Lissu kwa Zitto ni ujasiri

Muktasari:

 

  •   Zitto ameandika kuhusu ujasiri kutokana na alivyomuona Lissu

Mbunge wa Kigoma Mjini(ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameeleza ujasiri ni nini baada ya kumtembelea Mbunge wa Singida Mashariki(Chadema), Tundu Lissu anayendelea na matibabu jijini Nairobi.

Lissu anaendelea na matibabu jijini Nairobi baada ya kushambuliwa na risasi na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma.

Zitto baada ya kumtembelea hospitalini aliandika, “Ujasiri ni nini

Zitto Kabwe
Nimetumia wikiendi iliyopita kumsabahi ndugu Tundu Lissu jijini Nairobi. Nimerudi nikiwa mwenye unyenyekevu zaidi kwasababu ya nguvu na ujasiri ambao kaka yangu ameuonyesha licha ya kuwa kwenye maumivu makali.

Si mara nyingi hapa nchini utasikia tukiongelea ujasiri. Lakini namfikiria Lissu na vile nilivyojisikia nikiwa pamoja naye Nairobi. Najua hivyo ndivyo alivyo. Waliomshambulia wamemuumiza. Wamemuumiza kweli. Na bado wakati tuliokuwa naye amenionyesha shukrani, ari na pia ucheshi. Huo ni ujasiri.

Alichopitia na anachoendelea kupitia Lissu sio kitu rahisi kwa mtu yoyote kutafakari. Kufikiria hali ile kungeniacha nimeumia moyo Sana kama asingesema maneno haya kwangu "tumeshinda. Tumeshashinda".

Ujasiri ni Lissu