MAONI: Kukaliwa kwa ripoti ya operesheni tokomeza kunawaumiza wananchi

Muktasari:

Lilikuwa mwiba kwa kuwa sasa inaelekea miaka mitatu toka ilipofanyika Operesheni Tokomeza na kuundwa kamati ya Bunge ambayo ilitoa ripoti yake na kuiangusha Serikali kwa maana mawaziri wanne waliachia ngazi huku maazimio yake yakimtaka rais achukue hatua ikiwa ni pamoja na kuunda Tume ya Kijaji.

Katika mjadala wa Wizara ya bajeti ya Maliasili na Utalii moja ya swali mwiba liliibuliwa na wabunge ni juu ya taarifa ya Operesheni Tokomeza ambayo kimsingi Serikali iliahidi kuwasilisha bungeni.

Lilikuwa mwiba kwa kuwa sasa inaelekea miaka mitatu toka ilipofanyika Operesheni Tokomeza na kuundwa kamati ya Bunge ambayo ilitoa ripoti yake na kuiangusha Serikali kwa maana mawaziri wanne waliachia ngazi huku maazimio yake yakimtaka rais achukue hatua ikiwa ni pamoja na kuunda Tume ya Kijaji.

Operesheni Tokomeza ilifanyika kwa mwezi mmoja kuanzia Oktoba 4 hadi Novemba 2013 na kusitishwa na Bunge. Tangu wakati huo mpaka sasa Serikali haijawahi kukamilisha upelelezi. Pamoja na kuwa taarifa ya kijaji ilishatolewa ikiwa na mapendekezo ya nini kifanyike, bado Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alitoa jibu rahisi bungeni akisema: “Suala hilo bado linafanyiwa uchunguzi na kuwa liachwe mpaka litakapokamilika.” alisema hivyo bila kuweka wazi uchunguzi huo ni dhidi ya nini na nani anahusika na ni mpaka lini.

Maana taarifa hiyo ni muhimu kwa umma. Ni suala lililoligharimu taifa kuunda kamati mbili; ya Bunge na Rais kwa gharama za umma.

Operesheni Tokomeza ililenga kunusuru maliasili za umma kutokana na kukithiri kwa ujangili.

Itakumbukwa kuwa Mei 1, 2014 aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete aliunda Tume iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Jaji mstaafu, Hamisi Msumi na Katibu wake, Fredrick Manyanda na ilipewa hadidu rejea sita na zote zimo kwenye taarifa yao hiyo, ambayo watendaji wa Serikali walipaswa kuwa wameifanyia kazi ili kupunguza baadhi ya migogoro ambayo inaendelea sasa.

Tume hiyo ilitumia siku 265 kwa kutembelea wilaya 38 katika mikoa 20 na kuhoji mashahidi 259 katika mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa, Mbeya, Kagera, Geita, Shinyanga, Simiyu, Mara, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Morogoro, Pwani, Tabora, Singida, Manyara, Arusha na Tanga.

Wakati hayo yanafanyika Masaju alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mwishoni akawa ni Mwanasheria Mkuu, kwa kifupi anajua nini kilichokwishafanyika.

Hapa najiuliza huo uchunguzi anaosema sasa unaendeshwa na nani? Maana Tume hiyo ilikabidhi taarifa ya uchunguzi Aprili 10, 2015 kwa Kikwete ikiwa ni baada ya kukamilisha uchunguzi wake.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni Operesheni Tokomeza ilivyotekelezwa, kama walizingatia sheria, kanuni, taratibu, kama walikiuka sheria wakati wa utekelezaji dhidi ya wakosaji na mali zao. Na kupendekeza hatua zinazostahili kuchukuliwa dhidi ya maofisa wa Operesheni Tokomeza waliokiuka sheria, Kanuni, taratibu na kupendekeza mambo yanayopaswa kuzingatiwa kupanga na kutekeleza iwapo itaendelea ili kuzuia malalamiko kama yaliyotokea.

Mambo mengi yalibainika ikiwamo vifo, kujeruhi, kudhalilishwa na wapo waliokufa wakiwa chini ya mikono ya askari, uporaji wa mali, viongozi au watu huru kutokushirikishwa wakati wa upekuzi na yapo mambo yaliyoongezwa chumvi na kupoteza maana halisi ya zoezi zima.

Kupitia Ripoti ya Tume ya Kijaji, jambo la muhimu kwao walilochukua lilikuwa ni kuwasafisha Mawaziri wote waliojiuzulu bungeni, Dk Emmanuel Nchimbi, Balozi Khamis Kagasheki, Mathayo David na Shamsi Vuai Nahodha kuwa hawakuhusika na Makosa yaliyotokana na utekelezaji wa operesheni hiyo na kwamba waliwajibika kisiasa.

Hivi Mwanasheria Mkuu ambaye kimsingi ndiye mshauri wa Rais kwa masuala ya sheria hajui kuwa Watanzania kupitia Bunge walishapewa baadhi ya taarifa ya matokeo ya Tume ya Kijaji ikiwamo kuwasafisha mawaziri waliohusishwa na sakata hilo?

Kuna watu wamejenga ndani ya hifadhi, kuna mapori Serikali ilisema hayazalishi na kuwa kuna haja ya kuyabadilisha matumizi ili wapewe wakulima, utekelezaji ungefanyika huenda kasi ya migogoro kati ya wafugaji na wahifadhi ingekuwa imepata majawabu.

Migogoro ni gharama kubwa kuitatua, hivyo kukalia taarifa ama kutokukamilisha upelelezi kwa wakati kama alivyojibu si kwamba kunaisaidia Serikali badala yake kunaiingiza kwenye gharama kubwa.

Pia, majibu kama hayo yanakinzana na dhamira ya Rais John Magufuli aliyoitoa Februari 4, mwaka huu katika kilele cha Siku ya Sheria Duniani akihimiza vyombo vinavyohusika kuharakisha uchunguzi wa mashauri mbalimbali ili haki iweze kutendeka.

Nategemea Ofisi ya Mwanasheria Mkuu iwe kielelezo ya kustawi haki kwa kushughulikia tatizo hili.

Mchambuzi ni mwandishi wa gazeti hili mkoani Mara (0759891849).