Zitto alifikisha sakata la Spika Ndugai, CAG ngazi za kimataifa

Muktasari:

Profesa Assad ameingia kwenye mzozo na Bunge la Jamhuri ya Muungano baada ya kusema katika mahojiano na idhaa ya Kiswahili ya kituo cha televisheni cha Umoja wa Mataifa kuwa chombo hicho cha kutunga sheria hakitekelezi majukumu yake kama inavyotakiwa na kusababisha Spika Job Ndugai amuite mbele ya Kamati ya Maadili na Hadhi ya Bunge kujieleza.


Dar es Salaam. Mzozo ulioibuka baina ya Spika Job Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad limepelekwa ngazi nyingine baada ya kongozi wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe kumuandikia barua katibu mkuu wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA), Akbar Khan akimtaka kuingilia kati.

Katika barua hiyo, ambayo Zitto amewatumia pia maspika wote wa nchi wanachama wa CPA na wanasheria wakuu, Zitto amesema sakata hilo lilianza baada ya Profesa Assad kusema anaamini kuwa kutotekelezwa kwa ripoti anazozitoa, ni udhaifu wa Bunge.

Zitto, ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini, amesema maoni hayo yamemfanya Spika Ndugai kumtaka Profesa Assad kufika mbele ya kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili ahojiwe na kujieleza.

“Mimi binafsi nimeguswa na suala hili. Naomba mabunge ya Jumuiya ya Madola muingilie kati si tu kwa sababu agizo la Spika Ndugai linavunja Katiba bali pia ni hatari kwa mustakabali wa Jumuiya ya Madola kwa ujumla,” ameandika Zitto katika barua hiyo.

Zitto amesema kama CAG ataadhibiwa na kamati ya Bunge kwa kutoa maoni yake, basi ni wazi kwamba uhuru wa Taasisi ya Juu ya Ukaguzi (SAI) utakuwa umevunjwa, kinyume na makubaliano yaliyofikiwa na kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola mwaka 2013.

Kila mwaka CAG hutoa ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali, taasisi zake na mashirika ya umma na kumkabidhi Rais na baadaye Bunge kwa ajili ya kuhoji sehemu zenye udhaifu na kufanyia kazi mapendekezo yake.

Suala lililoibua utata hivi karibuni ni kutoonekana kwa Sh1.5 trilioni katika matumizi ya Serikali, jambo ambalo Profesa Assad alisema wanaotakiwa kuhoji zilipo fedha hizo ni Bunge.

Profesa Assad alisema anaamini kuwa fedha hizo zilitumika katika matumizi mengine ya Serikali, lakini alisema kama zilitumike hivyo, Bunge lilitakiwa lijulishwe na baadaye kuidhinisha matumizi hayo.