BARAZA LA SALIM: Wazee ni hazina ya Taifa wanaoihitaji kutunzwa

Katika orodha ndefu ya mambo mazuri ya mila na utamaduni ambayo jamii ya watu wa Zanzibar ilikuwa inarithi ni kuheshimu na kuwasaidia wazee.

Kwa muda mrefu ilikuwa kawaida kila jambo katika familia au jamii huwa halifanyiki bila ya kupata ushauri, nasaha na baraka za wazee.

Hata serikali iliendesha shughuli zake kwa kusikiliza mawazo ya hekima na maarifa ya wazee, wakiwamo watumishi waliostaafu.

Huu ni utamaduni wa kujivunia na katika kuendeleza mwendo huu mzuri mara baada ya mapinduzi ya 1964, serikali iliyoongozwa na Rais Abeid Amani Karume ilionyesha mfano mzuri wa kuwaenzi na kuwatunza wazee.

Miongoni mwa hatua ilizochukua serikali ni kuwajengea wazee makazi Unguja na Pemba na kuwapatia huduma muhimu za maisha.

Rais wa awamu ya saba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein miaka mitatu iliyopita alianzisha mpango wa kuwapatia wazee posho ya kila mwezi kwa kuanzia na kiwango cha Sh20,000 kwa mwezi.

Hivi sasa wanapatiwa Sh70,000 kila mwezi na malipo ya pensheni ya watumishi wa serikali wastaafu yameongezwa kidogo.

Hatua hizi inafaa kupongezwa na inafaa kuweka bayana kwamba hakuna serikali kusini ya jangwa la Sahara inayowalipa wazee kama inavyofanyika Zanzibar.

Unaweza kusema kutokana na hali ya maisha ilivyo hivi sasa, kiwango hiki hakikidhi mahitaji, lakini hapana ubishi kwamba angalau fedha hizi zinasaidia kuwapunguzia wazee matatizo waliyonayo.

Lakini kinachosikitisha ni kusikia taarifa za hapa na pale kuwa katika jamii ya watu wa Zanzibar wapo vijana wanaowanyanyapaa na kutoonyesha utu na heshima kwa wazee, kama vile wao watabaki na ujana wao milele.

Taarifa zilisikika karibuni za wazee kufanyiwa vitendo vya ukatili wakati wa kongamano la kupinga ukatili wanaofanyiwa wazee zinasikitisha na kutisha.

Hali iliyoelezwa na washiriki mbalimbali inakufanya ujiulize watu wa Visiwani waliosifika kwa miaka mingi kwa kuheshimu wazee na kuwatendea wema wanaelekea wapi?

Hili ni suala ambalo kila Mzanzibari anapaswa kujiuliza na kuchukua hatua za kuirekebisha hali hii kabla haijafikia pabaya.

Kwanza ni muhimu kwa kila Mzanzibari kuelewa suala la kila mtu kumtunza na kumsaidia mzee wake ni wajibu na halina mbadala, kama huyo mzee na kutunza wakati akiwa mdogo na sasa.

Katika maisha kinachotakiwa ni kwa mzee kumlea mtoto wake na hatimaye mtoto anapokuwa mkubwa naye kuwa zamu yake kumtunza mzee wake.

Kinachoweza kufanywa na serikali ni kuchangia kusaidia wazee kwa kutilia maanani na kuheshimu mchango walioutoa katika jamii na nchi zama za ujana wao.

Si haki hata kidogo kwa jamii kudhani kwamba kazi ya kutunza wazee ni ya serikali. Kinachofanywa na SMZ ni kuisaidia kuwapunguzia wazee matatizo, lakini bado jukumu la kuwatunza linabaki la watoto na wana wa familia zao.

Wazanzibari wanapaswa kutafakari kwa makini urithi uliotukuka wa kuheshimu na kuwatunza wazee walioachiwa na waliowatangulia.

Kuupoteza au kutouthamini urithi huu ni kosa kubwa ambalo jamii italijutia. Ni aibu, fedheha na dhambi kwa mtu kutomjali, kumdharau au kumnyanyapaa mzee wake au wa mwenzake na hii haikubaliki kidunia wala kidini kama ilivyo kwa mzazi kutomtunza na kumpa malezi mazuri mwanawe.

Kwa upande mwingine nadhani wakati umefika wa kuwa na sheria kali zitakazosaidia kudhibiti ukatili wanaofanyiwa wazee, iwe na watoto wao au watu wengine katika jamii.

Tusiruhusu kujenga taifa ambalo haliheshimu au kuthamini mchango uliotolewa na wazee na kuelewa kwamba kila anayewatendea maovu anapaswa kujua anajenga mazingira ya yeye naye kutafanyiwa hivyohivyo anapokuwa na umri mkubwa.

Wazee ni hazina ya nchi na inafaa kuenziwa na kutunzwa. Hadaa mbalimbali za ulimwengu zisipelekee kuitupa hazina hii adhimu kwani tukifanya hivyo tutakuja hapo baadaye kujutia haya tunayoyatenda hivi sasa.

Kila mmoja wetu aanze kuchukua hatua zinazofaa kwa kumtunza, kumuenzi na kumheshimu mzee wake na wa mwenzake.