Rich Mavoko ‘ aitosa’ WCB

Thursday July 26 2018
mavoko pic

Rich Mavoko

Baada ya kutamba na nyimbo Kokoro, Sheri na Ibaki Stori  akiwa chini ya Lebo ya WCB, mwanamuziki Rich Mavoko  ameanza maisha mapya na wimbo wa ‘Happy’ ambao ameutoa takribani wiki moja iliyopita.

Katika kipindi cha miezi mitatu limekuwapo gumzo la mwanamuziki huyo kuondoka katika lebo hiyo inayoongozwa na mwanamuziki Diamond Platnumz.

Kutoka kimya kimya kwa wimbo huu, ambao hata hivyo Rich Mavoko ameufuta katika akaunti yake ni tofauti na taratibu za WCB.

Hayo yalifuatia kuwapo sintofahamu kati yake na yanayoendelea katika lebo hiyo inayowasimamia wanamuziki wengine kama Harmonize, Rayvanny, Mbosso, Queen Darlin na Lavalava.

Kukosekana kwa  Rich Mavoko katika promo za shoo mpya ya televisheni itakayoitwa The Real Life of Wasafi kuligongelea msumari wa mwisho kuwa huenda sasa rasmi mwanamuziki huyo ameondoka WCB.

Juni 19, mwaka huu wakati WCB wakitambulisha chaneli yao ya Wasafi kuingia katika king’amuzi cha Startimes, mmoja wa maneja wa kundi hilo Babu Tale alisema Rich Mavoko hakuonekana siku hiyo kwa sababu alikuwa akirekodi kazi yake mpya.

Advertisement

Hata hivyo, jana alimwambia mwandishi wa Mwananchi kuwa ukifika wakati sahihi watalizungumzia suala la Rich Mavoko iwapo ameondoka au la.

Naye Rich Mavoko alipotafutwa na Mwananchi alisema hawezi kulizungumzia hilo akimtaka mwandishi autafute uongozi wa WCB kwani wao ndio wana nafasi ya kulizungumzia.

“Sitaki kuulizwa kuhusu WCB, watafuteni wenyewe watawaambia,” alisema Rich Mavoko na kisha akakata simu.

 


Advertisement