Klabu za Unguja, Pemba kuamua hatma ya Ligi Kuu Zanzibar

Dar es Salaam. Viongozi wa klabu 28 kutoka Unguja na Pemba watakutana ili kupanga mikakati ya kuanza kwa mfumo mpya wa Ligi Kuu  Zanzibar kwenye Uwanja wa Gombani Pemba, kesho Jumamosi 

Msemaji wa Chama cha Soka Zanzibar(ZFA), Ally Bakari Cheupe amesema baada ya  Zanzibar kuwa mwanachama mpya wa Shirikisho la Soka Afrika(Caf), wanatakiwa kubadilisha uendeshaji wao wa ligi.

"Unajua zamani ligi ya Zanzibar ilikuwa inashirikisha timu 36, lakini  wakati rais wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Jamal Malinzi  anawasilisha maombi ya kutaka  Zanzibar iwe mwanachama wa Caf aliwasilisha kuwa ligi ya Zanzibar inashirikisha timu 12.

"Hivyo baada ya kupata uanachama inatakiwa tuhakikishe msimu ujao Ligi  Kuu ya Zanzibar inashirikisha timu 12 kama Caf wanavyotambua au tukishindwa msimu ujao basi msimu mwingine utakaofuata lazima tufanye hivyo," alisema Cheupe.

Aliongeza"Ndio maana hizo klabu zinakutana ili kufanya maamzimio ya mfumo gani uweze kutumika kuzipata hizo timu 12 zitakazoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar."

Cheupe alisema  watahudhuria mkutano huo kama waangalizi tu ili kupata  kujua mfumo upi utumike kuzipata timu 12 zitakazoshiriki Ligi Kuu Zanazibar.

"Kama wataamua tucheze Ligi ya Muungano ili kutafuta hizo timu 12 sawa, kama wataamua vingine, tutajua hiyo Jumamosi  kitu gani klabu hizo zitakubaliana"alisema Cheupe.