Uchaguzi wa serikali za mitaa ukitazamwa na jicho tofauti

Wednesday November 20 2019

 

By Daniel Mjema, Mwananchi

Vyama saba vya upinzani vimesusia uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa wa Novemba 24 na hakuna dalili kwamba vinaweza kurejea. Swali linalojitokeza ni je, matokeo ya uchaguzi huo yatakuwa na maana gani kisiasa, swali ambalo linajibiwa kwa mtazamo tofauti.

Ni wazi CCM itaibuka na ushindi pengine wa zaidi ya asilimia 99 kwa vile tayari imepita bila kupingwa katika maeneo mengi, lakini hoja hapa ni kwamba ushindi huo utakuwa na maana gani?

Ni uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi ambao unakwenda kufanyika huku CCM ikiwa kama imeshashinda baada ya asilimia 90 ya wagombea wa upinzani kuenguliwa.

Ni hali inayovutia mjadala mpana. Msomi wa sayansi ya siasa ambaye sasa ni balozi, Dk Benson Bana anasema vyama vya upinzani havikuwekeza katika mitaa na ndiyo maana vinajiondoa.

“Sasa unaingia na mtaji gani? Tukipitapita kwenye vijiji huko wala hatuoni alama za vyama vya upinzani. Hawajafanya kazi ya siasa. Walijua wanaingia kwenye uchaguzi lakini hawajawekeza...Kama hujawekeza, kiherehere cha nini kuingia kwenye uchaguzi. Kwa hiyo utatafuta nafasi uweze kujiondoa,” anasema.

Wajkati Dk Bana anautazama kwa jicho hilo, mwanasiasa mzoefu wa siasa za Zanzibar, Ismail Jussa ana jicho tofauti, anasema ikiwa uchaguzi huo utafanyika kama ulivyo sasa, utakosa uhalali wa kisiasa ingawa utakuwa halali kisheria.

Advertisement

Mambo yalivyoanza

Mchakato wa uchaguzi huu ulianza kuingia mushkeli baada ya idadi ya wapiga kura waliojitokeza kujiandikisha katika daftari la mkazi kuwa ndogo hadi Serikali ikaamua kuongeza siku tatu za uandikishaji.

Kutokana na kusuasua huko, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman akalazimika kuishtaki mikoa ambayo ilikuwa imeonekana kufanya vibaya ukiwamo mkoa wa Dar es Salaam ambao hadi Oktoba 12, ulikuwa umeandikisha asilimia nane tu ya malengo, Kilimanjaro asilimia 12 na Arusha asilimia 13.

Baada ya Jafo kuongeza siku tatu za ziada za uandikishaji ndio idadi ya waliojiandikisja ikafikia milioni 19.6.

Uchaguzi uliingia nongwa zaidi wakati wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu pale baadhi ya ofisi za wasimamizi wasaidizi zilipofungwa na kusababisha ama wagombea wakashindwa kuchukua au kurejesha fomu.

Lakini kubwa zaidi ambalo pengine linaweza kuingia katika kitabu cha maajabu cha Guiness, ni pale asilimia 90 ya wagombea wa upinzani walivyoenguliwa hata walipoamua kupinga kwa rufaa.

Baadhi waliambiwa hawajui kusoma na kuandika licha ya kwamba ni wahitimu wa vyuo, wengine wakaambiwa walikosea kuandika majina yao au ya vyama vyao na wengine tarehe ya kuzaliwa na hata umri wao.

Ni kutokana na dosari hizo na nyingine nyingi, vyama vya siasa vya upinzani vipatavyo saba, vikaamua kutoshiriki uchaguzi huo na kueleza kuwa vimewaondolea udhamini wagombea wake.

Hali hiyo imetokea katika mwaka ambao baadhi ya vyama vya upinzani vinajigamba kwamba vilikuwa vimejiandaa vizuri kuwafikia wananchi na kusimamisha wagombea katika sehemu kubwa nchini.

Mathalan, Chadema inasema ilikuwa imeweka wagombea kwa asimia 85 nchi nzima, idadi ambayo haijawahi kuifikia tangu ianze kushiriki uchaguzi, lakini kati yao zaidi ya asilimia 60 walienguliwa.

Pamoja na kuwaondolea udhamini wagombea waliosalia huku wasomi na wachambuzi wengine wa hali ya kisiasa wakishauri yawepo maridhiano, Tamisemi imesisitiza uchaguzi uko palepale na kwa namna ileile.

Ukitizama mijadala katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, inaonekana uchaguzi huu umewagawa Watanzania katika makundi mawili, jambo ambalo linaweza lisiwe na afya huko mbeleni.

Mathalan, viongozi wa dini ambao walidiriki kuhamasisha waumini wao wajitokeze kupiga kura, wameshambuliwa vikali kwenye mitandao ya kijamii na wachangiaji wengine hata wakiwatukana.

Ukiziangalia sababu kubwa za kususia uchaguzi duniani zinazotajwa na wanazuoni, zinashabihiana na zinazotajwa na wapinzani katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa.

Miongoni mwazo ni pale mtu anapoona mfumo mzima wa uchaguzi unapendelea wagombea fulani na pale chombo kinachoandaa kinaponekana kukosa uhalali kisiasa na pale wanapohisi kutakuwa na udanganyifu katika uchaguzi huskka.

Ipo sababu nyingine ambayo ni pale kama wagombea hawana umaarufu au hawajulikani, lakini sababu hii haiingii katika hatua tuliyokuwa tumefikia katika mchakato wa uchaguzi tulionao ambao wagombea wote wanatoka mitaani au vijijini wanakojulikana vizuri.

Lakini nje ya hoja hizo, hata mawazo ya Jusa na Dk bana yanadhihirisha pande mbili zinazotofautiana kuhusu uchaguzi huo.

Kauli za Jussa, Dk Bana

Jussa anasema pale inapotokea uchaguzi wa viongozi wa kisiasa unalazimishwa au unakuwa si huru unakosa uhalali kisiasa.

“Ukiangalia uhalali wa kisheria unaweza kusema (uchaguzi wa Serikali za Mitaa) ni halali kwa hoja kwamba sheria, hata kama ni mbovu, maadamu ipo utaelezwa kama ni halali,” anasema Jussa, msomi wa shahada ya sheria, chuo kikuu cha Hull nchini Uingereza.

“Ni kama sheria ile ya Afrika Kusini iliyokuwa inahalalisha ubaguzi wa rangi. Kule walipitisha sheria ikawa kwamba ni jambo la kisheria kubagua watu.

“Kwa msingi huohuo ukiendesha uchaguzi ambao si huru na wa haki utakosa uhalali kisiasa, utakuwa si halali kimaadili lakini wenyewe watakuambia ni halali kwa sababu umefuata sheria.

Ananukuu Katiba ya Tanzania Ibara ya 8 inayotamka kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa ni nchi ya kidemokrasia na yenye kuzingatia haki za kijamii...

“Ibara ya 8(1) (a) inasema kwamba nchi itaongozwa kwa kuzingatia kwamba wananchi ndio msingi wa madaraka ya serikali na vyombo vyote vya serikali vitapata mamlaka kwa wananchi..

“Sasa kwa msingi huo inategemewa kuwa yeyote anayetawala, awe mwenyekiti wa Serikali ya kijiji, kitongoji au mtaa bila ridhaa ya wanaoongozwa, hawezi kupata uhalali wa kisiasa na uhalali kikatiba,” anasema.

Kwa upande wake Dk Bana anasema kila mtu angependa uchaguzi ambao ni huru na haki na uchaguzi ni kielelezo kikubwa katika jamii inayozingatia utawala bora.

“Katika uchaguzi wowote lazima sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza uchaguzi huu ziwe mwafaka kwa watu wote wanaoshiriki kwa maana ya vyama vya siasa, wapiga kura na wagombea,” anasema.

Hata hivyo, anavishangaa vyama vilivyojitoa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wakilalamikia ukiukwaji wa kanuni ambazo anasema walishiriki kuzitunga na kuziridhia.

“Nadhani kulikuwa na muafaka. Ambaye hakuwa na mwafaka hakutwambia, lakini ukweli hakuna kanuni, sheria au taratibu ambayo itamridhisha kila mtu, lakini yale ya msingi walikubaliana.

Pamoja na maoni hayo, vyama vya upinzani vililalamika tangu kanuni zinatungwa, vikisema vilishiriki hatua ya kwanza na kutoa mapendekezo ya awali, kisha wakakubaliana kuwa na kikao cha pili cha kuona hatua iliyofikiwa ambazo hata hivyo hakikufanyika, badala yake walishtukia kanuni zinazinduliwa.

Balozi huyo anayesubiri kupangiwa kituo cha kuhudumu anaongeza, “Najiuliza uchaguzi uliopita (2014) hivi vyama vilikuwa na mitaa kweli? Hivi vyama vina serikali za vijiji kweli? Waliwekeza kiasi gani ili ule ushindi walioupata uweze kudumishwa?” anahoji Dk Bana.

“Nikiangalia vyama vile kwa sababu asilimia karibu 96 ya mitaa, vitongoji na vijiji iko mikononi mwa CCM. Kwa hiyo wanaingia katika uchaguzi huu CCM ina mtaji wa asilimia 96,” anasema.

“Sasa unaingia na mtaji gani? Halafu tukipitapita kwenye vijiji huko wala hatuoni alama za vyama vya upinzani. Hawajafanya kazi ya siasa. Walijua wanaingia kwenye uchaguzi lakini hawajawekeza.

“Kama hujawekeza kiherehere cha nini kuingia kwenye uchaguzi. Kwa hiyo utatafuta nafasi uweze kujiondoa.

“Katika mazingira ya namna hiyo mimi sishangai vyama kujitoa kwa sababu havikuwezeka. Kwa hiyo ili wasiaibike kupata mitaa kidogo zaidi, wameamua kuchukua hatua hii ya kujitoa,” anasema.

Anaongeza, “Sababu nyingine ni kwamba hizi chaguzi za Serikali za Mitaa hazina uhusiano na ruzuku. Kungekuwa na ruzuku ya chama, hivi vyama visingejitoa,” anasema Dk Bana.

“Ukijitoa katika ngazi ya kitaifa unawaumiza wanachama wako, unawaumiza wapenzi wako kwa kuwaamulia, ni udikteta wa namna fulani. Tusiruhusu hali hiyo.

“Chama si chako usiwanyime fursa hiyo. Usiposhiriki uchaguzi utaingia 2020 utakuwa huna mtaji. Nadhani hawakushauriwa vizuri. Wangekuja kwetu tuwashauri. Hawakupata ushauri mzuri”.

Pamoja na maoni hayo, ukweli unabaki palepale kwamba uchaguzi unaokwenda kufanyika bila kushirikisha vyama vingine, hasa vile vikubwa, utakuwa umelalia upande mmoja, hali ambayo si vizuri kuiendekeza.

Advertisement