Sugu ‘achana’ mistari ya Ana Miaka 18 bungeni

Muktasari:

Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ leo ametumbuiza kwa wimbo wake wa Ana Miaka 18, mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika Job Ndugai, Naibu Spika Tulia Ackson na wabunge mbalimbali ndani ya ukumbi wa zamani wa Bunge jijini Dodoma.Dar es Salaam. Mwanamuziki wa muziki wa kizazi kipya na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ leo ametumbuiza ndani ya ukumbi wa zamani wa Bunge jijini Dodoma, mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Spika Job Ndugai, Naibu Spika Tulia Ackson na wabunge wengine mbalimbali katika uzinduzi wa Mkakati na Mpango Kazi wa Kujumuisha Masuala ya Jinsia ndani ya Bunge.

Sugu alitumbuiza kwa wimbo wake wenye jina Ana Miaka 18 ambao amesema aliutunga zaidi ya miaka 20 iliyopita, baada ya kufanya utafiti na kubaini namna wasichana walivyokuwa wakinyanyasika kijinsia na kubaguliwa hali iliyopelekea pia wakajiingiza katika biashara haramu ya ngono.

Amesema kwa kuwa yeye si msomi, badala ya kupeleka matokeo ya utafiti wake huo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliamua kuwasilisha matokeo hayo kwa njia ya wimbo huo.

Mshereheshaji wa shughuli hiyo, alimtambulisha Sugu kwa kusema namleta kwenu msanii mkongwe, ambaye alikuwepo kwenye muziki miaka mingi, kabla hata ya Konki Masta Dudubaya na kwa sasa ni mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, atupatie burudani, hali iliyoinua shangwe kutoka kwa wabunge.

Sugu alitumia muda wake vizuri, kwa kutumbuiza wimbo huo wa miondoko ya Hip Hop na kuwainua wabunge mbalimbali waliopunga mikono na baadhi walijitokeza mbele na kumpa fedha na kumpongeza kwa wimbo huo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo, alipoanza kutoa hotuba yake alianza kwa kumpongeza Mbunge huyo kwa wimbo huo aliouita mzuri na wenye ujumbe kwa jamii.