Wanawake walio kwenye ndoa hatarini maambukizi VVU

Muktasari:

Wataalamu na wanaharakati wenye ujuzi wa ziada wa mambo ya Ukimwi Afrika Mashariki wamesema wanawake walio katika ndoa wapo hatarini zaidi kuambukizwa Virusi vya Ukimwi (VVU).

Rwanda. Wataalamu na wanaharakati wenye ujuzi wa ziada wa mambo ya Ukimwi Afrika Mashariki wamesema wanawake walio katika ndoa wapo hatarini zaidi kuambukizwa Virusi vya Ukimwi (VVU).

Akizungumza leo Desemba Mosi, 2019 katika kongamano la kisayansi lililowakutanisha wanasayansi, vijana na wajuzi hao kutoka nchi za Afrika, mratibu wa programu  ya VVU wa nchini Kenya, Dk Maureen Akolo amesema wanawake walioolewa wanapata virusi zaidi ikilinganishwa na makundi mengine ya wanawake.

Amesema makundi yaliyo katika hatari yamefikiwa na kupewa dawa kinga na njia nyingine za kujikinga, kwamba ni vigumu kupata maambukizi.

“Wanawake walio katika hatari hasa wanaofanya biashara ya ngono waliopata mafunzo kiwango cha virusi kinaenda chini.”

“Lakini ukiangalia wanawake walioolewa mara nyingi wanapata VVU kwa sababu hawana nguvu ya kuzungumza na wenza wao kuhusu kupima au kama wanaweza kumeza dawa kinga au kutimia kondomu,” amesema Dk Akolo.

Dk Okolo amesema mafunzo yatolewe kwa wote pasipo kuangalia makundi hatari kwa maelezo kuwa mambo mengi yamebadilika.

Amewataka wanaume kutotumia majibu ya wake zao na kujiamini kuwa wapo salama.

Dk Okolo amesema kwa sasa asilimia 60 ya wanawake wanaojiuza wana maambukizi ya VVU katika nchi za Kenya, Tanzania na Uganda.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema wasichana chini ya miaka 18 barani Afrika wanaendelea kuwa katika hatari ya kuambukizwa ya VVU.