Tabia nne unazozihitaji kama kiongozi bora kazini

Tafiti zinaonyesha kuwa mafanikio ya taasisi yanategemea kwa kiasi kikubwa, tabia za mtu mwenye dhamana ya kufanya maamuzi yanayohusu wafanyakazi wa taasisi husika.

Kiongozi akikosa sifa, ni vigumu walio chini yake kufanya wajibu wao.

Migogoro, kutokuelewa, hujuma, utegeaji, kukosa hamasa ni baadhi ya athari zinazoweza kuzaliwa na uongozi usio na sifa.

Ingawa tunaweza kusema mengi yanayohusu wajibu wa mfanyakazi lakini bila kiongozi kuwa na sifa, itakuwa vigumu kupata ufanisi unaotakikana.

Katika makala haya, tunaangalia tabia nne muhimu unazozihitaji kiongozi ili kujenga hamasha ya watu kuyfanya kazi.

Mazingira bora ya kazi

Hamasa ya kazi inaanzia kwenye namna unavyomwezesha mfanyakazi kutekeleza kazi yake bila vikwazo. Utendaji wa kazi, kwa mfano, unategemea upatikanaji wa vitendea kazi vya msingi. Hakikisha vitendea kazi anavyovihitaji mfanyakazi wako vinatosheleza.

Pia, weka mazingira yanayomwezesha mfanyakazi kutumia vipaji vyake ipasavyo. Moja wapo ya sababu zinazoongeza motisha ya kazi ni mtu kuona mamna gani anaweza kutumia uwezo alionao kikamilifu. Weka mazingira yanayompa fursa hiyo.

Kadhalika, masilahi mazuri yanampa mfanyakazi utulivu wa nafsi. Mfanyakazi mwenye msongo wa mawazo wa namna atakavyoendesha maisha yake, hawezi kuwa na hamasa ya kufanya kazi kwa kujituma. Mlipe mfanyakazi wako kiwango kinacholingana na makubaliano mliyojiwekea.

Kuaminika na kuheshimika

Kila binadamu analo hitaji la kuaminiwa. Unapokuwa na uhakika mtu unayemheshimu anakuamini unakuwa na motisha ya kufanya vizuri zaidi kukidhi imani yake. Kama kiongozi kazini, unahitaji kuwa na tabia ya kuonyesha unaamini utendaji wa watu wako pasipo kuwaingilia bila sababu.

Unaweza kuonyesha imani kwa namna nyingi. Kwa mfano, badala ya kumfuatilia mtu kwa karibu mno, mpe kiasi fulani cha uhuru wa kufanya kazi kwa namna anayoona inafaa muhimu asiharibu kazi.

Hitaji kuona matokeo ya kazi badala ya kudhibiti kila kinachofanywa ikiwa si lazima.

Kadhalika, kuwaamini wafanyakazi kunakwenda sambamba na kuwaheshimu. Heshima kwa watu walio chini yako, iweni kwa maneno na vitendo vyako; hii inakutengenezea mazingira ya kuheshimiwa. Epuka kuonekana unawadharau watu kwa kuwatendea kama watoto.

Hata pale wanapokuwa wamekosea onyesha staha kwa namna unavyoshughulika makosa yao. Jifunze kudhibiti hasira hata pale unapokuwa na sababu ya kuhalalisha kuudhika mbele ya kadamnasi.

Kutambuliwa na kushirikishwa

Kutambuliwa ni kuonyesha kuelewa nafasi ya mfanyakazi wako kwenye ofisi, idara, kampuni au taasisi.

Unapomtambua mfanyakazi, unamfanya ajisikie kuthaminiwa. Kwa mfano, kufahamu jina na kumtambua kwa nafasi aliyonayo inatuma ujumbe kuwa unathamini uwepo wake.

Kadhalika, namna bora ya kuthibitisha kuwa unawatambua wafanyakazi wako ni kuwafanya wajione ni sehemu ya taasisi au kampuni yako. Washirikishe kwenye maamuzi hata kama unajua wewe ndiye mwenye sauti ya mwisho. Omba mawazo ya watu waliochini yako. Onekana ukiandika mawazo unayoyapokea. Kile kinachowezekana kufanyiwa kazi, kitekeleze. Unapofanya hivi kwa dhati watu watakuwa na ari ya kazi.

Kueleweka kwa malengo

Moja wapo ya mambo yanayofanya watu wakose ari ya kazi, wakati mwingine ni kutokueleweka kwa malengo ya taasisi. Hali hii hufanya kila mtu ajikute anafanya kile kinachomjia kichwani ili naye aonekane anachapa kazi.

Fanya jitihada wafanyakazi wajue kampuni au taasisi inalenga kufika wapi. Malengo ya muda mrefu na ya muda mfupi yaeleweke. Kwa mfano, kama ni kampuni, ifahamike mnataka kupata mafanikio gani katika kipindi cha mwaka mmoja. Kila mmoja aelewe mwelekeo wa pamoja.

Christian Bwaya ni mhadhiri wa Saikolojia na Unasihi, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya , 0754 870 815