu Aprili 8, 2019 kuwa maoni hayo yaliyokusanywa yamefikishwa ofisi ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam na mengine yakitarajiwa kutumwa jijini Dodoma kuanzia kesho Jumanne.

Mmoja ya waratibu wa kampeni hiyo, Msabaha Hamza Msabaha amesema maoni hayo yanafikishwa leo mchana.

“Tunapeleka katika ofisi ndogo za Bunge hapa Dar es Salaam na mengine tutayatuma kwa ofisi za Bunge Dodoma,” amesema wakati akiwa njiani kwenda ofisi za Bunge.

Kampeni hiyo iliyoanzishwa Aprili 3, 2019 siku moja baada ya Bunge kuazimia kutofanya kazi na CAG Profesa Assad, imelenga kukusanya sahihi za wananchi kutoka sehemu mbalimbali kupinga hatua hiyo.

Wengi waliochangia maoni yao kwenye mtandao wamekuwa wakielezea namna walivyo tayari kusimama bega kwa bega na Profesa Assad. Wengi wanataka Bunge liendeshe mambo yake kwa kuzingatia matakwa ya kikatiba na si vinginevyo.

“Bunge liongozwe kwa kutumia sheria na ripoti ya CAG ipokelewe na kujadiliwa,” ameandika mchangiaji aliyejitambulisha kwa jina la Seleman Mfaume huku mshiriki mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Elinasi Monga akiandika kuwa “maamuzi ya Bunge hayana mashiko yoyote”.

Tangu Bunge lipitishe azimio lake kumekuwa na maoni mbalimbali kuhusiana na sakata hilo huku CAG mwenyewe akionya uwezekano wa kuzaliwa mgogoro wa kikatiba.

Wiki iliyopita Bunge la Tanzania lilipitisha azimio la kutofanya kazi na CAG baada ya kumtia hatiani kwa tuhuma za kudharau chombo hicho.

Wabunge wamefikia uamuzi huo baada ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kutaka waridhie mapendekezo yao dhidi ya CAG.

Kamati hiyo ilimhoji CAG Januari 21 baada ya kufanya mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York mwezi Desemba 2018 ambapo alisema kuwa Bunge la Tanzania halina meno na hivyo limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo Serikali.

Akizungumza na TBC, CAG Profesa Assad alisema suala hilo linaweza kuwa kubwa kuliko lilivyo sasa na kutaka busara itumike zaidi ili kupata ufumbuzi.

"Tunaweza kuwa na mgogoro wa kikatiba, kwamba ripoti (za ukaguzi wa mwaka 2017-18) zimeshawasilishwa kwa Rais na mimi siwakilishi ripoti Bungeni, basi Rais atazipeleka ndani ya siku sita kama Bunge likikataa kuzipokea hilo ni tatizo kubwa zaidi. Ni dharau (kwa katiba) wasiwasi wangu ni huo. Zikiwasilishwa bungeni zinakuwa mali ya umma na mimi napata nafasi ya kuzungumza, na hilo pia linaweza kuwa tatizo. Tafsiri ya kuwa (Bunge) hatuwezi kufanya kazi na CAG ni tafsiri pana sana na inatakiwa tuijue vizuri," alisema.