Mchumba wangu yupo masomoni, nimenasa kwenye penzi la hawara

Sunday December 15 2019

 

Mchumba wangu baada ya kwenda chuo mbali nami nimejikuta nikiingia kwenye penzi la mwanamke mwingine.

Nifanyeje ili nijinasue kwa sababu mchumba wangu ameanza kuhisi na anakaribia kurudi. Hakika ninawapenda wote.

Uliyoyaandika hapa yaseme kwa nguvu na ujisikilize yanavyovuma masikioni mwako kama upo sahihi au unahitaji ushauri nasaha.

Mchumba wako amekwenda kusoma tu, ingawa hujasema kwa muda gani lakini ushapata mwingine, ikitokea akaumwa muda mrefu si utakuwa na wapenzi kiboa. Kuitwa binadamu kunajumuisha kujitambua, kujithamini na kupima mambo, ndiyo maana wanyama hawavai nguo, hawaogi na hufanya hadharani ya faragha. Iweje wewe umepewa akili na upo kwenye kundi la wanaojitambua yaani binadamu na unafanya vitu unavyojua vitamuumiza mtu unayemuita mchumba.

Vaa viatu vyake, yaani wewe uwe masomoni halafu azame kwenye mapenzi na mwanaume mwingine, utajisikiaje? Umeniudhi na uchumba wako na huyo msomi unanifikirisha, jitafakari mara mbili kama upo tayari kuwa mume au unailaghai akili yako. Kama hujamaliza ujana na hujakubali kuwa mambo yasiyo na staha yana wakati wake, mwambie binti wa watu atafute atakayemfaa. Usimpotezee muda akaambulia maumivu na kilio. Kumbuka penzi haligawanyiki, huwezi kuwapenda wote lazima utaelemea kwa mmoja na kusababisha ugomvi au uchumba wenu kuvunjika.

Hee! Mambo ya mpenzi wangu ni makubwa

Advertisement

Nimekuwa katika mahusiano na kijana kwa miaka mitatu, lakini hivi karibuni nikiwa likizo kwa mjomba wangu akanitambulisha watoto wake waliokuwepo na wengine kupitia picha cha kushangaza mmoja ni huyo mpenzi wangu.

Kibaya zaidi baada ya utambulisho mama akaanza kulalamikia tabia za mtoto wa kaka yake kutembea na kina mama watu wazima.

Nifanyeje na tunapendana?

Kuhusu kuwa ndugu yako kwa baadhi ya makabila isingekuwa shida kwani mnaitana binamu. Makabila au imani nyingine binamu si ndugu wa damu hapo kila mmoja ana ukoo wake, hilo lingezungumzika kama mnapendana ingawa kuna baadhi ya familia kwao ndugu ni ndugu hakuna binamu kinyama cha hamu. Jipange kuuelekeza moyo wako cha kufanya kuhusu huyo mpenzi wako kwa kuwa hamjafika mbali kwa maana ya kupeana mimba au kuzaa, nakushauri jiondoe taratibu.

Huo uhusiano usio rasmi hauna mwendelezo, mtaishia kuwa wapenzi tu, huwezi kufanya naye maisha kwani ni ndugu yako na ana tabia alizosema mama yako. Simaanishi upangiwe wa kuwa naye, ila kwa huyu unayemuita mpenzi, vikwazo vimekuwa vingi tena vinavyoweza kuigusa familia moja kwa moja.

Ingekuwa siyo ndugu yako ingekuambia ujipe muda kujiridhisha kuhusu tuhuma alizozitoa mama yako, lakini ni ndugu yako.

Pili unakujaje kwangu kuulizia mambo ya mpenzi? Tumechoka kusikia vilio vyenu kila siku mkiachwa, tafuta mtu mwenye nia ya kuwa na wewe kwa kukuchumbia angalau unakuwa na uhakika.

Advertisement