ONGEA KILIMO : Anguko la mazao ya biashara liwe somo kwa wadau

Saturday May 18 2019Elias Msuya

Elias Msuya 

By Elias Msuya

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umasikini (Repoa) umeonyesha kushuka kwa sekta ya kilimo hasa katika eneo la masoko.
Utafiti huo uliozinduliwa kwa mfumo wa vitabu vinne, umetaja sababu kadha wa kadha kuhusu anguko hilo, lakini kwa ufupi tu, utafiti uliofanywa na Dk Donald Mmari umeonyesha kudorora kwa kilimo tangu wakati Tanzania inapata uhuru mwaka 1961 hadi mwaka 2015.
Katika utafiti huo imeonekana kumekuwa na anguko la mauzo ya nje ya mazao ya kilimo kwa kipindi chote hicho. Mazao ya kimkakati ni pamoja na pamba, chai, kahawa, korosho, katani na tumbaku.
Wakati mazao hayo yakidaiwa kushuka kwa mujibu wa utafiti huo, utafiti huo pia umebaini kuwepo kwa ongezeko la gharama za bidhaa kutoka nje ya nchi. Hii maana yake ni kwamba, kama hatuzalishi mazao ya kutosha kuuza nje, tutakuwa tunategemea bidhaa zilizotengenezwa na viwanja vya nje kwa ajili ya matumizi yetu.
Afadhali kama hayo mazao yasingeuzika nje yakabaki kwenye viwanda vya ndani, lakini hata hivyo viwanda vyenyewe havitoshelezi kuweza kusindika bidhaa hizo kwa wingi.
Tukumbuke kuwa mazao haya ya kimkakati pamoja na mazao ya chakula, yote yanazalishwa na wakulima wadogo, kwa hiyo anguko lake linawagusa wakulima moja kwa moja.
Kwa mfano, tumeona mauzo ya korosho kwa msimu uliopita. Mvutano uliokuwepo kati ya wafanyabiashara na wakulima na baadaye Serikali kuingilia soko hilo, ndiyo mambo yamefika hapo yalipofika.
Licha ya Serikali kujipa jukumu la kununua korosho zote kutoka kwa wakulima, bado kuna wakulima wanaolalamika kutokamilishiwa malipo yao, wakati ambao wanajiandaa na msimu mpya.

Dk Blandina Kilama aliyeshiriki katika utafiti huo, ameshauri katika andiko lake kuwaacha huru wakulima kujitafutia masoko ya mazao yao kama ilivyo kwa nchi ya Vietnam.
Huo ndio utaratibu uliokuwepo ambapo wakulima walikuwa wakiuza korosho zao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo wanunuzi walishindana kupitia minada.
Ni kweli Serikali inatakiwa kudhibiti masoko, lakini haikupaswa kuingilia kila kitu. Kwa kuwa kilimo ni biashara, nguvu ya soko ndiyo inayoshindana, si nguvu ya dola.

Advertisement