TUONGEE KIUME: Shoga wa mkeo akitaka kuharibu ndoa, fanya hivi

Monday December 9 2019

 

By Kelvin Kagambo

Mwanaume mwenzetu, sitomtaja jina alioa mwanamke mzuri sana, na kwa upendo wa Mungu na upendo wao binafsi wamedumu kwenye ndoa kwa miaka mitano sasa. Katika hii miaka mitano wamepata watoto wawili, gari moja dogo na nyumba ambayo walihamia kabla haijamalizika vizuri.

Kifupi wao si maskini, wala hawana shida sana, lakini ukiwalinganisha na maeneo waliyohamia kidogo wanakuwa chini. Watu wa kule wengi ni vigogo, wenye pesa. Mfano hata nyumba yao ni nzuri, lakini kwa vile haijamalizika vizuri inaonekana kama gofu ukilinganisha na majumba mengine ya huko. Sasa huku wakapata majirani lakini mke akapata majirani na mashoga, tuache upande huu, tutarudi baadaye.

Sasa huyu mwenzetu, mara akaanza kuona mke wake anabadilika ghafla. Akawa na katabia ka kupondea kila kitu ndani ya nyumba utasema hawakutengeneza pamoja, aliolewa akavikuta. Tena si kulalamika tu, analalamika kwa njia ya kufanisha na vitu vingine nje. Akilalamika kuhusu kigari chao, hatosema gari tu, atasema kigari hiki kidogo, unajua tukiongeza mtu mmoja tu kwenye familia hakitotosha tena hata kuendea kanisani. Tukiuze tuongezee pesa tununue gari yenye nafasi kidogo tena tukiongea vizuri na Sarah atatupeleka kwa mtu wake, tutapata gari yenye nafasi kama ile yake kwa bei rahisi.

Sarah ni yule jirani na shoga yake niliyekwambia mwanzo.

Akilalamika kuhusu kuboresha nyumba hatosema nyumba tu, atasema fenicha zimeisha sana hizi mume wangu hata akija mgeni aibu kumkaribisha sebuleni. Mwisho wa mwezi tukope pesa tununue zingine, tena tukiongea na Sarah anatupeleka kwa mtu wake atatuuzia kama zile za kwake kwa bei nyepesi sana.

Sasa mwenzetu hii kitu inamkwaza sana na akaileta kwenye baraza akiuliza afanyeje. Na hii ndiyo siku niliyosikia ushauri bora zaidi uliowahi kutolewa kwa msukumo wa pombe.

Advertisement

Jamaa yetu mmoja akamwambia mkeo amekuwa na tamaa kwa sababu ya mtu anayekuwa karibu naye siku hizi. Kwa hiyo hapa sumu ni vitu viwili, tamaa mpya ya mkeo na kubwa zaidi ni huyo Sarah. Hivyo kupunguza tamaa ya mkeo unahitaji kumpunguza anayeichochea hiyo tamaa.

Sasa wanawake ukiwaambia moja kwa moja kwamba sitaki uwe na ukaribu na Sarah, itakuwa mada nyingine na itaibua makorokoro mapya na utaharibu vitu, hivyo hapo unatakiwa utumie akili.

Akili ni hakikisha ukirudi nyumbani unasifia maumbile ya Sarah, ila si kwa namna ya kuyatamani, bali kwa kuonyesha tu kwamba huna chuki hata chembe na mwanamke huyo na ungependa awe shoga wa mke wako mpaka mwisho wa dunia.

Mwambie mke wangu, unajua Sarah ni mwanamke mzuri sana, akitabasamu, anatabasamu vizuri sana, na wanaume tunapenda wanawake wanaotabasamu, ni kama wewe mke wangu. Atakayemuoa Sarah atakuwa amepata mke.

Rudia sifa za namna hii angalau kwa wiki mara tatu kila akianzisha stori zinazomhusisha Sarah. Nakwambia hutomaliza wiki mbili, hutosikia tena stori za Sarah wala kumuona anakanyaga nyumbani kwako.

‘Kadhalika nyinyi wanaume, kaeni na wake zenu kwa akili’ Biblia

Advertisement