Kilichomponza Okello baada ya kuongoza Mapinduzi

Muktasari:

Kabla ya mapinduzi, Zanzibar ilitawaliwa na Sultani ikiwa himaya ya Uingereza. Ilipata uhuru Desemba 10, 1963, japo Serikali ya Zanzibar haikuitambua siku hii.

Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yaliyouondoa utawala wa Sultani yametimiza miaka 55. Haya ndiyo yaliiangusha serikali ya mseto ya vyama vya Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Peoples Party (ZPP).

Zanzibar ya kale iliyoongozwa na Sultan ilijulikana kama Zenj ilikuwa visiwa vya Unguja, Pemba, Mafia, Mombasa na Lamu. Makao makuu yalikuwa Mji Mkongwe, Unguja.

Kabla ya mapinduzi, Zanzibar ilitawaliwa na Sultani ikiwa himaya ya Uingereza. Ilipata uhuru Desemba 10, 1963, japo Serikali ya Zanzibar haikuitambua siku hii.

Kumbukumbu ya mapinduzi

Watu wa Zanzibar waliamka Januari 12, 1964 na kukukuta hali tafauti na ilivyokuwa walipokwenda kulala.

Mfalme wa Zanzibar, Sultan Jemshind bin Abdulla bin Khalifa bin Harouh el Busaidy alikuwa amepinduliwa.

Jemshid anaishi Porstmouth, Uingereza na aliyekuwa Waziri Mkuu wake na kiongozi wa ZPPP, Sheikh Mohamed Shamte Hamad alifariki akiwa Dar es Salaam.

Kiongozi wa ZNP, Ali Muhsin Barwany, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Sheria, aliiaga dunia Dubai alipokuwa akiishi.

Mengi juu ya mapinduzi yanasimuliwa, lakini zaidi hutegemea utashi wa mtu, alivyohadithiwa na kuongeza au kupunguza uhalisia, kwa ama kujipendekeza au kuhofia usalama wake.

Kama ilivyo sarafu, mapinduzi ya 1964 yanayo pande mbili. Wapo wanaoelezea mazuri tu na wengine hujikita kuzungumzia mabaya.

Lisilo shaka, ijapokuwa wapo watu wanaotaka isielezwe ni kwamba mapinduzi yalikuwa na umwagaji damu. Upo utata wa idadi ya waliokufa, waliojeruhiwa na waliodhalilishwa wakati wa mapinduzi na baada ya hapo, walioachwa mayatima na hasara iliyopatikana.

Ukisikiza maelezo ya mapinduzi hutaamini yaliofanyika Zanzibar iliyosifika kuwa watu wake ni wapole na karimu.

Nimeyaona na kusikia mengi juu ya mapinduzi, ikiwa pamoja na kuelezewa na watu walioyaandaa na kuyatekeleza.

Tokea mdogo, nilikuwa karibu na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume. Niliwafahamu wasaidizi wake na wengine walikuwa walimu wangu wa shule au kukaa nao katika baraza na kuwasikia wakitoa dondoo zilizohusu mapinduzi.

Tangu Desemba 10, 1963 (Zanzibar ilipopata uhuru), viongozi wa Afro-Shirazi Party (ASP) walioongozwa na Karume na wa Umma Party walioongozwa na Abdulrahman Mohamed Babu hawakuridhia visiwa hivyo kuongozwa na mseto wa ZNP na ZPPP.

Kinachoaminika kuchochea mapinduzi ni serikali ya mseto ambayo baada ya kukabidhiwa utawala na Uingereza iliwafukuza kazi askari polisi wengi wenye asili ya Bara walioiunga mkono ASP wakati wa kutafuta uhuru.

Kutokana na hilo, hali ilikuwa ya wasiwasi na polisi walifanya doria mjini Unguja asubuhi na usiku. Lakini walipigwa changa. Januari 11 palitayarishwa fete (burdani ya bahati nasibu, ngoma na biashara) katika uwanja wa Mapipa ya Ngozi.

Hapo palikuwa pakianikwa ngozi za ng’ombe na mbuzi juu ya mapipa na ndipo yalipokuwa makao makuu ya ASP. Jengo hili sasa ni ofisi kuu ya CCM Zanzibar.

Hii fete ilitayarishwa na Umoja wa Vijana wa ASP.

Tangu asubuhi ya Januari 11, askari walifanya doria, lakini jua lilipotua walirudi kambini na kurudisha silaha ghalani.

Nilichogundua ni kuwa mpango wa mapinduzi ulijumuisha makundi tofauti.

Yalikuwepo makundi yenye mitazamo iliyokinzana, lakini yote lengo lao lilikuwa kuiondoa madarakani serikali ya Sultani.

Lilikuwapo kundi liliongozwa na Saleh Saadalla Akida na Abdallah Kassim Hanga na jingine liliongozwa na Seif Bakari na Abdulla Said Natepe.

Ali Lumumba ndiye aliyewakutanisha viongozi wa ASPYL na John Okello aliyeongoza mapinduzi.

Viongozi wa chama hicho na wa chama cha Zanzibar Communist Party walivutia vijana kutokana na kila aliyehutubia kutoa visa na kushambulia ukoo wa kifalme na matajiri.

Lumumba na viongozi wengine wa chama walioshiriki kufanya mapinduzi ni pamoja na Juma Musa (Jimmy Ringo) na Saleh (Mavi ya Mbuzi) aliyewahi kuwa sheha wa Kikwajuni.

Hii inayoonyesha mbali ya viongozi wa ASP kuelezwa kuwa ndio waliofanya mapinduzi, lakini ulikuwapo mchango wa viongozi wa vyama vingine vya siasa.

Walioanza mashambulizi walikuwa katika makundi yaliyovamia wakati mmoja kutoka pande tafauti kambi ya Polisi ya Bomani (sasa Ziwani) usiku wa manane wa kuamkia Januari 12.

Katika kundi moja walikuwemo askari walioachishwa kazi baada ya uhuru. Kiongozi wao alikuwa Said Idi Bavuai aliyekuja kuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na baadaye waziri.

Katika kundi hili walikuwamo Lumumba na Ramadhani Haji aliyekuwa Waziri Kiongozi wakati Aboud Jumbe Mwinyi akiwa Rais wa Pili wa Zanzibar.

Kundi jingine liliongozwa na Aboud Mmasai (Mngazija aliyefanana na Wamasai) na wengine ni Yusuf Himidi.

Wengine ni Mohammed Abdulla (Kaujore), Pili Khamis na Kopa (baba wa Khadija Kopa).

Kinachoshangaza ni kuona watu waliobeba silaha na kupindua serikali husikii mchango wao ukitajwa badala yake hujitokeza waliokuwa majumbani wakati mapinduzi yakifanyika.

Wakati mapigano ya yalipopamba moto, makundi hayo yaliongezewa nguvu na kundi lilioongozwa na John Okello na hatimaye kuiteka kambi ya polisi.

Okello alikuwa pamoja na Khamis Darweish, Absalom Engen (msaidizi wa Okello) na Juma Abdulla (Mabodi), baba wa Abdulla Juma Mabodi, sasa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar.

Usiku ule milio ya risasi ilisikika mjini Unguja na watu wengi walijiuliza kulikoni mpaka ilipopatikana taarifa asubuhi za kufanyika mapinduzi.

Aliyetoa tangazo la kwanza la mapinduzi ni Mdungi Ussi, mmoja wa waasisi wa ASP.

Alifanya kazi Sauti ya Unguja mpaka katika miaka ya mwisho ya 1950 na kustaafu alipoingia kwenye siasa na baada ya mapinduzi alichaguliwa mkuu wa kituo cha radio.

Muda mfupi baada ya tangazo la Mdungi yalisikika matamshi ya mtu ambaye si mzaliwa wa Zanzibar wala ukanda wa pwani wa Afrika ya Mashariki. Alijitambulisha kwa kusema: “Mimi ni Field Marshal Okello. Amkeni, hapana tena serikali ya kibeberu Visiwani. Hivi sasa ipo serikali ya wapigania uhuru. Amkeni watu weusi. Kila mmoja achukue bunduki au silaha nyingine kupambana na mabaki ya mabeberu. Msichoke kama mnataka kisiwa hiki kuwa chenu.”

Okello aliapa kuwateketeza waliopinga mapinduzi na kuwataka mawaziri wa Sultan kusalimu amri na kufika Rahaleo, karibu na jengo la Sauti ya Unguja.

Hapo ilianzishwa kambi ya kuwaweka kizuizini waliodaiwa kupinga mapinduzi.

Wakati taarifa ya Okello ilipotolewa ilisikika milio ya risasi Malindi huku watu wakiuawa sehemu mbalimbali za Unguja.

Maelezo niliyopata ni kwamba waliojaribu kuvamia kituo cha polisi cha Malindi walipata upinzani mkali. Mapambano yalichukua saa tano mpaka kituo kilipotekwa na maiti nyingi kuzagaa hapo.

Uvamizi huo uliongozwa na Amour Dugheish, kijana wa chama cha Umma na alikuwa pamoja na Ahmed Maulid (aliwahi kuwa Mkuu wa Itifaki wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania).

Vilevile walikuwamo vijana wengi wa ASP na wa Chama cha Umma. Hawa vijana wa Umma walikuwa wamepata mafunzo ya siri ya kijeshi katika jangwa la Sinai, Misri 1961 na baadaye katika kambi ya jeshi ya Playa Marianao, Cuba, 1962.

Vijana waliopata mafunzo Misri na Cuba walikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Jeshi la Ukombozi la Watu wa Zanzibar.

Miongoni mwao ni Shaaban Salim, Hashil Seif, Salim Saleh, Ali Mshangama, Hemed Hilal, Abdulla Juma (Bulushi), Ali Baalawy na Musa (Meki).

Mapambano ya Malindi yalipopanda moto mfalme alikwenda bandarini na kuelekea Dar es Salaam.

Maeneo nyeti yalipokuwa yakitekwa Aboud Jumbe, Saleh Saadala na Abdulaziz Twala walisimamia ulinzi wa kituo cha radio.

Kazi ya kukamilisha mapinduzi ilimalizwa Januari 13 kwa kutekwa jela ya Kiinua Miguu (Chuo cha Mafunzo, Kilimani) na aliyeongoza zoezi alikuwa Hemed Hilal, sasa anaishi Denmark pamoja na Hashil Seif.

Wafungwa, wakiwemo waliohukumiwa kifo, waliachiwa huru na gereza kuwa tupu. Mmoja wa wafungwa alikuwa Mohamed Humud aliyehukumiwa kifo kwa kuua.

Mohamed alikamatwa tena na kuuawa akiwa jela. Mtoto wake, Humud, aliyekuwa mwanajeshi baada ya Mapinduzi akiwa na vijana wengine wanne ndio waliomuua kwa risasi Rais Karume Aprili 7, 1972.

Mawaziri walisalimu amri siku ileile ya

Januari 12 na wengine kupigwa na kuteswa walipojisalimisha.

Baada ya mawaziri kusalimu amri watu waliendelea kuuawa majumbani kwao na maduka kuporwa.

Okello alishtua watu alipotangaza kuwa viongozi wa serikali iliyopinduliwa wangenyongwa na wengine kutumikia vifungo vya muda mrefu.

Baada ya kutoka tangazo la Okello, Babu aliwaambia waandishi wa habari kuwa amri ya Okello ya kuua watu imefutwa.

Baadaye Karume alitangaza hakuna atakayeuawa na hii ilionyesha kutoelewana kati ya Okello na viongozi wa ASP na Umma Party.

Hanga niliyefahamiana naye kwa karibu kama Mzee Karume na mawaziri wengi aliwahi kuniambia, “Karume aliposikia Okello amesema mawaziri wangeuawa, alishtuka na kusema, ‘Ebo! mshenzi huyu. Haiwezekani. Sisi si washenzi na akafanye ujahili kwao Uganda’”.

Baadaye Okello alifukuzwa Zanzibar.