Mbinu kukabiliana na machungu ya ada Januari

Aghalabu miezi ya Desemba na Januari, moja ya mazungumzo yanayoteka hisia za wengi vijiweni, kazini mitandaoni na hata kwenye vyombo vya habari huwa ni kuhusu maumivu ya ada kwa wazazi

Ndicho kipindi ambacho kama katuni zitachorwa magazetini, watu watatumiana ujumbe wa utani katika mitandao. Lakini ukweli unabaki kuwa miezi hii inawatesa wazazi wengi wenye watoto shuleni.

Abby Bakari ana miaka takriban 10 katika ndoa, ana mtoto mmoja anayesoma darasa la nne katika shule moja ya mchepuo wa Kiingereza jijini Dar es Salaam. Hana kipato cha uhakika, kila mwisho wa mwaka unapofika, Bakari hujikuta katika lindi la matatizo kuanzia pango la nyumba, ada na michango mingine shuleni. Aghalabu amekuwa akiponea mikopo anayosema imekuwa ikimsaidia kujinasua na matatizo ya mwisho wa mwaka.

‘’ Nina mikopo mpaka imepandiana kuanzia katika benki hadi kwa watu binafsi. Nalazimika kufanya hivyo kwa sababu nahitaji kumpatia elimu bora mwanangu,’’ anasema.

Si Bakari pekee anayeguswa na machungu ya ada, Jarden Chundu ambaye ni baba wa watoto watatu anasema kama isingekuwa kuendesha mambo yake kwa bajeti, ingekuwa vigumu kwake kusomesha watoto wake shule nzuri.

“Tuache uongo Januari ni mwezi mwiba, usipokuwa makini unaweza kuuza hata vitu vya ndani ili ulipe ada za watoto. Ni mwezi mgumu ikiwa ni baada ya kutoka katika sikukuu mbili mfululizo,” anasema.

Wakati Bakari akiamini dawa ipo katika mikopo, Chundu ambaye ni mfanyabiashara wa kati anaamini katika utengaji wa bajeti kama dawa ya maumivu ya ada.

“Bajeti ndiyo kila kitu; unaangalia nini kifanyike na kwa wakati gani ili kuondoa matumizi yasiyo halali ya fedha. Hata ukiwa unaingiza mamilioni mangapi kama hauna mipango kila kitu kitakuwa ni mzigo kwako,”anaeleza.

Ushauri wa wachumi

Baadhi ya wataalamu wa wachumi wanabainisha kuwa inawezekana kwa mzazi hata aliye na kipato cha kati kumudu gharama za kumsomesha mtoto wake katika shule nzuri bila kuhisi mzigo.

“Kupanga ni kuchagua, unapochagua kuwa nacho utakipata na usipokitaka hautakipata,” anasema Dk Abel Kinyondo ambaye mhadhiri mwandamizi wa uchumi Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Anasema kuna watu walio na vipato vikubwa lakini wanashindwa kufanya vitu vya maendeleo, ukilinganisha na wale walio na kipato kinachooneka kuwa kidogo lakini wanafanya mambo makubwa

“Mara nyingi watu ambao wana malengo ya kufanya vitu tofauti huangalia na kuweka mipango kwa muda mrefu ni nini anataka afanye na anapanga bajeti ambayo itamsaidia katika kutimiza kila kitu bila kuathirika,” anasema Dk Kinyondo

Anasema jambo hilo limewafanya wengi kusomesha watoto wao katika shule nzuri tena kwa vipato vyao vya kawaida kutokana na jambo hilo kuwa ndiyo kipaumbele chao.

“Kila mtu huwa na kipaumbele chake, kuna wengine huweza kukopa na kununua gari, mwingine hukopa na kusomesha mtoto hivyo suala hili haliwezi kumuathiri mtu kama amejipanga” anasema na kuongeza:

“Mara nyingi watu hulia Januari kuwa ngumu inapofika bila kujua kama mipango ya nyuma ingeweza kuweka kila kitu sawa. Huwa wanajisahau kuwa hakuna Januari lakini mipango pekee ndiyo inaweza kuondoa hali hiyo.’’

Wekeza kidogokidogo

Mchumi mwandamizi nchini, Profesa Samwel Wangwe anasema ili kuondokana na mzigo wa kulipa ada ya watoto,wazazi wanatakiwa wajifunze tabia ya kuwekeza kidogo kidogo

“Wekeza kidogo kidogo, unajipanga mapema kabla siku hazijafika, Najua kuna baadhi ya shule unaruhusiwa kulipa kidogo lakini hicho nacho inabidi ukiandae na hata wakati unasherehekea sikukuu za Mwaka mpya na Christimas unaendelea kujipanga kwani kufanya hivyo kutakufanya usihisi mzigo wakati wa kulipa ada,’’ anasema.

Huna haja ya kusubiri hadi mwisho mwa mwaka. Anza kudunduliza ada tangu mwanzo mwa mwaka. Kila kipato unachokipata unaweza kutenga kiasi maalumu kwa ajili ya ada

Jiandae mapema

Elimu ni uwekezaji na kimsingi sio jambo la kukurupuka kama inavyofanyika kwa wazazi wengi.

Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja anasema wazazi hawana haja ya kusubiri hadi ifike Januari ndio waanze kufukuzana na ada. Anasema bado wana fursa ikiwa watajipanga mapema.

Anasema licha ya kuwa mwezi huo huja baada ya kupita kwa sikukuu za Christmas na mwaka mpya, lakini kama kunakuwa na mipango na matumizi ya sasa na baadaye kila kitu huwa rahisi.

‘’Muda wa kulipa ada ukifika kama mzazi anatakiwa awe tayari ameshajiandaa na siyo huo uwe muda wa kuanza kutafuta kiasi cha kuhisi kuwa jambo hilo limekuja kwa kushtukiza,’’ anasema.

Profesa Semboja anazisihi shule pia kuona haja ya kufikiria hali za kimaisha za wazazi…’’ Shule iwe tayari kumvumilia mzazi katika siku ambazo anatafuta fedha huku mtoto wake akiruhusiwa kusoma’’

Unaweza kulipa kidogokidogo

Baadhi ya shule kwa kuzingatia hali halisi ya wazazi, zimeanzisha utaratibu wa malipo ya ada kwa awamu kadhaa ndani yam waka. Lakini pia zipo ambazo wazazi wanaruhusiwa kulipa kiasi chochote na kulipa wakati wowote wanapoweza.

Utaratibu huu umekuwa nafuu kwa Daniel Bonjera anayesema tangu utaratibu huo uanzishwe katika shule wanazosoma watoto wake wawili, maumivu ya ada yamepungua.

‘’ Walituita kikaoni na kutueleza kuwa wanachotaka ni fedha iingie kwenye akaunti yao, haijalishi ni kiwango gani. Mimi naendesha malori mikoani na nchi jirani, nalipwa kwa kamisheni. Ninachokipata mara nyingi ndicho ninachokipeleka hata ikiwa ni chini ya Sh30,000. Nimekuwa nikifanya hivyo na kujihakikisha namaliza ada yao,’’ anasema Bionjera.

Anavyosema dereva bodaboda

Paschal Chacha ni dereva wa bodaboda anayesema malengo yake ni kuhakikisha mtoto wake anasoma katika shule nzuri pamoja na kuendeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi.

“Wakati mwingine tunalalamika watoto wetu hawafanyi vizuri shuleni kwa sababu sisi kama wazazi tumeshindwa kuwekeza ili wapate elimu bora. Ikiwa mtu unayo fedha ya kuwanunulia rafiki zako vilevi au wewe kuvinjari kila mwisho wa wiki unakosa wapi fedha ya kumsomesha mtoto,”anahoji.

Anasema licha ya kuwa shule binafsi kulipisha ada kubwa lakini zipo baadhi zinaruhusu mzazi kulipa kwa awamu, jambo analosema mzazi makini akijipanga anaweza kuondokana na adha ya ada shuleni.

“Kama mzazi hili linaondoa mzigo kwetu na linatupa muda wa kujipanga kwani tunakua tukijua kabisa kila baada ya muda fulani tunatakiwa kulipa ada tofauti na kulipa yote kwa mpigo. Inaumiza na inafanya watu kusahau jukumu lao kwa muda na huweza kukuacha na madeni,” anasema Chacha.