Breaking News

Uchafu wa miji ni kero inayolalamikiwa na watalii

Thursday March 7 2019

 

By Gadiosa Lamtey na Julius Mnganga,Mwananchi [email protected]

Alipokuwa akifungua kongamano la kujadili hali ya mazingira mapema wiki hii, Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alisema Mji wa Tabora unapendeza kwa kuuangalia nje, lakini ukiingia ndani ni mchafu.
Kutokana na alichokiona wakatio akitembezwa mitaa tofauti, Samia alisema uongozi wa mkoa huo na wananchi wake wamejitahidi kuipendezesha Tabora kwa kupanda miti kwenye barabara mbalimbali za manispaa lakini hali hiyo ni tofauti ukiingia ndani ya mji huo.
 “Jicho langu linaona mbali kwelikweli. Huu usafi usiishie barabarani tu, tuufanye hadi tunakotoka,” alisema Samia.
Alichokiona Samia kwenye ziara yake mkoani Tabora ndicho kinachoonwa na wengi lakini kinawakera zaidi watalii  wanaokuja Tanzania. Kitendo cha makamu huyo wa Rais kushikia bango kaulimbiu ya ‘utunzaji wa mazingira kwa maendeleo ya Tabora’ ni miongoni mwa juhudi za kuhamasisha usafi wa miji.
Utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ikishirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) umebainisha uchafu kama kero inayohitajika kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo ili kuwaridhisha wageni wanaokuja kupumzika nchini.
Licha ya uchafu, ripoti hiyo inataja changamoto nyingine nne zinazohitaji kufanyiwa kazi ili kuboresha sekta hiyo nchini.
Matokeo yanaonyesha baadhi ya watalii hawaridhishwi na kiwango cha usafi wa miji na viwanja vya ndege. Kutoka na hali hiyo, ilishauri: “Ipo haja kwa mamlaka za miji kusimamia sheria na kanuni za usafi kwa kuongeza mapipa ya taka mtaani, vifaa vya usafi na kutoa elimu kwa wananchi.
Ripoti hiyo ijulikanayo ‘the 2017 Tanzania Tourism Sector Survey (TTSS),’ inaonyesha idadi ya watalii iliongezeka kwa asilimia saba mwaka 2017 na kufika zaidi ya bilioni 1.32 kutoka bilioni 1.23 ulimwenguni kote.
Wakati hali ikiwa hivyo ulimwenguni, nchini idadi hiyo iliongezeka kutoka zaidi ya milioni 1.28 mwaka 2016 hadi milioni 1.33 mwaka 2017.
Wakati taarifa za ripoti hiyo zinakusanywa, halmashauri ya mji wa Njombe ilitangazwa kuibuka kidedea katika mashindano ya Taifa ya afya na usafi wa mazingira yaliyohusisha halmashari za miji, majiji, manispaa na wilaya 73 mwaka 2017.
Njombe ilishika nafasi ya kwanza katika udhibiti wa taka ngumu, usimamizi wa sheria, udhibiti wa maji taka, uwepo wa maji safi na salama pamoja na ushirikishaji wa sekta binafi katika usafi wa mazingira.
Katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda anasema wanayafanyiakazi mapendekezo yote yaliyomo kwenye ripoti hiyo kuhakikisha fursa zaidi zinapatikana na wananchi pamoja na Taifa kwa ujumla linanufaika na vivutio vilivyopo.
“Kampeni ya usafi ni suala linalohusisha mamlaka nyingi. Tulipotoka ni kubaya zaidi kuliko tulipo…mamlaka za Serikali za Mitaa zinashindana. Hata mbuga zetu, usafi unaimarishwa sana siku hizi,” anasema Profesa Mkenda.
Changamoto nyingine
Ripoti inaonyesha wageni wengi waliokuja nchini walikaa kwa wastani wa siku 10 kwa miaka sita iliyopita hivyo kuhitaji jitihada za ziada hasa kuvitangaza vivutio visivyofahamika ili mtalii akija atumie siku nyingi zaidi kuvitembelea.
Ofisa mtendaji mkuu wa Chama cha Wakurugenzi wa Hoteli Tanzania (HAT), Nura-Lisa Karamagi anasema utalii upo zaidi kaskazini na Zanzibar maeneo kuliko kusini na maeneo mengine licha ya vivutio vilivyopo.

ali kutembelea Tanzania ukilinganisha na nchi nyingine hivyo kuna haja ya kuboresha eneo hilo ambalo kwa namna nyingine linaweza likawashawishi kukaa siku nyingi zaidi.
“Wizara ina kazi kubwa, wageni wakikaa nchini kwa muda mrefu itaongeza kipato kwa Serikali na watoa huduma pia,” anasema.
Kwa upande wake katibu wa Shirikisho la Vyama vya Utalii (TCT), Richard Rugimbana ili mtalii akae nchini muda mrefu lazima kuwe na vitu vya kumshawishi. “Tanzania kuna takriban makabila 120, bidhaa za utamaduni zikiboreshwa bila shaka idadi ya siku itongezeka. Siku kumi sio mbaya lakini uwiano na idadi ya vivutio haiko sawa,” anasema.
Vilevile, watalii wanaokuja nchini, ripoti inaeleza kuwa wanalalamika kuhusu kutotumika kwa kadi za malipo badala yake fedha tasilimu kupendelewa zaidi. Asilimia 19 walilipa kwa kadi na asilimia 73 wakalipa fedha tasilimu.
Profesa Mkenda anasema wizara inaandaa mfumo mfumo wa kielektroniki kukusanya mapato ili kuondokana na matumizi ya fedha taslimu kwa wageni wanaotembelea mbuga na hifadhi zilizopo.
“Tanapa na Ngorongoro tayari kuna mfumo wa kielektroniki. Tunachofanya hivi sasa ni mkakati wa kuyafikia mapori tengefu pamoja na malikale. Ndani ya wiki moja au mbili za ufungaji tutakuwa tumekamilisha jukumu hilo,” anasema.
Kama yalivyo maeneo mengine, foleni ndefu jijini Dar es Salaam ni kero nyingine ambayo inawasumbua watalii lakini kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la Mfugale lililopo makutano ya Tazara pamoja na flyover inayoendelea kujengwa makutano ya Ubungo yatasaidia kuimaliza.
 Kero nyingine ni muda mrefu unaotumika kushughulikia viza pindi wageni hao wanapofika kwenye viwanja vya ndege vilivyopo nchini.
Profesa Mkenda anasema kukamilika kwa terminal III katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kutasaidia kupunguza usumbufu huo.
“Uwanja uliopo sasa unaelemewa lakini terminal III ikianza kutumika, hali itabadilika sana. Wageni sasa hivi wanaweza kuomba viza mtandaoni au kwenye ofisi zetu za ubalozi,” anasema katibu mkuu huyo.
Ufanisi wa sekta
Kutoka na ongezeko la wageni mwaka 2017, mapato ya sekta ya utalii yalipanda kwa asilimia 5.6 na kufika Dola 2.25 bilioni za Marekani.
Takriban asilimia 85 ya fedha hizo zilitokana na matumizi yaliyofanywa na watalii waliokuja kwa mapumziko huku wale waliowatembelea ndugu zao wakichangia kiasi kidogo.
Ingawa waliowatembelea ndugu na jamaa zao wanatumia kiasi kidogo zaidi lakini ripoti inasema kundi hilo ndilo linalopata taarifa za uhakika kuhusu vivutio vilivyopo nchini likiwa juu ya wale wanaozipata kupitia matangazo ya utalii.

Advertisement