Mbolea za viwandani nzuri kutumia, lakini…

Saturday May 4 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Mbolea ni chakula cha mimea, ambacho ni mchanganyiko wa virutubisho mbalimbali vinavyoongezwa kwenye udongo au vinavyowekwa moja kwa moja kwenye mimea, ili kuongeza ukuaji na uzalishaji wa mimea.

Virutubisho hivyo ni pamoja na madini muhimu yanayohitajika na mmea kwa kiasi kikubwa kama vile naitrojeni, fosiforasi na potashi.

Haya yanahitajika kwa kiasi kikubwa na ndio mana kila mbolea inayotengenezwa kiwandani huwekwa madini haya muhimu matatu.

Madini mengine muhimu ni salfa, chokaa, magneziam, boroni, shaba. Zinki, molybedenum, chuma na mengineyo.

Mbolea za viwandani

Hizi ni mbolea zinazotengenezwa kiwandani kisasa na kuwekewa kiwango maalumu cha virutubisho muhimu katika ukuaji bora na uzalishaji bora wa mmea.

Advertisement

Mfano wa mbolea hizi ni kama CAN, Urea, DAP na nyinginezo.

Ikumbukwe mmea unahitaji virutubisho 16 lakini kuna vinavyohitajika kwa kiasi kikubwa na vingine kwa kiwango cha kawaida.

Mmea unaweza kushindwa kukua vizuri kwa kudumaa, kuwa na rangi ya njano au ukashindwa kuzalisha vizuri kwa kukosa virutubisho vinavyohitajika kwa kiasi kikubwa kwa ukuaji wa mmea.

Virutubisho hivyo muhimu ni Naitrojeni, Fosiforasi na Potashi. Kila mbolea ya dukani ambayo itatengenezwa huwekwa virutubisho hivi vikuu vitatu kwa uwiano tofauti kutokana na mahitaji ya mmea.

Kwa mfano, kuna mbolea zenye naitrojeni kwa wingi kama vile CAN (27:0:0). Uwiano huo una maana kuwa Naitrojeni (27), Fosiforasi (0) na Potash (0).

Hivyo, mkulima ajiulize anapoweka naitrojeni kwa wingi, anajua kazi yake kwa mmea? Naitrojeni ndiyo inayotengeneza kijani kibichi katika mmea.

Mfano wa pili ni mbolea ya DAP; hii ina fosiforasi kwa wingi (18:46:0). Uwiano huo una maana kuwa Naitrojen (18), fosiforasi (46) na Potasiam (0).

Wakulima wanashauriwa watumie DAP kupandia kwani mmea kwa maisha ya mwanzo kabisa unahitaji fosiforasi kwa wingi. Hii ni faida moja kubwa kwa mbolea za viwandani dhidi ya mbolea za asili.

Mkulima anayetumia mbolea asili, hawezi jua kiwango cha naitrojeni wala potash anachoweka kwenye mmea wake.

Faida za mbolea za kemikali

1.Hufanya kazi kwa haraka, Ni rahisi mno kuokoa mmea unaokaribia kufa kutokana na ukosefu wa virutubisho.

Hii ni kwa sababu virutubisho vilivyopo katika mbolea za kemikali huwa rahisi kufyonzwa na mmea mara moja baada ya mbolea hii kuwekwa kwenye mmea. Mara nyingi huwa katika hali ya chenga chenga hivyo mkulima akishamwagilia maji mmea wake kisha akaiweka umbali wa sentimita 4 kuzunguka mmea huyeyushwa na kufyonzwa na mmea moja kwa moja.

2. Upatikanaji rahisi: mbolea hii ni rahisi kupatikana katika maduka ya pembejeo na maeneo mengine..

3. Hutumika kidogo tu: Kwa ekari moja kwa mfano wakati wa kupandia mfuko mmoja wa kilo 50 unaweza kutosha kwa baadhi ya mazao kwa kuwa uwekaji wake ni gramu tano kwa shimo.

Lakini kwa mmea unaokaribia kutoa maua mpaka mifuko miwili ya kilo 50 inaweza kutumika kwani hapa mkulima atahitajika kuweka gramu 10 kuzunguka mmea.

4. Ina virutubisho muhimu vinavyohitajika katika mmea na mkulima hutambua ameweka kiasi gani. Mkulima hujua anaweka naitrojeni kiasi gani, fosiforasi kiasi gani na potashi kiasi gani. Mkulima anayetumia mbolea za asili hawezi kujua kaweka virutubisho kiasi gani kwenye udongo wake.

Hasara za mbolea za kemikali

1. Gharama kubwa: Mfuko mmoja wa mbolea za kemikali wenye kilo 50 unauzwa siyo chini ya Sh 50,000. Kwa wakulima wengi wadogo, huu ni mzigo mzito kidogo kuubeba.

2. Kuondolewa virutubisho kwa urahisi: Kwa kuwa kuwa virutubisho vyake huwa karibu, mkulima anapaswa kuwa makini kwani maji yakiwa mengi yanaweza kusababisha upotezwaji wa virutubisho hivyo muhimu.

3. Huathiri udongo na mmea: Matumizi ya mbolea za kemikali kwa muda mrefu huongeza chumvi ambayo baadaye huathiri udongo na uzalishaji hupungua kutoka katika udongo husika na kuua kabisa rutuba ya udongo.

Lakini pia hata katika mmea husika mkulima akizidisha kiwango zaidi ya alichoelezwa, ataunguza mizizi ya mmea na kuusababishia kufa.

4. Inahitaji elimu katika matumizi: mkulima anahitaji kujua vipimo maalumu katika matumizi.

5. Athari kwa afya, mbolea hizi zinahitaji umakini maana zinaweza kuleta madhara katika ngozi na mfumo wa upumuaji kwa ujumla kwa mkulima kama asipokuwa makini na matumizi yake.

6. Huondoa wadudu muhimu katika ukuaji wa mmea. Wote tunajua kuwa mfumo wa udongo unahusisha wadudu wanaoishi udongoni ambao pia huboresha muundo wa udongo, kuvunja vunja mabaki ya wanyama na mmea, na kuupa kinga mmea na magonjwa na wadudu.

Uwekaji mbolea ya dukani kwa muda mrefu husababisha kuongeza asidi ( ph) ya udongo na kuua mfumo asili wa udongo ambao hautokuwa rafiki kwa wadudu muhimu kwa mmea hivyo wadudu hawa huondoka. Hii itasababisha mmea kuathirika katika ukuaji wake na mazao kupungua.

Wito

Mbolea hii ni nzuri kama itatumiwa na mkulima kwa muda mfupi na siyo kutumia kwa muda mrefu, kwani ina athari kwenye rutuba ya udongo.

Advertisement