ANTI BETTIE: Kila nikimpata mtu mpya nashindwa kuwajibika, tatizo nini?

Anti habari! Sijui niseme nini jinsi ninavyovurugwa na hali ya jogoo wangu. Imekuwa kawaida nikipata mpenzi mpya agome kuwika siku ya kwanza tukikutana na ya pili, huko baadaye ndiyo anazoea.

Nifanyeje, maana kuna ambao wananikimbia kwa sababu hiyo?

Ungekuwa unazungumza ningekuambia sikiliza maneno yako, lakini kwa hiki ulichokiandika kisome tena kwa sauti na usikilize unazungumza nini? Ina maana una mwanamke zaidi ya mmoja na unazidi kusajili wengine kila siku. Jogoo hakupi ushirikiano unamchosha kila siku kukutana na watu wapya, kama ulipata mwanamke akagoma kuwika baadaye akazoea na kuendelea kwa nini usitulie na huyo, haya hao wengine ukishawapata zaidi ya faragha huwa unapata nini?.

Aibu unazitaka kwa kuhangaika, ungetulia na mwanamke mmoja usingekuwa unaaibika. Kuhusu tatizo lako la msingi la jogoo kushindwa kuwika, ninashindwa kuwa na jibu la moja kwa moja, kwani sifahamu hali hiyo ilianzaje.

Ila wataalamu wa afya wanashauri mambo kadhaa ikiwamo kupunguza unywaji wa pombe, uvutaji sigara, msongo wa mawazo.

Ninachokushauri kwa sababu imekutokea mara kadhaa ni rahisi kurudia tena, hivyo onana na washauri nasaha walio karibu nawe ili kukuondolea hofu, ninahisi huwa unapatwa na hofu ukipata mwanamke mpya kama ambavyo umetangulia kujieleza.

Nimekuwa mtumwa kwa machejo yake

Nimeoa huu mwaka wa sita, sijawahi kumzoea mke wangu, kila siku ananifanyia jambo jipya tukiwa faragha. Tatizo lake siyo mwaminifu katika ndoa yetu anachepuka kadri anavyoweza na mimi ninashindwa kumuacha kwa sababu ananipa kabla sijamuomba na ananijulia.

Nifanyeje?

Kwanza nafurahi kusikia kuwa mwenza wako anakupa unachotaka tena kabla hujaomba. Turudi katika mada husika, inakuwaje unakuwa mtumwa wa penzi na kuacha kuangalia mambo ya msingi ya maisha yenu?

Hivi akikuua na maradhi anayoyatafuta kwa nguvu kutakuwa na faida gani ya hayo machejo, maana hutayaona tena.

Unakubali vipi mwanaume kudhalilishwa kwa kuwa na mwanamke asiyekuwa mwaminifu katika ndoa kwa sababu hilo ndilo jambo la msingi na la kwanza kuzingatiwa na wenza, unaweza kuvumilia mambo yote, lakini siyo hilo.

Mweleze ukweli kuwa pamoja na kukufikisha na kukupa burudani inayokata kiu yake, unafikiria kuachana naye kwa sababu ya kutokuwa mwaminifu, ukishindwa washirikishe ndugu wa pande zote mbili ili mlitatue jambo hilo.

Lakini hakikisha una ushahidi wa kutosha na siyo kusikia sikia au kuhisi, kwa sababu unachokifanya ni kunusuru ndoa yako na si vinginevyo, hivyo ukiita watu kuja kuwasikiliza uwe na la maana la kuwaeleza. Ukifanya hivyo anaweza kuacha, lakini ukilalamika lalamika kwa kusikia sikia ataona kawaida na ataendelea na tabia zake. Ila jambo la muhimu, jiulize kwa namna mnavyoishi anakupenda kweli au anakupa huduma ya mwili ili akuburuze anavyotaka? Ukipata jibu kuwa anakupenda endelea na juhudi za kunusuru ndoa yako, lakini ukiona anatumia ujuzi wake faragha kama pombe ya kukulevya ili afanye ufuska wake jifikirie mara mbili...Acha kuwa mtumwa wa penzi.